Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Mchezo wa Kuteleza Kwenye Theluji Mashambani Unakufaa?

Je, Mchezo wa Kuteleza Kwenye Theluji Mashambani Unakufaa?

Je, Mchezo wa Kuteleza Kwenye Theluji Mashambani Unakufaa?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KANADA

MSEMO “LANGLÄUFER LEBEN LÄNGER” wamaanisha kwamba wale wanaoteleza kwenye theluji mashambani (watelezaji wa skii) huishi muda mrefu. Msemo huo wa Kijerumani unaojulikana sana unaonyesha kwa nini watu wengi wanapenda mchezo wa kuteleza kwenye theluji mashambani (skii) wakati wa majira ya baridi kali. Kwa kweli, katika nchi nyingi zinazopata theluji katika majira ya baridi kali, maeneo ya mashambani huwa na vijia vya kutelezea kwenye theluji. Katika nchi nyingine, mara nyingi kunakuwa na ishara zinazoonyesha umbali kati ya miji na vijiji, na vijia vingi vina taa zinazowasaidia watelezaji kuona njia wanapoenda na kutoka kazini kwa skii.

Mchezo wa kuteleza kwenye theluji sehemu za mashambani umekuwa maarufu sana katika sehemu nyingi ulimwenguni katika miaka ya karibuni ijapokuwa ni watu wachache sana walioucheza kabla ya miaka ya 1960. Watu fulani wanakadiria kwamba watu wapatao milioni nne hufurahia mchezo huo kila mwaka huko Amerika Kaskazini peke yake! Kwa nini unasisimua na kuvutia watu wengi? Kwa sababu ni mchezo rahisi na vifaa vyake havigharimu fedha nyingi. Mbinu fulani za kuteleza kwenye theluji eneo la mashambani si ngumu sana kama mbinu za kuteleza kwa mapindi kwenye theluji katika mabonde na milima. Yule anayeteleza kwenye theluji milimani anahitaji vifaa na mavazi maalumu ya gharama kubwa. Ni lazima asafiri hadi kwenye milima au vilima vya pekee vya mchezo huo. Na huenda akalazimika kulipa fedha nyingi ili kusafirishwa kwa lifti ya pekee hadi kileleni na pia kusubiri lifti hiyo kwa muda. Ni watu wachache sana wapya walio na ukakamavu unaohitajiwa ili kuteleza kwenye theluji milimani. Kwa upande mwingine, watu wa umri mbalimbali wanaweza kufurahia mchezo wa kuteleza kwenye theluji sehemu za mashambani. Vitu vinavyohitajiwa ni tabaka jembamba la theluji, vifaa vya kutelezea kwenye theluji vya bei nafuu, mabuti ya skii, fimbo za skii, na mazoezi kidogo.

Kuteleza kwenye theluji mashambani ni mchezo unaoweza kusisimua sana! Mtelezaji anaweza kwenda popote anapotaka—kuvuka viwanja na maeneo ya malisho, maziwa na vijito vilivyoganda, na kuingia katika misitu yenye utulivu na mabonde yaliyofunikwa na theluji. Mtelezaji anapata fursa ya kutafakari, kuwaza na kuwazua; ni pindi nzuri ya kuwasiliana na Muumba wetu na kumshukuru kwa ajili ya maajabu ya uumbaji. Majira ya baridi kali hutokeza mandhari ya pekee sana ya uumbaji wa Yehova Mungu. Mandhari inayong’aa ya theluji inatokeza hali ya utulivu. Dunia yaonekana ikiwa safi na mpya kana kwamba inahitaji kuvumbuliwa. Mtu anapopita msituni, anatulia moyoni na akilini anapotazama miti iliyofunikwa na utando wa theluji. Hakuna hekaheka za kawaida, sauti pekee inayosikika ni mvumo wa vifaa vya kutelezea thelujini.

Tafrija ya kuteleza kwenye theluji huunganisha na kuimarisha uhusiano wa washiriki wa familia au marafiki. Siku hizi, katika nchi nyingi za kaskazini mwa Ulaya, familia fulani husafiri umbali wa kilometa 20 au 30 kwa treni kisha huteleza pamoja kwenye theluji hadi nyumbani.

Mwanzo wa Mchezo Huo

Huenda wengine wakafikiri kwamba mchezo wa kuteleza kwenye theluji sehemu za mashambani ulianza hivi majuzi, lakini sivyo ilivyo. Mnamo mwaka wa 1927, michongo iliyo kwenye miamba iliyodumu kwa maelfu ya miaka ilipatikana kwenye kisiwa cha Rødøya huko Norway. Mchoro mmoja unaonyesha mwindaji aliyevalia kinyago chenye umbo la sungura. Ni kana kwamba anateleza kwenye theluji kwa jozi ya mbao ndefu za skii. Hivi majuzi, wafanyakazi waligundua mamia ya skii za kale ambazo hazijachakaa katika vinamasi vya Skandinavia. Kuteleza kwenye theluji kulikuwa njia muhimu ya usafiri ya wakazi wa kale wa Norway katika majira marefu yenye theluji na baridi kali. Kulikuwa muhimu sana maishani mwao hivi kwamba hata waliabudu na kumheshimu mungu wa kiume na mungu wa kike wa mchezo wa kuteleza kwenye theluji! Leo majina ya miji na vijiji vingi nchini Norway na Sweden yanahusiana na imani hizo za kale za kipagani. Hata jina Skandinavia laweza kurejezea Skade, mungu wa kike wa wale wanaoteleza kwenye theluji.

Ingawa kuteleza kwenye theluji kumekuwa muhimu sana kwa wakazi wa Norway kwa karne nyingi, mchezo huo ulipata kuwa mchezo wa kimataifa katika karne ya 19 tu. Wakati huo wakazi wa Norway waliboresha vifaa vyao vya kale vya kutelezea kwenye theluji. Waliboresha umbo na kupunguza unene wa vifaa hivyo. Walibuni pia mikanda inayoshika visigino na vidole vya miguu kwenye ubao wa kutelezea. Mikanda hiyo imeboreshwa katika nyakati za kisasa. Muda si muda, walianzisha mashindano ya kuteleza kwenye theluji huko Telemark, eneo lenye milima upande wa kusini ya kati ya Norway. Yaaminika kwamba mashindano ya kwanza kabisa ya kuteleza kwenye theluji yalifanywa huko. Mshindi alisafiri umbali wa kilometa tano kwa muda wa dakika 30 hivi. Muda mfupi baadaye, mchezo wa kuteleza kwenye theluji ukaja kupendwa sana katika nchi za kaskazini mwa Ulaya. Lakini mchezo huo ulienea ulimwenguni baada ya tukio jingine.

Mwaka wa 1888, mvumbuzi wa kutoka Norway Fridtjof Nansen aliongoza kikundi cha uvumbuzi kupitia Greenland kwa kuteleza kwenye theluji. Aliandika kitabu kuhusu safari yake ya uvumbuzi. Kitabu hicho kilitafsiriwa katika Kiingereza, Kifaransa, na Kijerumani mnamo mwaka wa 1891. Kitabu hicho kinachosimulia safari hiyo ngumu ya kuvuka eneo lenye theluji na barafu la Aktiki, kiliwavutia sana wasomaji wa Uingereza. Kilichochea hamu yao ya kutembelea eneo hilo kubwa lililo ukiwa.

Katika miaka ya 1960, safari za familia kutalii kwa kuteleza kwenye theluji zilianzishwa kotekote. Vituo vya mchezo wa kuteleza kwenye theluji ambavyo vilikazia hasa kuteleza katika maeneo ya mashambani vilianza kuibuka. Watengenezaji wa vifaa vya michezo walipoona hivyo, walibuni vifaa vipya vya mchezo huo vilivyokuwa tata zaidi. Mchezo wa kuteleza kwenye theluji mashambani ulivutia hata zaidi kwa sababu vifaa vya kisasa vilibuniwa. Mabaraza ya miji yalijitahidi kutengeneza vijia vya kuteleza kwenye theluji katika mabustani, viwanja vya gofu na sehemu nyinginezo kwa sababu ya kushinikizwa na umma.

Faida za Kiafya

Mchezo wa kuteleza kwenye theluji unaonwa kuwa miongoni mwa michezo maarufu iliyo salama zaidi. Ingawa mtu anaweza kupata majeraha madogo anapoanguka, ni vigumu sana kujeruhiwa vibaya. Na mara nyingi mtelezaji hujeruhiwa vibaya anapoteleza kwenye theluji katika milima mirefu na katika mabonde.

Mwili wa mchezaji hunyumbulika kwa wepesi sana na taratibu, na hivyo viungo na misuli haiumii wala kushtuka kupita kiasi. Mara nyingi madaktari wanaotibu wanamichezo hupendekeza kwamba wakimbiaji au waendeshaji-baiskeli waliojeruhiwa wateleze kwenye theluji ili kupata nafuu. Ni mojawapo ya michezo michache inayochochea misuli yote mwilini na hivyo kuuzoeza kikamili mwili wa mchezaji. Moyo na mapafu hupata manufaa sana, na watelezaji wenye bidii kwa kawaida huwa na msukumo wa damu na mpigo wa moyo ulio chini kuliko watu wasiofanya mazoezi. Hivyo, wale wanaoteleza kwenye theluji mashambani huonwa kuwa miongoni mwa wanariadha bora sana ulimwenguni.

Mchezo wa kuteleza kwenye theluji unawafaa wazee-wazee kwa sababu si rahisi kujeruhiwa na pia mwili hunyumbulika kwa wepesi na kwa utaratibu. Katika nchi fulani za kaskazini mwa Ulaya, ni kawaida kuona wazee-wazee wakiteleza kwenye theluji.

Mchezo huo hutokeza joto jingi mwilini, hivyo basi mtu hustarehe wakati wa baridi. Siku zenye baridi kali, wale wanaoshiriki mashindano ya kuteleza kwenye theluji kwa kawaida huvalia nguo nyepesi, na mara nyingi hawavai glovu mikononi. Hata hivyo, wachezaji wasio na ujuzi wanahitaji kujifunika miguu na mikono ifaavyo kwa sababu ya baridi kali. Kwa kawaida mashabiki wa mchezo huo huvalia nguo nyingi. Kwanza, wanavaa nguo za sufu au sanisia, halafu wanavaa mavazi yasiyopenya maji, kisha nguo nzito za baridi. Mavazi hayo huwasaidia kustarehe na kudumisha joto mwilini. Wao huvua au kuvalia nguo zaidi ihitajiwapo. Wazazi wenye hekima wanapaswa kuhakikisha kwamba watoto wao wamevaa nguo zifaazo, kwani baridi huathiri watoto zaidi ya watu wazima. Kwa kuwa miili ya watoto hupoteza joto haraka sana kupitia ngozi wanaweza kuganda mwili kwa urahisi sana.

Fanya Majira ya Baridi Kali Yapendeze Zaidi

“Kama unaweza kutembea, basi unaweza kuteleza kwenye theluji.” Wachezaji wanaoteleza kwenye theluji husema hivyo kwa kawaida kwa sababu mwili hunyumbulika kama wakati wa kutembea. Ingawa msemo huo ni wa kweli kwa kadiri fulani, wengi wetu tunaweza kuwa stadi zaidi tukifundishwa kwa saa moja au mbili na mwalimu mwenye ujuzi. Vituo vya mchezo huo hufundisha watu mmoja-mmoja au kikundi cha watu, na baada ya muda mfupi, mwanafunzi hufahamu mambo ya msingi ya mchezo huo, kama vile, kuteleza kwenye maeneo tambarare, kupanda na kushuka milimani na kusimama! Watu wengi huwa tayari kuteleza kwenye theluji mara tu baada ya kufundishwa mambo hayo ya msingi.

‘Hakuna kitu kingine chochote kinachoweza kuimarisha misuli na kuufanya mwili unyumbulike na kuwa na nguvu kuliko mchezo wa kuteleza kwenye theluji,’ ndivyo alivyosema Fridtjof Nansen mnamo mwaka wa 1890 kuhusu mchezo wa kuteleza kwenye theluji eneo la mashambani. Huenda hata wewe ukafurahia mchezo huo. Huenda ukafanya majira ya baridi kali yapendeze zaidi.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mchezo wa kuteleza kwenye theluji mashambani haugharimu fedha nyingi, na unaweza kufurahiwa na watu wa umri mbalimbali

[Picha katika ukurasa wa 26]

Vifaa vya kale vya kutelezea kwenye theluji vilivyopatikana huko Voss, Norway

[Hisani]

Picha: © Universitetets kulturhistoriske museer, Eirik Irgens Johnsen

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mchongo ulio kwenye mwamba unaonyesha mchezaji akiteleza kwenye theluji

[Hisani]

Picha: Inge Ove Tysnes / Syv søstre forlag