Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Fahari Iliyosahaulika ya Milki ya Byzantium

Fahari Iliyosahaulika ya Milki ya Byzantium

Fahari Iliyosahaulika ya Milki ya Byzantium

KATIKA LUGHA FULANI NENO “BYZANTINE,” HUTUMIWA KUMAANISHA NJAMA, USIRI, NA UHAINI. HATA HIVYO, SI WATU WENGI WANAOJUA KWAMBA KIVUMISHI HICHO KILIKUWA JINA LA MILKI KUBWA ILIYOSITAWI KWA MUDA WA KARNE 12 HIVI.

MILKI ya Byzantium ilipofikia kilele cha usitawi, ilienea kutoka Caucasus hadi Atlantiki, kutoka Crimea hadi Sinai, kutoka Danube hadi Jangwa la Sahara. Wanahistoria wengi wanasema kwamba ilidumu kuanzia karne ya 4 hadi karne ya 15 W.K. Mbali na kuhifadhi utamaduni wa Ugiriki na Roma, milki hiyo ilichangia sana kuenea kwa Ukristo bandia. Kanuni za kisiasa, kijamii, na kidini ambazo zimedumu hadi leo zilibuniwa na kuratibiwa katika milki hiyo.

Lakini, milki hiyo yenye nguvu ilianza kwa njia ya kawaida tu. Kihistoria, Milki ya Byzantium ilitokana na Milki ya Roma huko Mashariki. Tarehe ya kuanza kwa milki hiyo ingali inabishaniwa. Wanahistoria fulani wanasema kwamba mfalme wa kwanza wa Byzantium alikuwa Diocletian (karibu 245–316 W.K.); wengine wanasema Konstantino Mkuu (karibu 275-337 W.K.); na wengine wanasema alikuwa Justinian wa Kwanza (483-565 W.K.). Hata hivyo, wengi wanakubali kwamba Milki ya Byzantium ilianza kuwa maarufu wakati Mfalme Konstantino alipohamisha jiji kuu la milki yake kutoka Roma hadi Byzantium mwaka wa 330 W.K. Aliliita jiji hilo Constantinople (leo ni Istanbul), kutokana na jina lake.

Inashangaza kwamba wala watawala wala raia wa milki hiyo hawakujiita kamwe Wabyzantium. Walijiona kuwa Waroma, au Waromaioi. Neno “Byzantine” lilianza kutumiwa baada ya karne ya 14.

Jiji Kuu Lenye Fahari

Mwanahistoria mmoja anasema Constantinople la kale lilikuwa jiji “maarufu sana lenye ufanisi.” Jiji la Constantinople lililokuwa kati ya Ulaya na Asia—katika Mlango-Bahari wa Bosporus—lilizingira rasi salama na bandari yenye ulinzi, iliyoitwa Golden Horn. Katika mwaka wa 657 K.W.K., walowezi Wagiriki waliliita jiji hilo Byzantium kutokana na jina la kiongozi wao mashuhuri Byzas. Baada ya karne kumi kupita, jiji hilo lilionwa kuwa Roma Mpya. Lilikuwa na wakazi wapatao nusu milioni lilipofikia kilele cha ustawi kati ya karne ya 6 na ya 11 W.K.

Watalii kutoka nchi za Magharibi walistaajabia jiji hilo kuu lililokuwa kituo muhimu cha kibiashara ulimwenguni. Bandari yake ilijaa mashua. Hariri, manyoya ya wanyama, johari, mbao zenye uturi, pembe za ndovu zilizochongwa, dhahabu, fedha, vito vilivyopakwa enameli, na vikolezo viliuzwa masokoni. Ndiyo sababu jiji la Constantinople lilionewa wivu na mataifa mengine yenye nguvu hivi kwamba yalijaribu tena na tena kulivamia. Kabla ya kushindwa na Uturuki mwaka wa 1453, maadui walifaulu kuvamia jiji hilo mara moja tu—yaani, “Wakristo” wa Krusedi ya Nne. Mpiganaji wa kidini Robert wa kutoka Clari alisema kwa mshangao kwamba “tangu ulimwengu kuumbwa hazina kubwa hivyo haijawahi kuwapo kamwe wala kupatikana.”

Matokeo Yenye Kudumu

Amini usiamini, serikali ya Byzantium, sheria, mafundisho yake ya kidini, na sherehe zake za kifahari zingali zinaathiri mabilioni ya watu leo. Kwa mfano, kanuni mashuhuri za kisheria za Justinian zilizoitwa Corpus Juris Civilis (Mkusanyo wa Sheria za Kiraia) zilikuja kuwa msingi wa sheria za Roma katika bara la Ulaya leo. Mfumo wa Sheria wa Napoléon ulisambaza sheria za Byzantium huko Amerika Kusini na katika nchi nyingine, ambako zingali zinatumika.

Zaidi ya hayo, wasanifu-ujenzi wa Byzantium walijifunza jinsi ya kujenga kuba kubwa juu ya majengo yenye umbo la pembe nne. Mtindo huo wa ujenzi ulienea hadi Urusi. Watu fulani hata wanasema kwamba watu wa Byzantium ndio walioanza kula kwa kutumia uma. Binti mmoja wa mfalme wa Byzantium aliyeishi katika karne ya 11 alikula kwa uma wenye meno mawili badala ya kula kwa vidole vyake huko Venice. Watazamaji walipigwa na butwaa! Hata hivyo, karne nyingi baadaye matajiri walianza kula kwa uma. Mapapa wa Roma pia waliathiriwa na uvutano wa Byzantium, walivalia taji lililofanana na taji la mfalme wa Byzantium. Wafalme wa Uingereza pia waliiga nembo na fimbo ya mfalme wa Byzantium.

Sheria na Utaratibu

Sera nyingi za kiserikali zinazovutia za Milki ya Byzantium zingalipo leo. Kwa mfano, watu maskini waliajiriwa madukani na katika makampuni ya serikali ya kuoka mikate. “Uzembe husababisha uhalifu,” ndivyo alivyoamini Mfalme Leo wa Tatu (karibu 675-741 W.K.). Mabaa yalifungwa saa 2 usiku kwa sababu ilidhaniwa kwamba ulevi ulitokeza vurugu na uchochezi. Gazeti la National Geographic Magazine linasema kwamba “mtu aliyehusika na ngono ya maharimu, uuaji, kutengeneza au kuuza kisiri mavazi ya zambarau (yaliyotumiwa na wafalme peke yao) au kuwafundisha maadui kutengeneza meli angeweza kukatwa kichwa, kutundikwa mtini au kuzamishwa majini akiwa katika gunia lenye nguruwe, jogoo, nyoka wa kipiri, na nyani. Mwuza-mboga aliyewaibia wateja alikatwa mkono. Wale walioteketeza mali ya wengine kimakusudi walichomwa moto.”

Inapendeza kwamba Milki ya Byzantium iliandaa huduma za jamii kuanzia utotoni hadi uzeeni kama ilivyo katika nchi zinazoandaa huduma za jamii leo. Wafalme na raia matajiri walijitoa mhanga kuchanga pesa za kudumisha hospitali, makao ya kuwatunza maskini na mayatima. Kulikuwa na makao ya wanawake walioacha ukahaba—baadhi yao wakaja kuwa “watakatifu.” Hata kulikuwa na makao ya kuwasaidia wanawake wenye shida wa jamii ya kifalme.

Milki Iliyositawishwa na Biashara

Ukarimu huo ulionyesha ufanisi wa milki hiyo. Serikali ilidhibiti bei za bidhaa, mishahara, na kodi. Ngano ilihifadhiwa katika maghala ili itumiwe wakati wa njaa. Maofisa walikagua maduka na mizani zilizotumiwa, vitabu vya hesabu, na ubora wa bidhaa. Watu walioficha bidhaa, wafanya-magendo, walaghai, waghushi, na wasiolipa ushuru waliadhibiwa vikali.

Mfalme alikuwa mfanyabiashara na mtengenezaji-bidhaa mashuhuri katika milki hiyo. Alikuwa na haki ya pekee ya kutengeneza sarafu, silaha, na bidhaa maridadi maarufu za Byzantium. Justinian ndiye aliyeanzisha kiwanda maarufu cha hariri katika milki hiyo. Hariri hiyo ilitokana na mayai ya nondo wa hariri walioletwa kimagendo kutoka China.

Huduma za bima na mikopo zilianzishwa pia. Hesabu za benki zilikaguliwa kwa uangalifu sana. Sarafu ya dhahabu iitwayo solidus, ambayo ilibuniwa na Konstantino, iliendelea kuwa na thamani kwa muda wa karne kumi! Ndiyo sarafu iliyokuwa imara zaidi katika historia yote.

Nyumba ya Kifalme ya Byzantium

Basi neno, “Byzantine,” lilihusianishwaje na njama, usiri, na uhaini? Mwanahistoria William Lecky anasema kwamba katika nyumba ya kifalme ya kuvutia ya Byzantium mlikuwa na “visa chungu nzima vya njama za makasisi, matowashi, na wanawake, visa vya watu waliouawa kwa sumu, vya uhaini, utovu wa shukrani, na visa tele vya watu waliowaua ndugu zao.”

Mwandishi Merle Severy asema hivi: ‘Mfalme asiyefaa hangeruhusiwa kuendelea kuwa mwakilishi wa Mungu duniani. Aliondolewa mara moja au kuuawa na watu waliotaka kujitwalia uongozi. Wafalme 13 kati ya 88 waliotawala kuanzia kwa Konstantino wa 1 hadi wa 11, walikimbilia kwenye makao ya watawa. Wafalme wengine 30 waliuawa kikatili—walikufa njaa, walitiliwa sumu, walipofushwa, walipigwa rungu, walinyongwa, walichomwa kisu, walikatwa viungo vya mwili, na kukatwa vichwa. Fuvu la Nicephorus wa Kwanza lilirembwa kwa fedha na kutumiwa na Khan Krum, kiongozi wa kundi la Bulgars, kama bilauri la kuwatakia heri watu wake wenye cheo.’

Hata Konstantino Mkuu aliyeonwa kuwa “mtakatifu” aliagiza mwanaye mkubwa auawe na mkewe anyongwe alipokuwa akioga. Mfalme wa kike aitwaye Irene (karibu 752-803 W.K.) alishikilia mno mamlaka hivi kwamba aliamuru mwanaye apofushwe na akachukua cheo chake cha mfalme.

Kuporomoka kwa Milki Hiyo

Milki hiyo haikuporomoka kwa sababu za kisiasa. Nchi za Ulaya Magharibi zilianza kubadilika kwa sababu ya Harakati za Kuboresha Elimu, Marekebisho Makubwa ya Kidini, Harakati za Kifalsafa na vilevile kutokea kwa sayansi. Hata hivyo, mabadiliko yoyote katika milki ya Byzantium yalionwa kuwa uzushi na uhalifu dhidi ya Serikali.

Zaidi ya hayo, mabadiliko makubwa ya kisiasa yalianza kuleta madhara. Katika karne ya saba, Uislamu ulienea katika Antiokia, Yerusalemu, na Aleksandria. Jiji la Roma lilitenganishwa na Constantinople wakati Waslavia walipovamia Balkani na wakazi wa Lombard kushinda Italia. Roma ilipokosa utegemezo wa Byzantium, ilijiunga na nchi za Magharibi zenye nguvu zilizozungumza Kijerumani. Kigiriki kilianza kutumiwa sana katika milki ya Constantinople iliyokuwa ikiporomoka. Kisha, mnamo mwaka wa 1054, askofu mkuu wa Kanisa Othodoksi la Ugiriki na papa wa Kanisa Katoliki walikosana kwa sababu ya tofauti fulani za kidini. Hilo lilisababisha uadui kati ya Kanisa Othodoksi na Katoliki na umeendelea hadi leo.

Milki hiyo ilikumbwa na matatizo makubwa zaidi mwaka wa 1204. Mnamo Aprili 12, wapiganaji wa Krusedi ya Nne walipokuwa wakielekea Yerusalemu walifanya kile kilichoitwa na mwanahistoria Bwana Steven Runciman, “uhalifu mkubwa zaidi katika historia”—waliteka na kupora jiji la Constantinople. Wapiganaji hao waliteketeza mali, wakapora, na kuwabaka watu kwa jina la Kristo, waliharibu jiji hilo na kupeleka mali waliyopora huko Venice, Paris, Turin, na sehemu nyinginezo katika nchi za Magharibi.

Miaka 50 ilipita kabla ya Constantinople kutwaliwa mwishowe na watu wa Byzantium. Wakati huo milki hiyo ilikuwa imedhoofika kabisa. Biashara ya milki hiyo ilidhibitiwa na wenyeji wa Venice na wa Genoa. Na muda si muda, Milki ya Byzantium ilishambuliwa na Waislamu wa Uturuki.

Milki hiyo ilianguka kabisa hatimaye kwa sababu ya mashambulizi hayo. Katika Aprili 11, 1453, Sultan Mehmed wa Pili aliuzingira mji mkuu, akitumia wanajeshi 100,000 na kundi kubwa la manowari. Wanajeshi 8,000 tu waliokuwa wakilinda Constantinople walishindwa baada ya majuma saba. Kisha, mnamo Mei 28, wavamizi wengi walipenya bandari yake isiyo na ulinzi mkali kupitia handaki la maji la jiji hilo. Kwa siku moja tu, jiji hilo lilikuwa mikononi mwa mtawala mwingine. Yasemekana kwamba Mehmed, aliyeshinda jiji hilo, alilia machozi na kuomboleza hivi: “Tumepora na kuharibu jiji zuri kama nini!” Milki ya Byzantium ilikuwa imeshindwa. Lakini athari zake zingalipo leo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 13]

MILKI YA BYZANTIUM NA BIBLIA

Mfumo wa utawa ulikuwa mojawapo ya mifumo ya kidini iliyokita mizizi katika milki hiyo. Makao ya watawa yalitumiwa kuwa vituo vya kunakili na kuhifadhi maelfu ya hati za Biblia. Hati tatu kati ya hati kamili zaidi na zilizo muhimu sana zilizopo leo, yaani, hati ya Biblia ya Vatican 1209, Sinaitic (katika picha ndogo), na Alexandrine (picha iliyo nyuma)—huenda zilinakiliwa au kuhifadhiwa katika makao ya watawa na katika nyumba za kidini za Byzantium.

[Hisani]

Hati zote mbili: Photograph taken by courtesy of the British Museum

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]

DINI KATIKA MILKI YA BYZANTIUM

Akizungumzia uhusiano wa karibu uliokuwapo kati ya Kanisa na Serikali, Norman Davies aandika hivi katika kitabu chake Europe—A History: “Serikali na kanisa zilikuwa kitu kimoja. Mfalme . . . na Askofu Mkuu walionwa kuwa nguzo za kisiasa na kidini waliopewa mamlaka na Mungu. Milki hiyo ilitetea Kanisa Othodoksi, nalo kanisa liliisifu Milki hiyo. Uhusiano huo wa kanisa na serikali haukuwa na kifani katika nchi za Magharibi.”

[Picha]

Jumba la Hagia Sophia, Istanbul —wakati mmoja lilikuwa kanisa kubwa zaidi la Byzantium, likafanywa msikiti mwaka wa 1453 kisha jumba la ukumbusho mwaka wa 1935

[Chati katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

MATUKIO MUHIMU

286 Diocletian aanza kutawala huko Nicomedia, Asia Ndogo

330 Konstantino afanya Byzantium kuwa jiji kuu la milki hiyo, na kuliita Constantinople

395 Milki ya Roma yagawanywa kabisa na kuwa na sehemu ya Mashariki na Magharibi

1054 Mfarakano wa kidini watenganisha Kanisa Othodoksi la Ugiriki na Kanisa Katoliki

1204 Wapiganaji wa Krusedi ya Nne wavamia na kupora Constantinople

1453 Constantinople na milki yote yashindwa na Waturuki

[Ramani katika ukurasa wa 12]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

BAHARI NYEUSI

CONSTANTINOPLE

Nicomedia

Nicaea

Efeso

Antiokia

Yerusalemu

Aleksandria

BAHARI YA MEDITERANIA

Eneo jeusi laonyesha milki hiyo ilipofikia kilele cha ufanisi (527-565 W.K.)

[Picha katika ukurasa wa 12]

Wasomi wabishana iwapo mfalme wa kwanza wa Byzantium alikuwa (1) Diocletian, (2) Konstantino mkuu, au (3) Justinian wa I

[Hisani]

Musée du Louvre, Paris ▸

[Picha katika ukurasa wa 15]

Picha iliyo kwenye hati inaonyesha Constantinople likiwa limezingirwa mwaka wa 1204

[Hisani]

© Cliché Bibliothèque nationale de France, Paris

[Picha katika ukurasa wa 15]

Sarafu ya dhahabu iitwayo solidus, mwaka wa 321 W.K., yaonyeshwa ikiwa imetiwa katikati ya mkufu

[Hisani]

Photograph taken by courtesy of the British Museum