Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Mtoto Wako Yuko Salama?

Je, Mtoto Wako Yuko Salama?

 Je, Mtoto Wako Yuko Salama?

Kwa mujibu wa Shirika la Kitaifa la Marekani la Usimamizi wa Usalama Barabarani (NHTSA), aksidenti za magari ndizo zinazosababisha vifo vingi zaidi vya watoto wenye umri wa kati ya miaka 5 na 14. Shirika la NHTSA lasema hivi: “Zaidi ya asilimia 50 ya watoto wanaokufa katika aksidenti hawakingwi na vifaa vya usalama. Isitoshe, watoto 4 kati ya 5 hukingwa isivyofaa.”

Shirika la NHTSA linatoa madokezo kadhaa ya usalama na tahadhari kwa wale wanaosafiri na watoto wao garini. Ingawa sheria za nchi au hata za majimbo mbalimbali hutofautiana, kanuni hizi huenda zikawasaidia wazazi na wale wanaowatunza watoto wafikirie hali hiyo kwa uzito. Tafadhali chunguza sheria za kwenu na ujitahidi sana kutunza usalama wa watoto unaowabeba garini!

MADOKEZO YA USALAMA

Kiti cha nyuma ni salama zaidi kwa watoto.

1 Watoto wachanga wanapaswa kuketishwa katika kiti salama chenye mkanda kinachotazama nyuma. Kiti hicho kiwekwe kwenye kiti cha nyuma.

2 Mtoto aliye na umri wa angalau mwaka mmoja na mwenye uzito wa kilogramu 9 hivi anaweza kuketishwa katika kiti kinachotazama mbele.

3 Anapokuwa na uzito wa kilogramu 18, mtoto anaweza kutumia kiti maalumu kinachowekwa juu ya kiti cha gari na kukingwa kwa mkanda wa mapajani na mkanda wa mabegani.

4 Anapokuwa na uzito wa kilogramu 36 hivi na kimo cha sentimeta 140 hivi, mtoto anaweza kutumia mkanda wa usalama wa watu wazima.

TAHADHARI

Watoto hawapaswi kuketi katika kiti cha mbele cha abiria hadi wanapokuwa na umri wa angalau miaka 13. Mfuko wa kinga unaotumiwa na abiria wanaoketi mbele unaweza kuwajeruhi watoto wachanga vibaya sana.

Kiti maalumu kinapotumiwa bila kinga, mkanda wa mapajani peke yake hauwezi kumkinga mtoto.

Usifikiri kwamba mkanda wa mabegani peke yake utamlinda mtoto; aksidenti inapotokea mkanda huo unaweza kumkaba mtoto koo na kumjeruhi vibaya sana au hata kumwua.

Fuata maagizo kwa uangalifu unapoweka na kutumia viti vya watoto. Shirika la NHTSA linasema kwamba “hata kiti ‘salama zaidi’ huenda kisimkinge mtoto wako kisipotumiwa ifaavyo.”

[Picha katika ukurasa wa 31]

Kuweka ifaavyo kiti cha mtoto kwatia ndani kukifunga kabisa kwa mkanda wa usalama