Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuchunguza Nywele Zako

Kuchunguza Nywele Zako

Kuchunguza Nywele Zako

“KATIKA kila enzi na utamaduni, nywele za mtu zinafunua jambo fulani kumhusu,” chasema kitabu kimoja cha marejeo. Basi, si ajabu kwamba watu walio wengi hupenda kuzitunza nywele zao ili ziwe nzuri na za kuvutia.

Mwandishi wa Amkeni! aliwauliza watengenezaji wanne wa nywele wenye ujuzi maswali kadhaa kuhusu muundo wa nywele na jinsi ya kuzitunza. Kumbe, nywele zako ni tata kuliko zinavyoonekana kwa nje.

Ukuzi na Kutoka kwa Nywele

S: Nywele zimefanyizwa na nini?

J: Nywele zina protini yenye nyuzinyuzi iitwayo keratini. Kila unywele hukua katika kibonyeo katika ngozi ya kichwa kiitwacho kinyweleo. Chini ya kila kinyweleo kuna kituta cha kuotea unywele, ambacho kina mishipa mingi ya damu. Kituta hicho hutokeza chembe za unywele ambazo husogezwa juu kuzunguka kinyweleo, nazo huungana kwa uthabiti na kufanyiza unywele.

S: Watu wengi huamini kwamba nywele hukua haraka zinaponyolewa au kupunguzwa. Je, jambo hilo ni la kweli?

J: La. Baadhi ya watu hudhani kwamba nywele hurutubishwa na mwili, kama vile matawi ya mti hurutubishwa na shina. Lakini nywele hazina uhai. Kwa hiyo, kunyoa au kupunguza nywele hakutasaidia nywele kukua haraka.

S: Mvi zinatokana na nini?

J: Tabaka la ndani la unywele lina chembe ambazo hutokeza rangi ya nywele. Wakati chembe hizo zinapokufa, ndipo mvi hutokea. Kuota mvi ni jambo la kawaida mtu anapozeeka. Mvi zinapotokea mapema maishani huenda zikasababishwa na ugonjwa au huenda hali hiyo imerithiwa. Hata hivyo, si kweli kwamba mvi zinaweza kutokea katika usiku mmoja. Chembe ambazo hutokeza rangi ziko chini ya ngozi ya kichwa. Kwa hiyo, mvi hutokea nywele zikiendelea kukua kichwani (sentimeta 1.25 hivi kwa mwezi).

S: Kwa nini nywele hutoka?

J: Kutoka kwa nywele ni jambo la asili. Kwa wastani, mtu hupoteza nywele 50 hadi 80 hivi kila siku. Lakini upara wa kawaida wa wanaume ni hali ambayo hurithiwa, na yaelekea husababishwa na hitilafu ya homoni. Kutoka kwa nywele isivyo kawaida kunaitwa kwa Kiingereza alopecia. *

S: Baadhi ya watu husema kwamba nywele hufichua hali ya afya ya mtu. Je, wewe umeona jambo hilo?

J: Naam. Damu hurutubisha nywele chini ya ngozi ya kichwa. Kwa hiyo, huenda nywele zenye afya zikadhihirisha damu yenye afya. Kwa upande mwingine, mtu ambaye hali chakula chenye afya au anayekunywa vileo kupita kiasi, huenda akapata kwamba nywele zake ni dhaifu na hukatika kwa urahisi, kwa maana damu yake haiwezi kurutubisha nywele zake kwa njia inayofaa. Kutoka kwa nywele au nywele dhaifu hata inaweza kuwa dalili ya mapema ya ugonjwa au ujauzito.

Kudumisha Afya ya Nywele na ya Ngozi Yako ya Kichwa

S: Eleza jinsi ya kuosha nywele na ngozi ya kichwa.

J: Watu wengi walio na ngozi ya kichwa inayoparara, huosha nywele zao mara nyingi kupita kiasi. Ni kweli kwamba, mafuta ya nywele zako huvuta uchafu na vipande vya ngozi ambavyo vinaweza kuziba vifereji vya mafuta vinavyoelekeza kwenye vinyweleo. Kwa hiyo, ni lazima kuosha nywele kwa ukawaida. Lakini mafuta hayo ya asili pia hulinda ngozi yako dhidi ya bakteria zenye kudhuru na kuhifadhi unyevu muhimu. Ukiziosha nywele zako mara nyingi kupita kiasi utaondoa mafuta hayo yenye kulinda na kusababisha matatizo kama vile kuparara kwa ngozi ya kichwa. Watu wenye ujuzi hupendekeza kuosha nywele wakati ambapo ngozi ya kichwa au nywele zimechafuka. Watu wenye nywele zenye mafuta mengi ya asili wapaswa kuosha nywele mara nyingi kuliko wale wenye nywele zisizo na mafuta mengi.

Unapoosha nywele, sugua ngozi ya kichwa. Hilo huondoa chembe za ngozi zilizokufa na kuongeza uzungukaji wa damu ambayo hurutubisha nywele zako. Kumbuka kuosha vizuri kwa maji safi! Ikiwa ungekosa kuosha mikono yako kwa maji safi baada ya kunawa na sabuni, ngozi yako ingeparara na kupasuka. Vivyo hivyo, ikiwa nywele hazioshwi vizuri kwa maji safi, ngozi ya kichwa itaweza kuparara.

S: Naweza kufanya nini ngozi ya kichwa inapoparara?

J: Ukinywa maji mengi, na kula chakula bora utaongezea ngozi yako unyevu na damu itakuwa yenye afya. Tumia sabuni ya nywele isiyo kali sana, na usugue ngozi ya kichwa kwa ukawaida. Baada ya kuosha nywele, baadhi ya watu hupaka nywele mafuta ili kuilainisha na kufanya ngozi ya kichwa isikauke.

Mtindo wa Nywele Zako

S: Mtu anapaswa kukumbuka nini anapokwenda kutengeneza nywele?

J: Ukitaka mtindo fulani, uende na picha inayoonyesha mtindo ambao unataka na labda nyingine ya mtindo ambao hutaki. Eleza kwa wazi mtindo ambao unataka na muda ambao unataka kutumia kutengeneza nywele zako kila siku, kwa maana mitindo fulani inataka kazi nyingi kuliko mitindo mingine. Kumbuka kwamba kwa ukawaida mtengenezaji wa nywele anahitaji kutengeneza nywele zako mara mbili au tatu kabla hajazoea nywele zako na kuelewa mapendezi yako. Kwa hiyo, usivunjike moyo na kubadili haraka mtengenezaji wa nywele!

Nywele Zako Hufichua Nini?

Utunzaji na mitindo ya nywele hufichua mambo fulani kumhusu mtu. Nywele zimekatwa, zimerefushwa, zimesokotwa, zimebadilishwa rangi, na kutengenezwa kwa njia mbalimbali ili kupatana na mitindo inayopendwa, itikadi za kidini, na hata maoni ya kijamii na kisiasa. Chunguza nywele zako kwa makini sana. Zinafichua nini kukuhusu? Nywele zenye afya ambazo zimetengenezwa vizuri humrembesha mtu naye huvutia wengine.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 12 Kwa habari zaidi, soma makala “Alopecia—Living in Silence With Hair Loss,” katika toleo la Aprili 22, 1991, la Amkeni! la Kiingereza.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kunywa maji mengi na kula chakula bora huenda kukazuia ngozi ya kichwa isiparare

[Picha katika ukurasa wa 26]

Ukiosha nywele zako mara nyingi mno utaondoa mafuta ambayo hulinda ngozi ya kichwa

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kuota mvi ni jambo la kawaida mtu anapozeeka