Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wawindaji Wadogo Wenye Kuvutia

Wawindaji Wadogo Wenye Kuvutia

Wawindaji Wadogo Wenye Kuvutia

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI

ALISIMAMA kwenye jua kali kwa miguu yake ya nyuma, akishikilia sana matawi membamba, na kujiimarisha kwa kutumia mkia wake kama mguu wa tatu. Aliangalia anga na ardhi kwa makini sana ili atambue hatari yoyote. Kila baada ya kipindi kifupi alitoa sauti ndogo-ndogo ili awaonyeshe wenzake walioendelea kutafuta chakula karibu naye kwamba hali ilikuwa salama. Angeendelea kulinda hadi mojawapo wa wenzake achukue zamu—hata kama mwenzake angechelewa kwa muda wa saa moja!

Huyo ni mnyama yupi? Yeye ni nguchiro anayeitwa meerkat. Mla-nyama mdogo huyo mwenye urefu wa sentimeta 40 kutoka pua hadi ncha ya mkia, ni mnyama mwenye urafiki anayeishi katika vikundi vyenye wanyama 10 hadi 30.

Kila asubuhi wakati nguchiro hao wanapotoka shimoni, wote hujipanga kwa mstari na kusimama kwa miguu ya nyuma ili kuota jua baada ya baridi ya usiku. Wanasafishana manyoya kwa upole huku wakitoa milio myembamba ya kirafiki. Ushirikiano huo wa urafiki unaweza kuchukua muda wa nusu saa au zaidi. Punde si punde wanaondoka pamoja ili waanze kuwinda.

Kuwinda kwa utaratibu kunawasaidia nguchiro hao kupata wadudu na wanyama wadogo watambaazi sikuzote. Na wana hamu kubwa kama nini ya chakula! Jitihada ya kutosheleza hamu yao inawachosha hivi kwamba kufikia saa sita mchana wengi wao hulala usingizi chini ya mti au kichakani, na wengine huchimbua mchanga baridi ili kuulalia.

Lakini kwa nini wanahitaji mlinzi? Kwa kuwa wanyama wengine wawindaji wanapenda kuwawinda nguchiro hao. Mbweha na ndege wala-nyama wanapenda kumwinda nguchiro huyo anapochimba ardhi ngumu kwa bidii. Nyakati nyingine nguchiro huchimba mchanga unaozidi uzito wake mara kadhaa ili apate funza mmoja tu.

Namna gani ikiwa mlinzi anaona hatari? Mlinzi anapotoa sauti ya kooni kwa ghafula wote watakimbilia shimo lililo karibu kwa fujo. Lakini, ikiwa sauti ya onyo ya mlinzi inaonyesha kwamba kikundi kingine cha nguchiro kimekaribia, nguchiro wa mahali hapo hawatakimbia. Badala yake watasongamana wakipinda migongo na kusimamisha manyoya na mikia wima. Watalia kwa ukali wanapoelekea wavamizi, huku wengine wao wakirukaruka kwa miguu iliyokakamaa kana kwamba wanacheza dansi ya vita. Mara nyingi wavamizi watakimbia wanapokabili kikundi hicho.

Jitihada ya Pamoja

Nguchiro wanasaidiana mara nyingi. Jambo hilo ni wazi hasa inapohusu kutunza watoto wao. Wote wanashughulikia sana wageni hao kwa majuma kadhaa baada ya kuzaliwa kwao. Wale wengine huwatembelea mama na watoto mara nyingi. Na jinsi wanavyomkaribisha mama anapowatoa watoto wake shimoni mara ya kwanza! Wote wanamwuma-uma mama shingoni kwa upole, wakitoa vilio vyembamba vya furaha, na kusuguana na watoto kwa wororo.

Wote watasaidia kuwatunza watoto kwa majuma machache. Karibu wote watashika zamu ya kutunza watoto kwa utayari, wengine wakienda kuwinda. Nguchiro wa kike wasio na watoto watatokeza maziwa ili wasaidie kuwanyonyesha watoto—kwa njia hiyo kazi ya mama mzazi hupungua. Shughuli hizo zote humzuia yule anayetunza watoto asipate fursa ya kutafuta chakula. Kwa hiyo, wengine ambao wamesaidia kutunza watoto wamepoteza asilimia kumi ya uzito wao!

Watoto wanapokuwa na umri wa kutosha ili kuondoka shimoni na kuambatana na wengine kuwinda, nguchiro wakomavu hufundisha kila mtoto kwa utayari na kwa subira jinsi ya kuwinda. Mara nyingi, watoto hupewa mawindo mazuri zaidi hata ingawa wanyama wakomavu hawatakula chakula cha kutosha siku hiyo. Iwapo mlinzi anatoa mlio wa hatari, angalau mmoja wao atahakikisha kwamba watoto wamefika shimoni salama.

Wanastahili Kutazamwa

Nguchiro wanazoea wanadamu kwa urahisi nao ni wenye urafiki. Kitabu Maberly’s Mammals of Southern Africa (Wanyama wa Kusini mwa Afrika) kinasema hivi: “Kwa ujumla, bila shaka, wanyama hao wadogo ni miongoni mwa wanyama wenye kupendeza na wenye kuvutia zaidi kusini mwa Afrika, nao wanastahili kutazamwa sikuzote.”

Alain, ambaye ametengeneza filamu juu ya nguchiro kwa miaka mingi, anakubali. Anakumbuka wakati ambapo nguchiro mmoja wa kike alipotoka shimoni akiwa amembebea kinywani mtoto wake aliyekuwa na umri wa siku nne na kumweka kwenye nyayo zake huku akilia kwa sauti ndogo. Alain alifikiri mtoto huyo alikuwa amekufa. Akasema hivi: “Lakini nilipomchukua kwa upole nilitambua kwamba alikuwa hai, na kwamba mama yake alitaka tu nimwone kwanza, kabla wale nguchiro wengine hawajaja kwa haraka kumpa hongera. Niliguswa sana hivi kwamba hata nilisahau kupiga picha.”

Sylvie, ambaye amechunguza nguchiro wa porini kwa miaka mingi, anakumbuka asubuhi moja alipokuwa akilala chini karibu na shimo lao, kisha nguchiro wakatoka shimoni. Kama kawaida, walijipanga kwa mstari umbali wa sentimeta chache kutoka kwake, na kuanza kusafishana manyoya na kukumbatiana. Alipoongea nao walijibu kwa kutoa milio myembamba. Sylvie alianza kumpapasa nguchiro wa kwanza wa kike kwa upole kwa kidole chake—hadi kufikia sikio lake. Alijiviringisha kwa furaha na kuanza kusafisha manyoya ya yule aliyekuwa karibu naye. Kisha Sylvie akasema hivi: “Nimekubaliwa kuwa mmoja wao katika desturi yao ya kukumbatiana, hilo ni pendeleo lililoje!”

Wale ambao wametumia wakati pamoja na nguchiro wana mengi ya kusimulia. Hao ni wawindaji wenye kuvutia kwelikweli!

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kuwafukuza maadui

Mlinzi anayeshika zamu

Kuota jua kabla ya kuanza kuwinda

[Hisani]

Picha zote: © Nigel J. Dennis