Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kuathiriwa na Kemikali Nina umri wa miaka 17 na ningependa kuwashukuru kwa ajili ya mfululizo “Kemikali za Kawaida—Je, Zinafanya Uwe Mgonjwa?” (Agosti 8, 2000) Hivi majuzi nilibainishwa kuwa na hali ya kuathiriwa na kemikali mbalimbali (MCS), na nilifarijika sana kujua kwamba watu wengi wanaugua ugonjwa huo wenye kufedhehesha.

S. C., Italia

Makala mliyochapisha awali yenye kichwa “Je, Uchafuzi wa Hewa Unafanya Uwe Mgonjwa?” (Juni 8, 1983, Kiingereza) ilikuwa na habari yenye kuokoa uhai. Ugonjwa huu mbaya sana hututenga na ushirika wa familia yetu ya kiroho na utendaji wa kijamii. Na bado, watu hawaelewi au kuwahurumia watu wenye ugonjwa huo. Makala zenu za karibuni zilieleza kinagaubaga matatizo ya watu wenye ugonjwa huo.

M. J., Ufaransa

Niliugua kwa zaidi ya mwaka mzima kabla ya kupata daktari ambaye aliweza kunisaidia. Kwa kipindi hicho, rafiki zangu walikuwa wenye fadhili na hawakuwa na maoni mabaya kunielekea, ingawa nilifahamu kwamba walitatanishwa na hali yangu. Kwa hiyo nawashukuru sana kwa makala hizo. Inatia moyo sana kuwa katika tengenezo linalojua mambo mengi.

S. B., Marekani

Ninaugua ugonjwa wa MCS na sijapata kamwe kusoma habari kamili na yenye usawaziko kama hiyo kuhusu ugonjwa huu na athari zake. Nilifurahi kusoma kwamba upendo na kicheko ni “dawa” ya kukabiliana na ugonjwa huo. Nilikumbushwa kwamba sipaswi kutarajia mengi mno kutoka kwa wengine.

D. G., Marekani

Nikiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, nimetumika kwa miaka kumi nikiwa mwangalizi asafirie na nimekutana na watu kadhaa wenye ugonjwa wa MCS. Ni wazi kwamba ugonjwa huo ni halisi wala si jambo la kuwaziwa tu. Kama ilivyo desturi, Amkeni! limefafanua ugonjwa huo na kutoa madokezo ya jinsi wengine wawezavyo kuonyesha wanaougua ugonjwa huo fadhili, upendo, na huruma.

T. M., Marekani

Mapambo ya Mwili Naandika kuhusiana na makala yenu “Maoni ya Biblia: Mapambo ya Mwili—Uhitaji wa Kuwa na Kiasi.” (Agosti 8, 2000) Mapambo ya mwili yafaayo ni maridadi—ufundi halisi wa sanaa. Jumuiya huenda ikaudhiwa na sura yangu ya nje, lakini najua mimi ni mwenye kupendeza machoni pa Mungu. Natumaini na kusali kwamba watu wasikazie uangalifu michoro katika mwili wangu bali waangalie utu wangu wa ndani.

K. M., Marekani

Makala hiyo ilikiri kwamba kujipamba au kutojipamba mwili ni uamuzi wa binafsi. Hata hivyo, njia moja ya mtu kuonyesha sura nzuri ya ndani ni kwa ‘kujiremba mwenyewe kwa kiasi na utimamu wa akili.’ (1 Timotheo 2:9) Biblia pia inasema wazi kwamba Mkristo ana wajibu wa kutunza dhamiri yake mwenyewe na “ile ya mtu yule mwingine.” (1 Wakorintho 10:29)—Mhariri.

Lugha Asanteni kwa makala “Lugha—Viunganishi na Vizuizi vya Mawasiliano.” (Agosti 8, 2000) Nimevutiwa daima na lugha, nami tayari nimejifunza lugha tano za Ulaya. Sasa najifunza Kisinhala. Jambo lenye kunipendeza zaidi ni kwamba kujifunza lugha mpya huniwezesha kufikia watu wa tamaduni nyingine na kuwafundisha “lugha iliyo safi” ya Biblia!—Sefania 3:9.

C. B., Italia

Kihoro Asanteni kwa makala “Je, Twapaswa Kuonyesha Kihoro?” (Agosti 8, 2000) Habari hiyo ilitugusa moyo kwa sababu mwana wetu alikufa miaka mitatu iliyopita. Ingawa sisi bado hulia na kuwa na kihoro, makala kama hizo hututia nguvu kuendelea.

J. A. na L. A., Marekani