Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nondo Maridadi

Nondo Maridadi

Nondo Maridadi

JIONI moja yenye kupendeza nondo mmoja aliingia kwenye mkahawa mmoja wa kifahari. Alipokuwa akirukaruka karibu na meza moja, mwanamke aliyekuwapo alimfukuza nondo huyo kana kwamba alikuwa akishambuliwa na mbu hatari! Nondo huyo aliruka kwenye meza nyingine, na hatimaye akatua kwenye koti la mwanamume mmoja. Mwanamume huyo na mkewe walivutiwa mno na nondo huyo. Walifurahia umaridadi na uzuri wa kiumbe huyo asiyedhuru.

“Nondo ni viumbe wasiodhuru kabisa,” aeleza John Himmelman, aliyeshiriki kuanzisha Shirika la Connecticut Butterfly Association. “Midomo yao haiwezi kuuma, na baadhi ya nondo wakomavu, kama vile nondo aina ya luna ajulikanaye sana, hawali chochote. Hawana viini vya ugonjwa wa kichaa cha mbwa wala ugonjwa mwingineo wote, hawaumi . . . Kwa kweli, watu wengi hata hawajui kwamba vipepeo ni nondo tu wanaoruka wakati wa mchana.”

Kila mtu huvutiwa na vipepeo, lakini ni watu wachache sana wanaovutiwa na jamii mbalimbali za nondo na umaridadi wao. ‘Umaridadi?’ huenda ukauliza kwa shaka. Watu fulani hudhani kwamba nondo ni kiumbe asiyevutia wa jamii ya vipepeo ambao ni maridadi. Hata hivyo, nondo na vipepeo wana jina moja la kisayansi—Lepidoptera, jina hilo linamaanisha viumbe wenye “mabawa yenye manyoya.” Kuna jamii nyingi sana za viumbe hao maridadi. Kichapo The Encyclopedia of Insects chasema kwamba kuna jamii 150,000 hadi 200,000 zijulikanazo za Lepidoptera. Lakini vipepeo ni asilimia 10 tu ya viumbe hao—jamii nyinginezo ni nondo!

Sawa na watu wengine wengi, mimi sikujali mno nondo hadi nilipokuwa nikitia dawa ya kufukuza nondo wanaokula nguo kwenye mavazi ninayotumia msimu wa baridi kali. Sikujua kamwe kwamba nondo waliokomaa hawali nguo. Wao hula nguo wanapokuwa viwavi. *

Mbona nikabadili maoni yangu kuhusu nondo? Siku chache zilizopita mimi na mume wangu tulitembelea Bob na Ronda ambao ni marafiki wetu. Bob alijua mengi kuhusu nondo. Alinionyesha sanduku dogo lililokuwa na kiumbe niliyedhani ni kipepeo maridadi. Aliniambia kiumbe huyo ni nondo aina ya cecropia, au nondo aitwaye robin, mojawapo ya nondo wakubwa zaidi katika Amerika Kaskazini. Upana wa mabawa yake kutoka ncha hadi ncha unaweza kufikia sentimeta 15 na duru yake ya maisha inaweza kuchukua muda wa mwaka mmoja. Nilishangaa kama nini kujua kwamba nondo huyo anaishi kwa siku 7 hadi 14 tu baada ya kukomaa! Nilijifunza mambo mengi mapya kuhusu nondo baada ya kumchunguza nondo maridadi aina ya cecropia.

Bob alinionyesha vitu vidogo-vidogo sandukuni. “Haya ni mayai, nami natarajia kuyatunza yatakapoanguliwa,” akasema Bob. Kulea nondo? Wazo hilo lilinishangaza sana. Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kulea nondo. Kwa muda wa majuma mawili Bob alishindwa kuyaangua mayai hayo. Kisha akaamua kuyatia kwenye mvuke. Juma moja baadaye mayai 26 kati ya 29 yalianguliwa siku moja. Bob akatia viluwiluwi hivyo dhaifu, kwenye bakuli laini ili visiende huku na huku. Kila kiluwiluwi kilitoshana na mbu.

Viluwiluwi hivyo vilikula kwanza vifuko vya mayai yao. Baada ya hapo, Bob alivipa chakula. Haikuwa kazi rahisi. Baada ya kufanya utafiti alivipa majani ya mti uitwao maple. Viluwiluwi hivyo vilitambaa kwenye majani hayo lakini havikuyala. Lakini, viluwiluwi hivyo vilikula majani ya cheri na ya mbetula, yaliyotiwa humo na Bob.

Viluwiluwi hivyo vidogo vilipokomaa na kuwa viwavi, Bob alivihamisha kwenye kijumba kilichofunikwa. Kijumba hicho kilikuwa na unyevu uliofaa viwavi hao na majani yaliyokuwamo. Pia, kijumba hicho kiliwazuia viwavi wasitoke, kwa kuwa mara tu walipoanza kutambaa walianza kwenda huku na huku.

Sikujua kwamba kulisha viwavi 26 wenye njaa ingekuwa kazi ngumu. Kila mara Bob alipojaza majani kwenye kijumba hicho, viwavi hao walikula majani yote kwa siku mbili tu. Ndipo alipomwomba dada yake na marafiki wake wawili, mvulana mmoja na msichana, wamsaidie kutunza na kulisha viwavi hao wenye kukua.

Ni lazima viwavi wale chakula kingi ili wakue na kuhifadhi chakula hicho wanapokomaa. Kwa mfano, nondo mkomavu aina ya cecropia hawezi kula kwa mdomo wake, na hali chakula hata kidogo! Nondo huyo mkomavu hutegemea chakula alichokula na kuhifadhi alipokuwa kiluwiluwi. Yeye huishi kwa muda mfupi tu baada ya kukomaa.

Kupata Ngozi Mpya

Viwavi wanapokomaa wanaambua ngozi zao mara kadhaa. Viwavi huambua ngozi zao katika hatua inayoitwa kwa Kiingereza Instar.

Ngozi ya kiwavi wa cecropia haikui, kwa hiyo kiwavi huyo anaponona ngozi yake hujivuta, halafu anaiambua. Bob alijua wakati barabara wa viwavi kuambua ngozi yao, kwa sababu wakati huo ulipofika viwavi hao waliacha kula chakula. Walisokota hariri na kuingia ndani yake. Halafu wakabaki papo hapo kwa siku kadhaa huku ngozi mpya ikikua mwilini. Walipopata ngozi mpya, viwavi hao waliibuka kwenye ngozi ya zamani na kuiacha kwenye hariri. Nilistaajabu sana kuona viwavi hao wakiambua ngozi mara ya mwisho kwani walikuwa wakubwa sana. Walikuwa na urefu wa sentimeta 12 hivi na walikuwa wakubwa kuliko kidole changu cha shahada.

Kusokota Kifukofuko

Baada ya kuambua ngozi mara ya mwisho, kila kiwavi alisokota kifukofuko—nyuzi nyingi za rangi ya kijivu zilizofungwa kwenye kijiti. Nondo aina ya cecropia husokota vifukofuko vya aina mbili. Kifukofuko cha kwanza ni kikubwa na kimelegea. Kina kitako cha mviringo na ncha nyembamba. Kifukofuko cha aina nyingine ni kidogo na kimeshikamana sana. Kina umbo la mstatili na kina ncha na kitako chembamba. Vifukofuko vyote viwili vina kifukofuko kingine kidogo ndani kilichosokotwa kwa nguvu sana. Kwa kawaida, vifukofuko vya nondo aina ya cecropia huwa na rangi ya kahawia-nyekundu, kahawia, kijani-kibichi hafifu, au rangi ya kijivu. Vifukofuko vya nondo aina ya cecropia huwa vikubwa mno tofauti na vifukofuko vya nondo wengine wa Amerika Kaskazini. Vinakuwa na urefu wa sentimeta 10 hivi na upana wa sentimeta 5 hadi 6. Vifukofuko hivyo vyenye kustaajabisha vinaweza kulinda viwavi hao hata katika baridi kali ya nyuzi Selsiasi 34 chini ya sufuri.

Baada ya viwavi kuingia ndani ya vifukofuko, hatukuwa na la kufanya ila kusubiri tu. Walitoka kwenye vifukofuko majira yaliyofuata ya masika, mwaka mmoja hivi tangu Bob alipoanza kumtunza yule nondo mkomavu. Bob alivitia vijiti vyenye vifukofuko kwenye plastiki ili viwe wima. Punde si punde, nondo wote walitoka kwenye vifukofuko vyao isipokuwa nondo mmoja tu. Kazi ngumu na subira ya Bob haikuwa ya bure.

Sasa Nathamini Sana Nondo

Kushuhudia duru yenye kustaajabisha ya maisha ya nondo aina ya cecropia kumenifanya nipendezwe zaidi na nondo wanaorukaruka karibu na taa na kutua kwenye majengo. Mambo hayo yalinichochea kujifunza mengi zaidi kuhusu viumbe hao wa ajabu. Kwa mfano, nilijifunza kwamba nondo na vipepeo ni warukaji stadi sana. Jamii nyingi huhamia sehemu za mbali sana. Upana wa kutoka ncha hadi ncha wa ubawa wa nondo mdogo aina ya diamondback ni sentimeta 25 tu, lakini pindi kwa pindi anaruka kutoka Ulaya hadi Uingereza na kuvuka Bahari ya Kaskazini yenye dhoruba. Na nondo aina ya sphinx, au hawkmoths, hupaa juu ya maua kama ndege-wavumaji.

Pindi moja baada ya kutazama duru ya maisha ya cecropia, nilimwona nondo mmoja akiwa juu ya kichaka kilichomulikwa na taa. Nilijua kwamba mtu hapaswi kumbeba kwa mabawa yake kwa sababu manyoya yaliyo kwenye mabawa yake ni mepesi mno. Hata hivyo, ukiweka mkono wako uliofumbuliwa mbele ya nondo, huenda akapanda kwenye kidole chako. Nilipofanya hivyo, nilifurahi sana kumwona kiumbe huyo maridadi akipanda kwenye kidole changu cha kati. Mwishowe aliruka angani na kutokomea. Alipokuwa akiruka, niliona kwamba alifanana kabisa na kipepeo. Unapomwona kipepeo wakati ujao, mtazame tena kwa makini. Huenda akawa nondo maridadi asiyedhuru.—Imechangwa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Viluwiluwi vya baadhi ya nondo huharibu mimea pia.

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

1. Nondo aina ya “Robin” (“cecropia”)

2. Nondo aina ya “Polyphemus”

3. Nondo aina ya “Sunset”

4. Nondo aina ya “Atlas”

[Hisani]

Natural Selection© - Bill Welch

A. Kerstitch

[Picha katika ukurasa wa 18]

Duru ya maisha ya nondo aina ya “cecropia” yatia ndani:

1. Mayai

2. Kiwavi

3. Nondo aliyekomaa

[Hisani]

Natural Selection© - Bill Welch