Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Dunia Je, ‘Misingi Yake Iliwekwa’ kwa Nasibu?

Dunia Je, ‘Misingi Yake Iliwekwa’ kwa Nasibu?

Dunia Je, ‘Misingi Yake Iliwekwa’ kwa Nasibu?

NI SHARTI dunia izunguke umbali unaofaa kabisa kutoka kwa jua ili isiwe na halijoto inayopita kiasi. Sayari zinazozunguka nyota zinazoshabihi jua zimegunduliwa katika mifumo mingine ya jua, nazo huonwa kuwa ‘sayari zinazoweza kukalika’—yaani, maji yaweza kudumu huko. Lakini hata zile zinazoitwa eti sayari zinazoweza kukalika huenda zisifae uhai wa mwanadamu. Lazima pia zizunguke kwa mwendo unaofaa na ziwe na ukubwa unaofaa.

Kama dunia ingekuwa ndogo na nyepesi kuliko ilivyo, nguvu za uvutano zingekuwa dhaifu zaidi na sehemu kubwa ya angahewa yake muhimu ingetokomea angani. Ndivyo ilivyo kwa mwezi na sayari mbili za Zebaki na Mihiri. Hazina angahewa kwa sababu ni ndogo zaidi na zina uzito mdogo kuliko dunia. Vipi ikiwa dunia ingekuwa kubwa kidogo na nzito kuliko ilivyo?

Basi nguvu za uvutano za dunia zingeongezeka zaidi, na gesi nyepesi, kama vile hidrojeni na heli, zingedumu katika angahewa kwa muda mrefu zaidi. “Na jambo kubwa hata zaidi ni kwamba,” chaeleza kichapo cha sayansi cha Environment of Life, “usawaziko nyeti wa gesi za angahewa ungevurugika.”

Au fikiria tu oksijeni, ambayo inachochea moto. Kama kiwango chake kingeongezeka kwa asilimia moja, mioto ya msitu ingetukia mara nyingi zaidi. Kwa upande mwingine, endapo gesi ya kaboni inayozidisha joto duniani ingezidi kuongezeka, basi tungechomwa na joto kali zaidi duniani.

Mzunguko wa Dunia

Umbo la mzunguko wa dunia linafaa sana pia. Ikiwa dunia ingezuka kwa duaradufu zaidi, halijoto ya dunia ingepita kiasi sana tusivyoweza kustahimili. Badala yake, dunia inazunguka kwa umbo linalokaribia kuwa duara. Bila shaka, hali ingebadilika endapo sayari kubwa sana kama Jupita ingepita karibu na dunia. Katika miaka ya majuzi wanasayansi wamepata uthibitisho wa kwamba sayari kubwa sana zinazofanana na Jupita huzunguka karibu sana na nyota nyingine. Idadi kubwa ya sayari hizo zinazofanana na Jupita huzunguka kwa umbo la yai. Kama kungekuwapo sayari nyingine kama dunia katika mifumo hiyo basi zingekabili matatizo.

Mtaalamu wa nyota Geoffrey Marcy alilinganisha mifumo hiyo ya mbali ya sayari na zile sayari nne Zebaki, Zuhura, Dunia, na Mihiri, ambazo hufanyiza sehemu iliyo karibu ya mfumo wetu wa jua. Katika mahoji, Marcy alisema hivi kwa mshangao: “Tazama jinsi [utaratibu] huu ulivyo kamili. Ni kama kito. Kuna mizunguko ya duara. Yote iko katika usawa uleule. Yote inazunguka kuelekea upande mmoja. . . . Ni jambo la pekee sana.” Je, kweli yaweza kuwa ilitokea kwa nasibu?

Mfumo wetu wa jua una jambo jingine la kustaajabisha. Zile sayari kubwa sana za Jupita, Zohali, Uranusi, na Kausi huzunguka jua mbali sana na dunia yetu. Badala ya kuwa tisho, sayari hizo hutimiza fungu muhimu. Wataalamu wa nyota huzilinganisha na ‘vifyonza-vumbi vya kimbingu’ kwa sababu nguvu zake za uvutano hufyonza mawe makubwa yanayotoka katika nyota, ambayo yanaweza kuhatarisha uhai duniani. Kwa kweli, dunia ‘imewekwa kwa misingi’ imara. (Ayubu 38:4) Ina ukubwa unaofaa na iko mahali barabara katika mfumo wetu wa jua. Kuna mengi zaidi. Dunia ina mambo mengi ya pekee ambayo ni muhimu kwa uhai wa wanadamu.

Oksijeni na Usanidi-Nuru

Atomu za oksijeni hufanyiza asilimia 63 ya uzani wa viumbe-hai duniani. Isitoshe, oksijeni iliyo katika angahewa ya juu zaidi hukinga mimea na wanyama walio duniani kutokana na miali ya urujuanimno ya jua. Lakini oksijeni huathiri elementi nyingine mara moja, kama inavyoathiri chuma na kusababisha kutu. Hivyo basi, angahewa huweza kudumishaje kiwango chake cha asilimia 21 cha elementi hiyo inayoathiri vitu vingine upesi?

Ni kwa sababu ya usanidi-nuru—hali ya kustaajabisha ambapo mimea iliyo duniani hutengeneza chakula kwa nuru ya jua. Kinachosalia kutokana na usanidi-nuru ni oksijeni—zaidi ya tani bilioni moja za oksijeni huongezwa kwenye angahewa kila siku. “Pasipo usanidi-nuru,” chaeleza kichapo The New Encyclopædia Britannica, “si kwamba tu uzalishaji wa chakula muhimu utakoma, bali pia Dunia itakosa oksijeni hatimaye.”

Vichapo vya sayansi hueleza kwa kurasa kadhaa hali ya usanidi-nuru inayotukia hatua kwa hatua. Hatua nyingine bado hazijaeleweka kikamili. Wanamageuzi hawawezi kueleza jinsi kila hatua ilivyogeuka kutoka kwa kitu kingine sahili. Kwa kweli, kila hatua yaonekana kuwa tata sana kiasi cha kutorahisishwa. “Hakuna maoni yanayokubaliwa na wote kuhusu chanzo cha hali ya usanidi-nuru,” chakiri kitabu The New Encyclopædia Britannica. Mwanamageuzi mmoja alitatua tatizo hilo kijuu-juu kwa kusema kwamba usanidi-nuru “ulibuniwa” na “chembe chache anzilishi.”

Taarifa hiyo isiyo ya kisayansi, inafunua jambo jingine linalostaajabisha pia: Usanidi-nuru huhitaji ukuta wa chembe ambamo hali hiyo yaweza kutukia ifaavyo, na kuendelea kwa usanidi-nuru hutegemea kuzaana kwa chembe. Je, yote hayo yalitukia kwa nasibu tu katika “chembe chache anzilishi”?

Kutoka kwa Chembe Inayozaana Hadi kwa Mwanadamu

Kuna uwezekano gani wa atomu kukusanyika pamoja kwa nasibu na kutokeza chembe sahili zaidi inayozaana? Katika kitabu chake A Guided Tour of the Living Cell, mwanasayansi aliyeshinda Tuzo la Nobeli Christian de Duve akiri hivi: “Hutaweza kwa umilele wote kuona chembe ya bakteria hata moja ikiibuka kutokana na mwungano wa atomu zake kwa nasibu.”

Baada ya kuzungumzia kirefu habari hiyo, acheni tupige hatua kubwa sana kutoka kwa chembe ya bakteria hadi kwa mabilioni ya chembe za pekee za neva zinazofanyiza ubongo wa mwanadamu. Wanasayansi wanasema kwamba ubongo wa mwanadamu ndicho kitu tata zaidi katika ulimwengu wote. Kwa kweli hauna kifani. Kwa mfano, sehemu kubwa za ubongo wa mwanadamu huitwa vituo vya habari. Vituo hivyo huchanganua na kufasiri ujumbe kutoka kwa sehemu ya ufahamu ya ubongo. Mojawapo ya vituo hivyo kilichoko nyuma ya kipaji chako cha uso hukuwezesha kutafakari maajabu ya ulimwengu. Je, vituo hivyo vya habari viliibuka kwa nasibu? “Hakuna mnyama awaye yote aliye na vituo kama hivyo vya pekee,” akiri mwanamageuzi Dakt. Sherwin Nuland katika kitabu chake The Wisdom of the Body.

Wanasayansi wamethibitisha kwamba ubongo wa mwanadamu huchanganua habari kwa kasi zaidi kuliko kompyuta iwayo yote. Kumbuka kwamba tekinolojia ya kisasa ya kompyuta imetokana na jitihada za wanadamu za makumi mengi ya miaka. Vipi ubongo wa mwanadamu ulio bora zaidi? Wanasayansi wawili, John Barrow na Frank Tipler, wakiri ifuatavyo katika kitabu chao The Anthropic Cosmological Principle: “Wanamageuzi wamefikia mkataa wa kwamba mageuzi ya viumbe wenye akili, wenye uwezo wa kuchanganua habari kama wanadamu, hayangeweza kutukia na pia haielekei kwamba yamewahi kutukia katika sayari nyingine yoyote katika ulimwengu wote mzima unaoonekana.” Kuwapo kwetu, wanasayansi hao wakata shauri, ni “nasibu njema kabisa.”

Je, Yote Yalitokea kwa Nasibu?

Umefikia mkataa gani? Je, kweli ulimwengu pamoja na maajabu yake yote waweza kuwa ulitokea kwa nasibu? Je, wewe hukubali kwamba kila muziki uliopigwa vizuri sana lazima uwe na mtungaji na kwamba ala zote lazima zipangwe vizuri ili zipendeze? Namna gani ulimwengu wetu wenye kustaajabisha? “Twaishi katika ulimwengu uliopangwa barabara kabisa,” asema mwanahisabati na mtaalamu wa nyota David Block. Afikia mkataa gani? “Ulimwengu wetu ni makao. Naamini kwamba yamebuniwa na Mungu.”

Ikiwa umefikia mkataa huo, basi bila shaka utakubaliana na maelezo haya ya Biblia kuhusu Muumba, Yehova: “Ameiumba dunia kwa uweza wake, ameuthibitisha ulimwengu kwa hekima yake, na kwa ufahamu wake amezitanda mbingu.”—Yeremia 51:15.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

SAYARI YA PEKEE

“Maji yaliweza kukusanyika kwenye dunia kwa sababu ya hali za pekee zilizo duniani zinazosababishwa na ukubwa wake unaofaa, elementi zilizomo, na mzunguko wake ulio nusura ya duara, umbali barabara kutoka kwa nyota iliyodumu muda mrefu, yaani jua. Ni vigumu sana kuwazia mwanzo wa uhai bila maji.”—Integrated Principles of Zoology, Toleo la Sita.

[Hisani]

NASA photo

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

UHAI—ULITOKEA KWA NASIBU?

Mnamo mwaka wa 1988 kitabu kinachojaribu kueleza jinsi uhai ulivyotokea kwa nasibu kilizungumziwa katika jarida Search, linalochapishwa na Shirika la Australia na New Zealand la Maendeleo ya Sayansi. Kwenye ukurasa mmoja tu wa kitabu hicho, mwandikaji wa sayansi L. A. Bennett alipata “taarifa 16 zisizo na msingi kabisa, kila taarifa ikitegemea uthibitisho wa ile inayotangulia.” Bennett alifikia mkataa gani baada ya kusoma kitabu chote? “Ni rahisi zaidi,” akaandika, “kukubali kwamba Muumba mwenye upendo aliumba uhai mara moja na kuuelekeza kupatana na kusudi lake . . . badala ya kukubali ‘nasibu [chungu nzima] zisizo na mwelekeo’ ambazo zahitajiwa ili kutetea hoja za mtungaji.”

[Picha]

Usanidi-nuru ni muhimu sana katika utengenezaji wa chakula na oksijeni

Ni nini kinachotokeza hali zinazofaa za dunia ambazo ni muhimu katika kutegemeza uhai?

Wanasayansi wanasema kwamba ubongo wa mwanadamu ndicho kitu tata zaidi katika ulimwengu wote. Ungeweza kutokeaje kwa nasibu?

[Hisani]

Picha: Zoo de la Casa de Campo, Madrid

Monte Costa, Sea Life Park Hawaii

[Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Ukubwa wa sayari umepunguzwa

Jua

Zebaki

Zuhura

Dunia

Mihiri

Jupita

Zohali

Uranusi

Kausi

Utaridi

[Hisani]

Jua: National Optical Astronomy Observatories; Zebaki, Jupita, na Zohali: Courtesy of NASA/JPL/Caltech/USGS; Zuhura na Uranusi: Courtesy of NASA/JPL/Caltech; Dunia: NASA photo; Mihiri: NASA/JPL; Kausi: JPL; Utaridi: A. Stern (SwRI), M. Buie (Lowell Obs.), NASA, ESA