Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Nani Atakayelisha Ulimwengu?

Ni Nani Atakayelisha Ulimwengu?

Ni Nani Atakayelisha Ulimwengu?

JE, WANADAMU wataanza kuhifadhi aina mbalimbali za mimea badala ya kuziangamiza? Mwanabiolojia John Tuxill asema kwamba ili wafaulu watahitaji “kubadili sana sera zao.” Hata hivyo, aongezea kwamba mabadiliko hayo “huenda yasitukie iwapo watu hawataelimishwa kuhusu manufaa ya jamii mbalimbali za mimea, au iwapo hawatakuwa tayari kubadili mbinu za kilimo wanazotumia leo, na kujaribu mbinu mpya.”

Wengi hawaamini kwamba mabadiliko hayo makubwa yatatukia. Na wengi hupinga mkataa wa Tuxill. Wanasayansi fulani wa mazingira wanaona kwamba bado watu hawaelewi umuhimu wa kukuza mimea mbalimbali, na kwamba huenda wanasayansi wenzao wanapotosha mambo. Hata hivyo, huku wanasayansi wakijadili suala hilo, yamkini inafaa kuzingatia malalamiko ya wataalamu wa kilimo. Yaonekana wana wasiwasi, si kwa sababu tu ya kutoweka kwa mimea mbalimbali bali pia kwa sababu hasara hiyo inasababishwa na pupa na kutofikiria hali ya wakati ujao. Hebu angalia maelezo yafuatayo kutoka kwa waandishi mbalimbali.

‘Karne moja tu iliyopita, mamia ya mamilioni ya wakulima kotekote duniani, walikuwa na hifadhi zao wenyewe za mbegu. . . . Leo, kiasi kikubwa cha mbegu hizo zimebadilishwa maumbile, na kampuni za kimataifa zimepata idhini maalumu ya kuhifadhi mbinu hizo. . . . Kwa kufikiria faida watakazopata sasa, makampuni ya biotekinolojia yanahatarisha sehemu muhimu za chembe za urithi ambazo huenda siku moja zikalinda mimea isiathiriwe na ugonjwa mpya sugu au na wadudu fulani sugu.’—Mwandishi wa sayansi Jeremy Rifkin.

“Vyombo vya habari vinakazia tena na tena kwamba mambo muhimu yanayopasa kuzingatiwa kwanza ni soko, biashara huru na uchumi wa ulimwenguni pote. Mara nyingi maoni hayo ya kiuchumi hufuatwa bila kupingwa kwa sababu vyombo vya habari hukazia hasa ufanisi na masilahi ya makampuni makubwa.”—Mtaalamu wa Chembe za Urithi David Suzuki.

Katika kitabu chake Seeds of Change—The Living Treasure, mwandishi Kenny Ausubel asema kwamba ni unafiki kwa ‘serikali na mashirika ya nchi zilizositawi kusikitikia hatari inayokabili ulimwengu wote ya kutoweka kwa desturi ya kawaida ya kuhifadhi chembe mbalimbali za urithi.’ Yeye asema kwamba serikali hizo zinahatarisha pia ukuzaji wa mimea mbalimbali kwa kusitawisha mbinu za kisasa za kilimo na ukuzaji wa mimea ya aina moja.

Iwe wanamazingira wana sababu nzuri za kuwa na wasiwasi au la, huenda ikawa vigumu kwako kuwa na uhakika kuhusu wakati ujao wa dunia. Je, dunia itadumu kwa muda mrefu kadiri gani ilhali inaonekana kwamba wanadamu wanachochewa na pupa? Watu wengi wanatumaini kwamba sayansi itasuluhisha mambo.

Je, Sayansi na Tekinolojia Zinaweza Kutuokoa?

Hivi majuzi shirika la Royal Society of Edinburgh lilisema kwamba linahangaishwa na maendeleo mengi ya kisayansi ambayo ni tata sana hivi kwamba huenda wanasayansi wasielewe kikamili matokeo ya maendeleo hayo. “Sayansi inafunua mambo machache sana kuhusu ulimwengu wa asili,” akaandika David Suzuki. ‘Hatujui jambo lolote kuhusu maumbile ya mimea na wanyama, sembuse kujua uhusiano uliopo kati yao na jinsi wanavyotegemeana.’

Gazeti Science lilieleza kwamba ‘hatari na manufaa za Mimea na Wanyama Waliobadilishwa Maumbile hazijulikani. . . . Hatuwezi kutabiri kwa usahihi jinsi mimea na wanyama hao wapya watakavyoathiri mazingira.’

“Maendeleo” mengi yamekuwa na manufaa na madhara. Yana faida fulani, lakini pia yanaonyesha kwamba wanadamu hawana hekima na mara nyingi huchochewa na pupa. (Yeremia 10:23) Kwa mfano, ingawa harakati za kuboresha uzalishaji zilitokeza chakula tele kwa watu, zilichangia pia kutoweka kwa ukuzaji wa mimea mbalimbali. Kwa kukazia mno matumizi ya dawa za kuua wadudu-waharibifu na mbinu nyingine ghali mno za kilimo, harakati za kuboresha uzalishaji mwishowe ziliwafaidi “matajiri na mashirika ya kilimo katika nchi zinazositawi na kuwaumiza watu wa kawaida,” akaandika Dakt. Mae-Wan Ho. Hali hiyo inaenea kwa sababu kilimo kinachotegemea biotekinolojia kinazidi kusambaa na kutia mizizi. Muda si muda tutaanza kutegemea chakula kinachokuzwa kisayansi.

Hata hivyo, matatizo hayo hayapaswi kutukatisha tamaa. Yanathibitisha tu jambo moja muhimu. Biblia inatufahamisha kwamba hatupaswi kutarajia wanadamu wasiokamilika, ambao sasa wanasimamia dunia na mali yake ya asili wasuluhishe mambo. Kwa kweli, kwa sasa mwanadamu hawezi kusimamia dunia. Ndiyo sababu Zaburi 146:3 inashauri hivi: “Msiwatumainie wakuu, wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake.” Lakini tunaweza kumtumaini Mungu kabisa. (Mithali 3:5, 6) Yeye anataka na anaweza kutusaidia.—Isaya 40:25, 26.

Karibuni Dunia Itasitawi na Kunawiri

Huenda ukahitaji kuondoa takataka katika nyumba iliyochakaa kabla hujaanza kuirekebisha. Vivyo hivyo, karibuni Yehova Mungu ataondoa uovu wote duniani, kutia ndani wale wanaotumia dunia yetu, mali zake za asili, na hata kuwakandamiza wanadamu wenzao ili kujifaidi na kufaidi mashirika yao. (Zaburi 37:10, 11; Ufunuo 11:18) Lakini Yehova atawaokoa wote wanaompenda na wanaojitahidi kufanya mapenzi yake.—1 Yohana 2:15-17.

Kisha, dunia na viumbe wote, kutia ndani wanadamu watiifu, wataongozwa na serikali iliyosimamishwa na Mungu—Ufalme wa Kimesiya. (Danieli 7:13, 14; Mathayo 6:10) Dunia itasitawi kama nini chini ya utawala huo wenye hekima! Zaburi 72:16 yasema: “Na uwepo wingi wa nafaka katika ardhi juu ya milima.” Naam, hakutakuwa na ubishi wala wasiwasi tena kwa sababu ya chakula. Badala yake, chakula kitakuwa tele na salama.

Kwa hiyo hali ya mfumo huu wa mambo izidipo kuzorota na kukatisha tamaa, wale wanaomtumaini Yehova wanaweza kutazamia wakati ujao mtukufu papa hapa duniani. Tumaini hilo ni sehemu ya “habari njema za ufalme,” ambazo Mashahidi wa Yehova wanahubiria wote wanaotaka ulimwengu bora na wenye haki zaidi. (Mathayo 24:14) Hata sasa tunaweza ‘kukaa salama, na kutulia bila kuogopa mabaya’ kwa sababu ya tumaini hilo hakika, na kwa sababu ya jinsi ambavyo Mungu akiwa baba anawatunza watu wake.—Mithali 1:33.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Chini ya Ufalme wa Mungu, chakula kitakuwa tele na salama

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]

FAO Photo/K. Dunn

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]

◀ Tourism Authority of Thailand