Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuiona Kimbele Paradiso

Kuiona Kimbele Paradiso

Kuiona Kimbele Paradiso

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

KWA Kawaida tembo, simbamarara, na swala hawapatikani katika migodi isiyotumiwa. Migodi isiyo na kina huacha eneo likiwa limeharibika sana lisifae kuwa makao ya wanyama walioletwa kutoka nchi za kigeni.

Lakini katika Bustani ya Wanyama ya Cabárceno mkoa wa Cantabria, Hispania, majaribio yasiyo ya kawaida yameonyesha kwamba hata maeneo mabovu yanaweza kugeuzwa na kuwa mazuri kama paradiso.

Kwa miaka ipatayo 3,000, eneo la Cabárceno lilijulikana sana kwa kutoa mawe bora yenye madini ya chuma. Wachimba migodi Waselti waligundua kwamba mawe yenye madini yaliyopatikana mahali hapo yangeweza kufanywa kuwa chuma—metali iliyohitajika sana kwa kutengeneza vifaa na silaha zao. Waroma pia walichimba madini mahali hapo kwa karne nyingi.

Kwa kuwa madini yalipatikana kwenye mchanga usio na kina, wachimbaji hao wa zamani waling’oa mawe yenye madini kwa sururu na sepetu, na kuacha mamia ya mawe yasiyofaa yakiwa yamezagaa kila mahali. Bila kutarajia walifanyiza mandhari inayofanana na eneo lenye mawe ya chokaa yaliyopigwa na maji.

Hata hivyo baada ya Mvuvumuko wa Viwanda, mashine za kisasa zilitumiwa kuchimba mlima huo ili kutoa madini ya thamani yaliyosalia. Hatimaye, mabuldoza yalipokuwa yamefagia madini yote katika eneo hilo, mgodi huo ulifungwa mwaka wa 1989. Mashine chache zenye kutu mlangoni mwa Cabárceno ndio ishara pekee yenye kuonyesha shughuli ya viwanda iliyofanyika hapo.

Eneo Bovu Labadilika Kuwa Bustani

Pasipo shaka, ni rahisi zaidi kuharibu eneo kuliko ilivyo kulitengeneza. Pasipo kukata tamaa, wenye mamlaka katika mkoa wa Cantabria walianzisha kazi ya kufanyiza Bustani ya wanyama katika eneo hilo bovu sana.

Ili kufanikiwa walitegemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa dunia wa kujitengeneza upya. Zaidi ya hilo, wafanyakazi walijitahidi kurekebisha madhara yaliyotokezwa na utumizi mbaya na kutojali mazingira kwa karne nyingi. Kwa muda wa miaka kadhaa, maelfu ya miti ilipandwa, udongo wa juu ukawekwa upya, mashimo yasiyovutia yakajazwa maji na kuwa maziwa yenye kuvutia, na vijia vya reli vya awali kufanywa kuwa vijia vya kupitia watu. Hatimaye, wanyama bora waliochaguliwa kipekee waliwekwa ndani ya maboma makubwa kadhaa ili kurembesha mandhari hiyo mpya.

Wale wageni 600,000 wanaotembelea Bustani ya Wanyama ya Cabárceno kila mwaka wanahisi kwamba kazi hiyo haikuwa ya bure. Wengi wao wamepaaza sauti hivi kwa msisimko: “Hii ni paradiso!” Neno “paradiso” linafaa sana kwa sababu lilitumiwa na Waajemi na Wagiriki wa kale kurejezea bustani kubwa yenye maji ya kutosha, yenye uzuri usio na dosari ambamo wanyama walilisha huko wakiwa huru.

Kwa kuwa maeneo mengi ya asili yameharibiwa, inafurahisha kutembelea mahali ambapo uzuri umerudishwa upya na kurembwa ifaavyo. Isitoshe, kazi ambayo imefanywa kwa sehemu ndogo katika Cabárceno inaonyesha uwezo wa dunia yetu ya ajabu wa kujitengeneza.

Dubu wa rangi ya hudhurungi sasa hukwea sehemu zilizochimbwa na wachimba-migodi Waroma pindi fulani iliyopita. Tembo na swala hulisha kwenye maeneo yenye nyasi nzuri ambayo awali yaliharibiwa na wachimbaji. Simbamarara wachanga huchezacheza wakizunguka mawe ya matale yaliyochongoka wakati Waselti walipokuwa wakichimba madini. Na badiliko hilo lilichukua muda wa miaka michache tu!

Biblia inaahidi kwamba wakati mmoja, kulingana na kusudi la awali la Mungu kwa binadamu, dunia yote itakuwa paradiso. (Mwanzo 1:28; 2:15; Isaya 65:17, 22-25; Luka 23:42, 43) Bustani za wanyama kama hiyo ya Cabárceno hazitoi tu fursa ya kuona kimbele jinsi paradiso itakavyokuwa bali pia hutukumbusha kwamba Muumba wetu ana uwezo wa kutimiza ahadi hiyo.

[Picha katika ukurasa wa 23]

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]

Picha zote: Parque de la Naturaleza de Cabárceno