Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mahali Ngamia na Farasi Hurandaranda

Mahali Ngamia na Farasi Hurandaranda

Mahali Ngamia na Farasi Hurandaranda

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

SEHEMU za mashambani za Australia—ni picha gani inayokuja akilini mwako unaposikia habari za eneo hilo? Mandhari yenye kangaruu wenye kurukaruka, emu wasiopuruka, majangwa yenye vumbi jekundu na joto kali wakati wa mchana? Kwa kadiri fulani picha yako ni sahihi—lakini pia eneo hilo lina mambo yenye kushangaza.

Je, unajua kwamba ni huko Australia pekee kunakopatikana makundi ya ngamia-mwitu, makundi makubwa zaidi duniani ya farasi-mwitu na punda wengi kama nzige? Wanyama hao huwakumbusha wakazi wa Australia juu ya wakati uliopita, hata hivyo ni watu wachache wanaojua hadithi ya jinsi wanyama hao walivyofika huko na kazi ngumu waliofanya.

Ngamia Alitumiwa Kusitawisha Eneo Hilo

Kwa miongo minne iliyopita, wafugaji wa ng’ombe katika sehemu za mashambani za Australia wamelalamika kama alalamikavyo mchungaji mmoja wa ng’ombe katika kitabu The Camel in Australia: “Nimeona mahali ambako ngamia 5 wameharibu kilometa 10 za ua wa kuweka mipaka . . . Katika eneo fulani waliharibu nyaya na vigingi na ua wote.”

Ua wa kuweka mipaka wenye kugharimu sana hauwezi kuzuia ngamia wenye miguu mirefu na miili yenye nguvu. Hata hivyo, wanyama hao ndio waliotumika kujenga barabara zinazopitia sehemu kavu ya bara hilo.

Katika safari yao maarufu ya kutoka kusini hadi kaskazini mwa Australia, wavumbuzi Burke na Wills walitumia ngamia waliokuwa wameingizwa Australia kutoka India katika mwaka wa 1860. Wanyama hao wageni walitumiwa na wasafiri wa mapema kwa sababu ya nguvu zao na uvumilivu. Wakiwa hodari wa kuishi muda mrefu bila kula, waliweza kubeba mizigo yenye uzani wa kilogramu 300 kwa umbali wa kilometa 800 na kunywa tu lita 15 za maji.

Kwa kuwa ngamia ni wenye kutegemeka sana, walitumika kupeleka chakula na vifaa kwenye majiji yaliyoibuka karibu na migodi ya dhahabu, walitumiwa pia wakati wa kuwekwa kwa nyaya za simu kutoka Adelaide hadi Darwin na kupimwa kwa njia ya reli (Trans-Australian Railway) inayounganisha miji ya Sydney na Perth. Kwenye eneo hilo kavu sana lenye ukubwa wa kilometa milioni 4 za mraba ngamia hao walifanya kazi ngumu ambayo hata mashine za kisasa haziwezi kufanya.

Idadi ya ngamia wenye kufugwa ilifikia kilele cha 22,000 katika mwaka wa 1922, lakini kwa sababu ya kuongezeka kwa magari, ngamia wengi waliachiliwa huru mbugani. Wakiwa huru kutembea na kuzaana wapendavyo, inasemekana kwamba sasa kuna zaidi ya ngamia 200,000 wanaoishi katika majangwa ya Australia na watu fulani wanakadiria kwamba idadi hiyo itaongezeka maradufu katika muda wa miaka sita ijayo.

Hata hivyo, si ngamia wote walio wa mwitu. Msemaji wa Shirika la Ngamia la Australia ya Kati aliliambia Amkeni! hivi: “Kwa sababu makundi ya ngamia katika Australia ndiyo pekee duniani yasiyo na maradhi, idadi ndogo ya wanyama hao husafirishwa hadi kwenye hifadhi na mbuga za wanyama huko Marekani na Asia.” Waendesha-biashara ya utalii huwapa nafasi wageni kupanda ngamia na kujionea sehemu za mashambani za Australia—ambako kunapatikana pia wanyama wengine wa kubeba mizigo walioachwa huru.

Farasi-Mwitu Ni Nani?

Kundi la kwanza la meli za Uingereza ziliteremsha shehena yake ya wafungwa, askari, na farasi kwenye fuo za Australia katika mwaka wa 1788. Historia yenye kuvutia na pia yenye kuhuzunisha ya farasi katika nchi hiyo ni sawa na historia ya wanadamu waliofika Australia wakati huo.

Farasi waliwasafirisha kila mahali walowezi wa kwanza waliojitahidi kulitiisha bara hilo. Punde si punde, farasi waliopotea au kutoroka walifanyiza makundi ya farasi-mwitu na farasi hao wakaja kuitwa Brumbies. Neno “Brumby” huenda lilitokana na neno baroomby la wenyeji wa Queensland linalomaanisha “-a mwitu.”

Washairi wengi wamevutiwa sana na maisha ya farasi-mwitu ya kufanya apendavyo.Wimbo uitwao “The Man From Snowy River” ulioimbwa na mmoja wa washairi hao A. B. (Banjo) Paterson, umefanya farasi huyo apendwe na wenyeji wengi wa Australia. Idadi ya farasi-mwitu iliongezeka sana baada ya Vita ya Ulimwengu ya Kwanza wakati farasi aina ya Waler—aliyezoezwa hususa kwa matumizi ya Kikosi cha Australia cha wapanda-farasi na kutumiwa na askari Wahindi—walipoachiliwa huru. Inakadiriwa kwamba leo kuna farasi-mwitu 300,000 wanaorandaranda kwenye bara hilo.

Wanaporandaranda, kwato zao huharibu udongo usio imara na kumomonyoa kingo za vidimbwi vya maji. Wakati wa ukame, hufa njaa au kiu. Farasi hao wamekuwa mzigo wenye kulemea kwa sababu eneo hilo lina ng’ombe wengi kupita kiasi. Kwa sababu hiyo, maelfu ya farasi hao huuawa kila mwaka ili kupunguza idadi yao. Nyama yao hutayarishwa kuwa chakula cha binadamu au cha wanyama.

Hata hivyo wanyama wengi zaidi katika eneo hilo ni punda-mwitu mwenye umbo linaloshabihi farasi-mwitu. Imekuwa lazima kuwapunguza wanyama hao wanaozaana sana kuliko farasi-mwitu na kuzagaa kwenye eneo kubwa kuliko ngamia.

Mbinu ya Yudasi

Punda, kama ilivyotukia na farasi, waliingizwa Australia mapema miaka ya 1700 kwa kusudi la kukokota mizigo au kuvuta plau, na walizoea upesi mazingira mapya. Baada ya punda wengi kuachiliwa huru katika miaka ya 1920, idadi yao iliongezeka na kuwa mara 30 ya idadi ya awali ya makundi ya punda-mwitu.

Kama ngamia, punda ameumbwa kuishi jangwani, ana uwezo wa kuzuia jasho lisimtoke anapoishiwa na maji na anaweza kustahimili kupoteza maji yanayolingana na asilimia 30 ya uzani wake. (Wanyama wengine hufa wanapopoteza maji yanayolingana na asilimia 12 hadi 15 ya uzani wao.) Wao hufurahia kula majani mororo lakini wanaweza pia kula majani makavu yasiyoliwa na ng’ombe. Kufikia miaka ya 1970, punda zaidi ya 750,000 walizagaa katika nusu ya bara hilo la Australia. Idadi hiyo yenye kuongezeka ilisababisha matatizo ya mazingira na kutatiza ufugaji wa ng’ombe hivyo ikalazimu hatua fulani ichukuliwe.

Jitihada ya kuwapunguza katika miaka ya 1978 hadi 1993 ilisababisha punda 500,000 kuuawa huko kaskazini-magharibi mwa Australia pekee. Leo, punda 300 wamewekwa mwilini mwao kifaa cha radio katika mpango unaojulikana kama mbinu ya Yudasi. Baada ya kuachwa huru kujiunga na wenzao, kifaa hicho cha radio kilicho mwilini mwa punda huwaongoza watu walio kwenye helikopta hadi mahali walipo punda wengi na punda hao hupunguzwa kwa kuuawa bila ukatili. Baadaye punda mwenye kifaa cha radio mwilini hujiunga na kundi jingine la punda na hivyo kuwaongoza waangamizaji kwa kundi hilo pia.

“Hilo ni tatizo la kudumu,” ofisa mmoja wa ulinzi wa mifugo kutoka eneo la Magharibi mwa Australia aliliambia Amkeni! Alionya hivi: “Kundi la punda wachache wenye kuzaana likisalia, baada ya muda mfupi kutakuwa na idadi kubwa ya punda kama ile ya miaka ya 1970. Watu wengi hushangaa kuona wanyama hao wakiuawa na mizoga kuachwa palepale. Hawafahamu kwamba maeneo hayo hayafikiki. Maeneo hayo hayana barabara na sehemu nyingi hufikiwa tu kwa helikopta. Ni matendo ya binadamu yaliyosababisha tatizo hilo na hivyo tunajaribu kuangamiza hao punda kwa namna isiyo na ukatili tuwezavyo.”

Hodari na Huzaana Sana

Huenda sasa unafikiri kwamba kuna wanyama wengi wachukua-mizigo wasiohitajiwa katikati mwa Australia. Lakini eneo la mashambani la Australia ni kubwa sana. Eneo ambalo wanyama hao hurandaranda linatoshana na Ulaya lakini linashabihi ardhi ya mwezi—kavu kama mwezi na lenye milima kama Ulaya. Kutafuta makundi ya wanyama ni vigumu sana sembuse kuwadhibiti.

Tofauti na wanyama wenyeji walio katika hatari ya kuangamia, punda hao hodari na wenye kuzaana sana wamekuwa sehemu ya kudumu ya mandhari ya eneo hilo. Kwa sababu hawana adui wa asili na hawashikwi na maradhi, wanyama hao hurandaranda tu kwenye eneo hilo la mashambani la Australia!

[Picha katika ukurasa wa 16]

Ngamia wapatao 200,000 hurandaranda katika majangwa ya Australia

[Hisani]

Agriculture Western Australia

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Farasi-mwitu hurandaranda ukingoni mwa Jangwa la Simpson

[Picha katika ukurasa wa 17]

Msafara wa ngamia wenye kubeba manyoya ya kondoo, mwaka wa 1929

[Hisani]

Image Library, State Library of New South Wales

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mtindo wa kukusanya farasi-mwitu kama itukiavyo kwenye eneo la mashambani la Australia

[Hisani]

© Esther Beaton

[Picha katika ukurasa wa 18]

Punda awekwa kifaa cha radio katika ile mbinu ya Yudasi

[Hisani]

Agriculture Western Australia