Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Athari za Kujaribu Kufanya Mambo Mengi Mno

Athari za Kujaribu Kufanya Mambo Mengi Mno

Athari za Kujaribu Kufanya Mambo Mengi Mno

NCHI ZA LEO ZA MAGHARIBI ZINAPENDA MNO KUFANYA MAMBO HARAKA-HARAKA NA KWA URAHISI.

MASHINE za kuoshea vyombo huokoa wakati jikoni. Mashine za kufulia nguo vilevile huokoa wakati wa kufua nguo. Mamilioni ya watu hawahitaji tena kutoka nyumbani ili kununua vitu au kufanya shughuli za benki—wao hufungua tu kompyuta yao na kutumia Internet.

Naam, ulimwengu, angalau kwa sehemu fulani, unafurika na kila aina ya mashine zenye kuokoa wakati na kupunguza kazi. Kwa sababu hiyo, ungedhani kwamba watu wangekuwa na wakati mwingi wa kuwa pamoja na familia zao na wa kupumzika. Lakini, mara nyingi, wengi husema kwamba wamelemewa na uchovu na mkazo zaidi kuliko awali. Sababu zinazosababisha hali hiyo ni nyingi na tata.

Mikazo ya kiuchumi ni mojawapo ya sababu kuu. Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya Uhusiano Viwandani cha Australia kilichanganua saa ambazo watu hutumia kazini na kupata kwamba “watu wengi hufanya kazi kwa ukawaida zaidi ya saa 49 kila juma” na kwamba “kuongezeka kwa saa za kazi huenda kukaathiri sana maisha ya familia na ya jumuiya.” Wafanyakazi wengi wanapendelea kuishi katika vitongoji vya mji vilivyo vitulivu na vyenye miti. Jambo hilo huwalazimu kutumia saa nyingi kila juma—au hata kila siku—wakisafiri kwa treni na basi zilizosongamana au katika barabara zenye magari tele. Pasina shaka, hilo huongeza shughuli za siku na mikazo yake.

Je, Una Deni la Usingizi?

Katika miaka ya hivi karibuni matatizo ya kupata usingizi yameenea sana hivi kwamba kliniki za matatizo ya usingizi zimeibuka katika sehemu nyingi za ulimwengu. Wachunguzi wamegundua kwamba watu ambao hawapati usingizi wa kutosha kwa ukawaida, hurundika deni la usingizi. Kwa asili, miili yao hutaka walipie deni hilo na huwalazimisha kufanya hivyo kwa kuwafanya wahisi wakiwa wachovu. Lakini kwa sababu ya mtindo-maisha wa kisasa wa watu kutolala usingizi wa kutosha, watu wengi huwa wachovu daima.

Katika nchi moja ya Magharibi, wakati wa kulala umepungua kwa asilimia 20 katika karne iliyopita, kutoka wastani wa saa tisa kila usiku hadi saa saba. Wachunguzi wamekusanya ushahidi chungu nzima unaoonyesha kwamba deni la usingizi husababisha matatizo ya kujifunza na kukumbuka mambo, kuharibika kwa misuli na kudhoofika kwa mfumo wa kinga. Wengi wetu tumegundua wenyewe kwamba akili chovu huelekea kufanya makosa. Kwa kusikitisha, baadhi ya makosa hayo huenda yakawa mazito na yenye kuleta hasara kubwa.

Gharama Kubwa ya Uchovu

Uchovu unaotokana na kufanya kazi kwa saa nyingi na kupunguzwa kwa wafanyakazi, yasemekana ulichangia baadhi ya misiba mibaya zaidi mwishoni mwa karne ya 20. Baadhi ya misiba hiyo ni ule wa nyuklia huko Chernobyl, Ukrainia; mlipuko wa chombo cha angani cha Challenger; na kumwagika kwa mafuta baada ya meli ya kubeba mafuta iitwayo Exxon Valdez kugonga tumbawe huko Prince William Sound, Alaska.

Mlipuko wa Chernobyl ulitokea wakati wa jaribio la pekee katika mtambo huo wa nguvu za nyuklia. Katika kitabu chake, The 24-Hour Society, Martin Moore-Ede asema kwamba jaribio hilo “lilisimamiwa na wahandisi wa umeme waliochoka ambao walikuwa wamefanya kazi katika mtambo huo kwa angalau saa kumi na tatu au hata zaidi kwa sababu idhini ya kuanza jaribio hilo ilichelewa kutolewa kwa muda wa saa kumi.” Vyovyote iwavyo, kulingana na uchunguzi wa hivi karibuni, athari moja ya muda mrefu ya mnururisho uliozuka ni kuongezeka mara kumi kwa kansa ya kikoromeo miongoni mwa watoto huko Ukrainia tangu mwaka wa 1986.

Baada ya uchunguzi kabambe wa mlipuko wa chombo cha angani cha Challenger, ripoti moja ya tume ya rais ilisema kwamba kiwango rasmi kisichozidi saa 20 kila juma cha kufanya kazi za ziada kilikiukwa mara 480 na kikundi kimoja cha wafanyakazi wa kandarasi na mara 2,512 na kikundi kingine. Ripoti hiyo yaongezea kusema kwamba uchovu wa wasimamizi, uliosababishwa na “kufanya kazi siku kadhaa kwa saa zisizo za kawaida na kutolala usingizi wa kutosha,” pia ni mojawapo ya sababu kuu zilizofanya idhini ya kurusha chombo hicho angani itolewe kimakosa. Ripoti hiyo ilisema kwamba “saa za ziada zikiwa nyingi kupita kiasi, umakinifu wa wafanyakazi hupungua na kuzidisha uwezekano wa kutokea kwa makosa ya kibinadamu.”

Kulingana na maofisa wa chama cha wafanyakazi, kupunguzwa kwa wafanyakazi, kwa minajili ya kupunguza gharama, kulisababisha mabaharia katika Exxon Valdez kufanya kazi nyingi kwa saa nyingi zaidi. Ripoti moja juu ya msiba huo inaeleza kwamba ofisa wa daraja ya tatu aliyekuwa ameshika usukani wa meli hiyo ilipokwama kwenye matumbawe baada tu ya usiku wa manane, hakuwa amelala tangu alfajiri. Takriban lita milioni 42 za mafuta—mafuta mengi sana kuwahi kumwagika huko Marekani—zilisababisha uharibifu mkubwa wa fuo na wanyama na usafishaji uligharimu zaidi ya dola bilioni 2 za Marekani.

Gharama Isiyoonekana ya Uchovu

Kulingana na kadirio moja, uchovu hugharimu ulimwengu angalau dola bilioni 377 kila mwaka! Lakini pesa haziwezi kabisa kulipia vifo na afya ambayo mara nyingi huathiriwa. Kwa mfano, fikiria aksidenti za barabarani. Kulingana na kliniki moja ya matatizo ya usingizi huko Sydney, Australia, kati ya asilimia 20 na asilimia 30 ya aksidenti zote za barabarani katika nchi hiyo husababishwa na madereva wanaosinzia wakiendesha magari. Inakadiriwa kwamba madereva wenye kusinzia wanapoendesha gari huchangia angalau aksidenti 100,000 za magari huko Marekani kila mwaka.

Isitoshe, huenda huo usiwe mwisho wa matokeo ya uchovu. Jeruhi wa aksidenti anayepelekwa haraka hospitalini anatazamia kumpata daktari aliye chonjo. Lakini kwa sababu ya shughuli chungu nzima na kufanya kazi kwa saa nyingi huenda daktari akawa amechoka! Ripoti moja ya Taasisi ya Afya na Hali Njema ya Australia, ilifunua kwamba asilimia 10 ya madaktari hufanya kazi zaidi ya saa 65 kila juma, asilimia 17 ya wataalamu wote hufanya kazi kwa muda unaozidi huo, na asilimia 5 ya “madaktari wachanga” hufanya kazi zaidi ya saa 80 kila juma!

“Mashine hulindwa na vitabu vya maagizo na vibandiko vyenye kuonya na pia watu huzoezwa jinsi ya kuzitumia,” asema Martin Moore-Ede. “Binadamu hana ulinzi wowote kama huo. . . . Ukweli wenye kushtua ni kwamba tunajua mambo mengi kuhusu mashine na kompyuta tunazotumia kuliko tujuavyo mwili wa binadamu.”

Mwili wetu hauna taa nyekundu zenye kumweka au kengele za kutuonya tusimame au tupunguze mwendo. Hata hivyo, mwili hutoa dalili za kuonya. Dalili hizo zatia ndani uchovu wa daima, kubadilika-badilika kwa hisia-moyo, mshuko-moyo, na mwelekeo wa kupatwa na magonjwa kwa urahisi. Ikiwa una dalili hizo—tuseme huna ugonjwa au matatizo mengine ya afya—basi inafaa uchunguze mtindo wako wa maisha.

Gharama za Kijamii za Kuwa Mwenye Shughuli Nyingi Mno

Mtindo wa maisha wenye mikazo na kutolala usingizi wa kutosha huathiri pia uhusiano wa binadamu. Fikiria kisa cha John na Maria, wenzi waliofunga ndoa hivi karibuni. * Walitaka vitu vinavyotamaniwa na wenzi wengi waliooana karibuni—nyumba nzuri na pesa nyingi. Kwa hiyo, wote walianza kufanya kazi wakati wote. Lakini kwa sababu ya kufanya kazi kwa zamu mbalimbali, hawakupata wakati wa kuwa pamoja. Punde si punde, uhusiano wao ukaanza kuzorota. Walipuuza dalili na kuendelea na shughuli zao nyingi hadi ndoa yao changa ikavunjika.

“Uchunguzi waonyesha kwamba kiwango cha talaka kati ya wenzi wa ndoa wanaofanya kazi ya zamu kinazidi kwa asilimia 60 kile cha wenzi wanaofanya kazi saa za kawaida,” chasema kitabu The 24-Hour Society. Hata hivyo, wawe wanafanya kazi ya zamu au la, wenzi wengi huwa na shughuli nyingi zinazoangamiza ndoa yao. Kwa wengine, huenda mkazo na uchovu ukawatumbukiza katika zoea la kutumia dawa za kulevya na pombe isivyofaa na kukosa kula vizuri—hayo hayazidishi tu uchovu bali yaweza kusababisha matatizo mengine mengi, kama vile kuwatendea watoto vibaya.

Ili kuwasaidia wazazi wakabiliane na ratiba zao zenye shughuli nyingi, makao ya kutunzia watoto yameongezeka, mengine yanatoa huduma saa 24. Isitoshe, televisheni ni mlezi halisi wa watoto wengi. Bila shaka, ikiwa watoto wanatazamiwa kukua na kuwa watu waliokomaa, wenye mazoea mazuri ya kihisia moyo, wazazi wanahitaji kutumia wakati mwingi pamoja nao. Ndiposa, wazazi ambao hawajishughulishi na watoto wao kwa sababu wamechoka sana wakijaribu kudumisha kiwango cha juu sana cha maisha, wanapaswa kujiuliza kama jitihada zao zina manufaa yoyote—kwao na kwa watoto wao.

Watu wazee-wazee pia wameathiriwa na mwendo wa kasi wa maisha na tekinolojia ya siku hizi. Mabadiliko ya kasi na furiko la vyombo vipya, hufanya wengi wajihisi wamevurugika, hawana usalama, wahofu, au hata kuhisi hawafai kitu. Kwa hiyo, wanaweza kutarajia nini wakati ujao?

Je, sote—wakubwa kwa wadogo—tuko chini ya udhibiti kamili wa ulimwengu unaokaza mwendo zaidi na zaidi? Au kuna mambo tuwezayo kufanya ili tukabiliane na hali na kuboresha maisha yetu? Kwa kupendeza, kuna mambo tuwezayo kufanya kama tutakavyoona katika makala ifuatayo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 20 Majina yamebadilishwa.

[Picha katika ukurasa 6]

Uchovu huenda ulichangia msiba wa nyuklia huko Chernobyl, mlipuko wa chombo cha angani cha “Challenger” na kumwagika kwa mafuta ya meli ya “Exxon Valdez”

[Hisani]

Courtesy U.S. Department of Energy’s International Nuclear Safety Program

NASA photo

[Picha katika ukurasa 7]

Hekaheka za maisha zaweza kuleta matatizo katika ndoa

[Picha katika ukurasa 8]

Ili wakabiliane na hali, watu fulani hutumia pombe isivyofaa