Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jaribio la Kutimua Vatikani Kutoka UM

Jaribio la Kutimua Vatikani Kutoka UM

 Jaribio la Kutimua Vatikani Kutoka UM

SHIRIKA la habari la huko Roma, Inter Press Service (IPS) liliripoti kwamba, “muungano wa mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali (NGO) zaidi ya 70 umeanzisha kampeni ya ulimwenguni pote ya kutimua Vatikani kutoka kwa Umoja wa Mataifa.” Kwa sasa, Vatikani ni mtazamaji wa kudumu, au taifa lisilo mwanachama, wa shirika hilo la UM. Vatikani imekuwa na wadhifa huo tangu mwaka wa 1964.

Kwa nini mashirika haya ya NGO, ambayo mwishoni mwa Aprili mwaka uliopita yalikuwa yameongezeka hadi 100 ulimwenguni pote, yanapinga kuwepo kwa Vatikani katika UM? Mashirika hayo yanabisha kwamba Vatikani ni mamlaka ya kidini wala si ya kisiasa (NGO). Msimamizi wa Wakatoliki Wenye Uhuru wa Chaguo, Frances Kissling, aliliambia shirika la habari la IPS kwamba muungano huo haupingi haki ya Vatikani kutoa maoni yake, lakini “linalobishaniwa ni swala la shirika lisilo la kisiasa kuwa na wadhifa sawa na serikali.”

Mkurugenzi wa Programu za Kimataifa katika Kituo cha Sheria na Sera ya Uzazi, Anika Rahman, alikubaliana na maoni hayo. Shirika la habari la IPS lilimnukuu akisema kwamba “iwapo UM unaipa Makao ya Papa pendeleo la kuwa mtazamaji wa kudumu kwa sababu ya mamlaka yake ya kidini, basi shirika hilo la kimataifa linachochea dini nyingine ziombe pendeleo lilo hilo.” Aliongeza kusema hivi: “Ili kuhakikisha kwamba Umoja wa Mataifa haupendelei dini fulani, basi matengenezo ya kidini kama vile Kanisa Katoliki hayapasi kuruhusiwa kuwa sehemu ya UM yakiwa watazamaji.”

Lakini vipi lile dai la kwamba Vatikani ni taifa na hivyo linastahili wadhifa wake wa sasa? Bi. Kissling alipokuwa akihojiwa alisema kwamba “hayo ni maneno yenye kupotosha. Sisi twasema kwamba, ufasili huo wa taifa na Vatikani ulikuwa wa karne ya 15, na kwamba kwa kweli muundo wa mamlaka ya Makao ya Papa ni wa kidini.” Alisema pia kwamba maneno “Vatikani” na “Makao ya Papa” yana “maana moja na Kanisa Katoliki.”

Hasa kinachoyaudhi mashirika ya NGO kuhusu wadhifa wa Vatikani katika UM ni maoni yake juu ya mambo ya uzazi. Kwa mfano, Vatikani imetumia warsha za UM kama ile Warsha ya Kimataifa Juu ya Idadi ya Watu na Maendeleo huko Cairo mnamo mwaka wa 1994, na ile Warsha ya Wanawake ya mwaka wa 1995 huko Beijing, kupinga vikali kupanga uzazi. “Kwa kuwa UM hufanya maamuzi yake kupitia upigaji-kura,” lasema shirika la habari la IPS, “maoni yenye kupinga kama yale ya Vatikani yameongoza kushindwa kwa mijadala kuhusu idadi ya watu, kupanga uzazi, haki za wanawake na utunzaji wakati wa uzazi.”

Kulingana na Bi. Kissling, “uhusiano wa Vatikani wapasa kuwa wa shirika la NGO—sawa na yale mashirika mengine ya NGO yanayowakilisha Waislamu, Wahindu, Wabudha, Wabahai na mashirika mengine ya kidini.” Muungano huo unamtaka katibu-mkuu wa UM Kofi Annan na hatimaye Baraza Kuu la UM kuchunguza rasmi wadhifa wa Vatikani katika shirika hilo la kisiasa lililo kubwa zaidi ulimwenguni.

[Picha katika ukurasa wa 31]

Mwakilishi wa Vatikani akihutubia UM

[Hisani]

UN/DPI Photo by Sophie Paris

UN photo 143-936/J. Isaac