Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Mwanadamu Anasababisha Upungufu wa Chakula?

Je, Mwanadamu Anasababisha Upungufu wa Chakula?

Je, Mwanadamu Anasababisha Upungufu wa Chakula?

“Tatizo linalotukabili leo [si] madeni na upungufu wa fedha wala si mashindano ya ulimwenguni pote lakini tatizo ni kuishi maisha mazuri na yenye kusudi bila kuharibu dunia yetu na mazingira yanayotegemeza vitu vyote vilivyo hai. Wanadamu hawajawahi kamwe kukabili tisho kama hili: yaani, kutokomea kwa vitu vinavyoendeleza uhai wetu.”—Mtaalamu wa Chembe za Urithi David Suzuki.

NI RAHISI sana kupuuza tunda linaloitwa tofaa. Ikiwa unaishi sehemu inayokuza matofaa kwa wingi, huenda ukafikiri kwamba ni rahisi sana kupata matofaa, na hata unaweza kupata matofaa ya aina mbalimbali. Lakini je, ulijua kwamba kuna aina chache sana za matofaa leo kuliko zilivyokuwa miaka 100 iliyopita?

Kati ya mwaka wa 1804 na 1905, aina 7,098 za matofaa zilikuzwa nchini Marekani. Leo, aina 6,121 kati yake—yaani asilimia 86—zimetokomea. Ndivyo ilivyo na mapea. Sasa, asilimia 88 hivi ya jamii 2,683 za mapea zimetokomea. Na idadi kubwa zaidi ya mboga mbalimbali zimetokomea. Aina mbalimbali ya mimea na wanyama inatokomea na hiyo inatia ndani aina mojamoja ya wanyama na mimea katika jamii ileile. Ukuzaji wa jamii mbalimbali za mboga nchini Marekani umepungua kwa asilimia 97 kwa muda usiozidi miaka 80! Lakini je, kweli ni muhimu kuwa na aina mbalimbali za mimea na wanyama?

Wanasayansi wengi wanasema kwamba ni muhimu. Ijapokuwa umuhimu wa usitawishaji wa aina mbalimbali za mimea na wanyama unabishaniwa, wataalamu kadhaa wa mazingira wanasema kwamba ni muhimu kwa uhai duniani. Wanasema kwamba ni muhimu kuwa na mimea mbalimbali ya mazao, vilevile mimea ya msituni na ile inayokua mbugani. Ni muhimu pia kusitawisha aina mbalimbali ya mimea na wanyama walio katika jamii ileile. Kwa mfano, kunapokuwa na aina mbalimbali za mpunga kunakuwa na uwezekano mkubwa kwamba baadhi yake zitaweza kukinza magonjwa ya kawaida. Hivi majuzi, makala iliyochapishwa na Taasisi ya Worldwatch ilisema kwamba upungufu wa chakula ndilo jambo pekee linaloweza kuwaonyesha wanadamu hatari ya kuangamiza mimea ya jamii mbalimbali.

Kutokomea kwa mimea kunaweza kuathiri mimea ya mazao angalau kwa njia mbili: kwanza, tunaharibu aina mbalimbali ya mimea ya mazao inayokua mwituni ambayo inaweza kuzaa aina nyingine mpya wakati ujao, na pili, tunapunguza aina mbalimbali katika jamii za mimea ya mazao. Kwa mfano, huenda aina zaidi ya 100,000 za mpunga wa kienyeji zilikuzwa barani Asia mapema katika karne ya 20, kukiwa na angalau jamii 30,000 nchini India peke yake. Sasa asilimia 75 ya mpunga nchini India hutoka kwa jamii 10 tu. Jamii 2,000 za mpunga nchini Sri Lanka zimetokomea na sasa zimesalia jamii 5 tu. Mexico, inayokuza mahindi kwa wingi, inakuza asilimia 20 tu ya jamii za mahindi yaliyokuwa yakikuzwa miaka ya 1930.

Lakini si akiba ya chakula tu iliyo hatarini. Asilimia 25 hivi ya madawa ya tiba yanayotengenezwa viwandani yanatokana na mimea, na mitishamba mipya ingali inagunduliwa. Lakini, mimea inazidi kutokomea. Je, huenda ikawa kwamba tunaangamiza aina mbalimbali ya mimea ambayo inategemeza uhai wetu?

Shirika la Uhifadhi Ulimwenguni linasema kwamba kati ya jamii 18,000 za mimea na wanyama waliochunguzwa, zaidi ya jamii 11,000 ziko katika hatari ya kutoweka. Katika sehemu kama vile Indonesia, Malasia, na Amerika ya Latini, ambako sehemu kubwa sana za misitu zimekatwa kwa minajili ya kusitawisha mashamba makubwa, watafiti wanakisia-kisia tu idadi ya jamii zinazoelekea kutoweka au zilizotoweka tayari. Hata hivyo, baadhi yao wanasema kwamba jamii zinatoweka kwa “kasi sana,” laripoti jarida la The UNESCO Courier.

Bila shaka, bado kuna chakula kingi sana kinachokuzwa duniani. Lakini itawezekanaje kulisha idadi inayoongezeka kasi ya wanadamu duniani kwa muda mrefu ikiwa jamii mbalimbali za mimea na wanyama zinatoweka? Nchi mbalimbali zimeshughulikia jambo hilo kwa kuanzisha hifadhi za mbegu ili kulinda mimea muhimu isitoweke. Jamii mbalimbali za mimea zinahifadhiwa katika bustani za pekee. Sayansi imevumbua vifaa vipya na njia mpya za kufanya utafiti wa chembe za urithi ili kuboresha jitihada hizo. Lakini je, kweli sayansi na hifadhi za mbegu zinaweza kweli kusuluhisha tatizo hilo? Makala ifuatayo itajibu swali hilo.