Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Matibabu ya Asili Kinachowafanya Wengi Wayatumie

Matibabu ya Asili Kinachowafanya Wengi Wayatumie

 Matibabu ya Asili Kinachowafanya Wengi Wayatumie

MATIBABU ya asili, au ya ziada, huwa na mbinu chungu nzima za matibabu. Mengi huitwa kwa ujumla naturopathy (matibabu ya asili), hiyo ni njia ya matibabu inayotegemea sana vitu vya asili au mbinu nyingine za kuuweka mwili katika hali fulani na kuuruhusu upone pasipo dawa. Idadi kubwa ya matibabu hayo, ambayo yametumiwa sana kwa karne nyingi, sasa yameachwa au kupuuzwa katika matibabu ya kisasa.

Mathalani, jarida la Journal of the American Medical Association la Agosti 27, 1960, lilisema  kwamba zoea la kutuliza majeraha ya kuchomeka kwa baridi “lilitumiwa na watu wa kale lakini yaonekana limepuuzwa na madaktari na watu wa kawaida vilevile. Licha ya kwamba vichapo hurejezea na kusifu matibabu hayo mara kwa mara, kwa ujumla hayatumiwi leo. Kwa kweli, madaktari wengi husema tu ‘hayatumiwi na yeyote leo,’ ingawa hakuna mtu ajuaye sababu.”

Hata hivyo, kutuliza majeraha ya kuchomeka kwa maji baridi au kwa barafu kumeungwa mkono tena na matibabu yasiyo ya asili katika miongo ya karibuni. Jarida la The Journal of Trauma, la Septemba 1963, liliripoti hivi: “Zoea la kutumia maji baridi katika matibabu ya mapema ya majeraha ya kuchomeka limesitawi tangu kutolewa kwa ripoti za Ofeigsson na Schulman mnamo mwaka wa 1959 na 1960. Tuliwatibu wagonjwa mwaka uliopita kwa kutumia njia hiyo; matokeo ya matibabu hayo yalikuwa yenye kutia moyo.”

Kutibu kwa maji baridi ni salama kwa kadiri fulani, na bila shaka humtuliza mgonjwa. Kutibu magonjwa kwa njia mbalimbali kwa kutumia maji (Hydrotherapy), hutumiwa katika matibabu ya asili, na sasa matibabu mbalimbali ya aina hiyo yanatambuliwa pia na matibabu ya kisasa. *

Vivyo hivyo, wataalamu wa matibabu ya asili mara nyingi hutibu magonjwa kwa kutumia mimea. Hilo ni zoea ambalo limedumu kwa mamia—hata maelfu—ya miaka katika sehemu fulani duniani. Kwa mfano, huko India mitishamba imekuwa nguzo muhimu ya matibabu kwa muda mrefu. Leo, uwezo wa kuponya wa mimea fulani umetambuliwa kotekote na wataalamu wengi wa afya.

Tukio Muhimu

Miaka 100 hivi iliyopita, Richard Willstätter, ambaye alikuja kuwa mwanafunzi wa biokemia ya mimea, alichochewa na mambo yaliyompata rafikiye wa karibu aliye mchanga, Sepp Schwab mwenye umri wa miaka kumi. Mguu wa Sepp ulikuwa umeambukizwa vibaya sana hivi kwamba daktari alisema mguu huo ulihitaji kukatwa ili kuokoa uhai wake, lakini wazazi wa Sepp waliahirisha shughuli hiyo hadi asubuhi iliyofuata. Wakati huohuo, walimfikia mchungaji mmoja aliyekuwa tabibu hodari wa madawa ya mitishamba. Mchungaji huyo alikusanya mimea mbalimbali, akaikatakata vipande vidogo sana hadi iliposhabihi mchicha uliopikwa, kisha akaitia penye jeraha.

Jeraha lilipata nafuu kabla ya alasiri, na shughuli ya kumkata mguu ikaahirishwa tena. Aliendelea kupata matibabu hayo, na baada ya muda, jeraha hilo likapona kabisa. Willstätter aliendelea kujifunza kemia katika Chuo Kikuu cha Munich huko Ujerumani, na baadaye akashinda tuzo ya Nobeli kwa sababu ya uvumbuzi aliofanya kuhusiana na  rangi ya asili ya mimea, hususan klorofili. Jambo muhimu ni kwamba asilimia 25 ya madawa ya tiba yanayotumika sasa yametengenezwa kikamili au kwa sehemu kutokana na kemikali zinazopatikana kiasili katika mimea.

Uhitaji wa Kuwa na Usawaziko

Lakini yapasa kukumbukwa kwamba matibabu yanayomsaidia kabisa mtu mmoja huenda yasimsaidie sana mwingine. Kufaulu kwa matibabu yoyote hutegemea mambo mengi, kutia ndani aina ya ugonjwa na afya ya ujumla ya mgonjwa. Hata wakati waweza kuathiri matokeo.

Matibabu ya asili kwa ujumla hufanya kazi polepole kuliko matibabu yasiyo ya asili, kwa hiyo ugonjwa ambao huenda ungekomeshwa endapo ungegunduliwa na kutibiwa mapema waweza kukomaa na kuhitaji madawa yenye nguvu—labda hata upasuaji ufanywe—ili kuokoa uhai. Kwa hiyo huenda lisiwe jambo la hekima kushikilia tu aina moja ya matibabu kana kwamba hiyo pekee ndiyo inayoweza kuponya ugonjwa fulani.

Matibabu ya asili hutofautiana na matibabu yasiyo ya asili katika masuala ya afya. Kwa kawaida mbinu zake za kuponya hulenga kuzuia ugonjwa, nazo hukazia mtindo wa maisha na mazingira ya mtu na mambo hayo yanavyoathiri afya yake. Yaani, wataalamu wa matibabu ya asili kwa ujumla humchunguza mtu kikamili badala tu ya kiungo kinachougua au hali ya ugonjwa.

Bila shaka, wengi huvutiwa sana na matibabu ya asili kwa sababu ya dhana ya kwamba matumizi yake ya bidhaa za kiasili na mbinu zake za matibabu hutuliza, nazo si hatari sana kama zile zinazotumiwa katika matibabu yasiyo ya asili. Hivyo basi, kwa sababu ya watu wengi kutaka kujua matibabu yaliyo salama na yenye matokeo, makala ifuatayo itazungumzia mifano michache ya matibabu ya asili.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Ona Amkeni!, Juni 22, 1988, ukurasa wa 25-26, (la Kiingereza).