Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kufanya Usafiri wa Ndege Uwe Salama Zaidi

Kufanya Usafiri wa Ndege Uwe Salama Zaidi

Kufanya Usafiri wa Ndege Uwe Salama Zaidi

RUBANI mkuu asukuma mbele vali ya kudhibiti mvuke wa petroli, na msaidizi wake atoa ishara ya kuwa wamepokea kibali kutoka kwa mnara wa kuongozea ndege. Nikiwa nimeketi nyuma ya marubani hao nahisi moyo wangu ukinienda kasi wakati injini za ndege zinaponguruma kwa nguvu. Nahisi nikivutwa nyuma kwa nguvu ndege hii aina ya Boeing 747 inapoongeza mwendo. Kisha, bila matatizo yoyote, tuko hewani, na barabara ya ndege namba 34 katika Uwanja Mpya wa Ndege wa Kimataifa wa Tokyo yabaki nyuma chini yetu.

Hatari Hewani!

Punde si punde, twasikia kishindo kikubwa na ndege yaanza kuyumbayumba na kugeuka kwa nguvu. Sauti kali inajaa chumba cha rubani. Ni king’ora! Taa kadhaa za rangi nyekundu na za kaharabu zawaka kwenye sehemu ya vifaa vya kuendeshea ndege huku rubani msaidizi akijaribu kuinyoosha ndege.

“Injini namba tatu imeshika moto!” rubani mkuu apaaza sauti huku akibonyeza kitufe ili kuzima king’ora. “Injini imekwama, mafuta hayana kanieneo, wala hakuna nishati katika injini namba tatu,” asema rubani msaidizi. “Punguza mafuta kwenye injini namba tatu. Kata mafuta kabisa kwenye namba tatu. Namba tatu haitumiki tena.” Kila amri inapotolewa, mmoja wa marubani anaitekeleza, na mwenzake ahakikisha imefanywa. Wanasonga huku na huku kwa wakati unaofaa, kana kwamba ni mtu mmoja, na mambo yanakuwa mazuri. Nimeshangazwa na utulivu wao wanapojitahidi kutengeneza mambo.

Halafu, rubani msaidizi awasiliana kwa redio na mnara wa kuongozea ndege akiomba ruhusa ya kutua kwa dharura na kuagiza vyombo vyenye kutumika wakati wa dharura viwekwe tayari. Kisha, aarifu wahudumu wa ndani ya ndege kutayarisha abiria kwa ajili ya kutua kwa dharura.

Marubani wanapokuwa wakifanya matayarisho yao ya dharura, mimi najaribu kupangusa jasho usoni wakati uleule nikiwa nimeshikilia sana kiti changu! Natulia wakati ndege inapotua bila matatizo yoyote. Najiona mpumbavu kwa kuhofu sana hivyo. Yaani, hayo yote hayakuwa mambo halisi. Sikuwa nikipaa kwa ndege huko Japani. Nilikuwa nimeketi ndani ya chombo cha kisasa zaidi kinachoiga hali halisi za usafiri (kinachofanana na kile kimeonyeshwa hapo juu) katika Kituo cha Mafunzo ya Uendeshaji-Ndege cha Shirika la Ndege la United Airlines, huko Denver, Colorado, Marekani. Wafanyakazi wa ndege walikuwa tu kwenye mafunzo. Nilisisimuliwa sana na jambo hili kwa kuwa nina ujuzi wa kuendesha vyombo vya aina hiyo kwenye kompyuta ndogo.

Kuiga kwa Minajili ya Usalama

Hali sawa na hiyo hurudiwa mara nyingi na wafanyakazi wa ndege kwenye vyombo vya kuiga hali halisi ya usafiri sawa na hiki. Kwa nini? Kwa ajili ya mafunzo yao na pia usalama wa abiria wanaosafiri—yaani usalama wako. Lakini, kwa nini mafunzo hayo yafanywe kwenye vyombo hivyo na wala si ndani ya ndege halisi? Kuna sababu nyingi, lakini kabla ya kuzieleza, acheni kwanza tuone jinsi ambavyo uigaji wa hali halisi za usafiri umepata kusitawi.

Wakati wa vita ya ulimwengu ya kwanza na ya pili, uhitaji wa marubani wenye ujuzi ulikuwa mkubwa na hivyo shule za mafunzo ya uendeshaji wa ndege zenye kutumia vyombo duni vya kuiga hali halisi zilianzishwa. Mwishoni mwa miaka ya 1960, ufundi wa vyombo vya kuiga hali halisi ya usafiri uliboreka sana, kwa hiyo vyombo hivyo vikaanza kufanana na ndege halisi. Hata vyombo hivyo vikawa na uwezo wa kuiga mambo madogo-madogo yaliyo magumu kutambua, kama vile utendaji wa ndege kulingana na uzito wake na kiasi cha mafuta kilichomo. Mambo hayo huathiri uendeshaji wa ndege. Kisha, inaposafiri mafuta huzidi kupungua na hilo hubadili mwendo wa ndege. Maendeleo katika tekinolojia ya elektroni na ya kompyuta yamewezesha kuiga hali hizo na hali nyingine nyingi.

Lengo ni kuweza kutengeneza vyombo vinavyoiga hali halisi za usafiri. Ili kutimiza lengo hilo, vyombo vya kisasa vya kuiga usafiri vimewekewa msingi wenye nguvu wa haidroliki wenye uwezo wa kusogea kwa njia mbalimbali. Mfumo huo unaendeshwa na mabomba makubwa ya haidroliki yenye uwezo wa kuwafanya wafanyakazi wa ndege wahisi kwa muda mwendo wenye kani ya +1 g hadi -1 g. *

Marubani wanaposhika-shika vidude vya uendeshaji, wanaweza kuona matokeo katika muda unaofaa—yanayolingana barabara na yale ambayo wangeona ndani ya ndege halisi. Kuongeza mwendo, kupunguza mwendo, kuyumbayumba, kutua na kukwaruza, na hali ya hewa, yote hayo rubani huyasikia siyo kwa masikio yake tu bali pia huyahisi kwa mwili wake wote.

Maendeleo yamefanywa ya kutumia mifumo ya kompyuta inayoonyesha picha za viwanja hususa vya ndege duniani pamoja na mandhari yake. Picha hizo zilizo halisi kabisa huonyeshwa kwenye skrini zinazozingira sehemu ya mbele ya chumba cha rubani cha kuiga. Pembe ya picha hiyo ni yenye upana wa digrii 180 na urefu wa digrii 40. Vyombo vyenye kuiga hali halisi ya usafiri huwaruhusu marubani “kuendesha ndege” katika aina zote za hali ya hewa—theluji, mvua, radi, mvua ya mawe, na ukungu—iwe mchana, jioni au usiku.

Kutembelea Chombo cha Kuiga Hali Halisi ya Usafiri

Mwingilio wa chombo nilichotembelea ulikuwa daraja la chuma lenye upana wa meta sita ambalo linatenganisha “nchi” na sanduku kubwa jeupe lisilo na dirisha na lililowekwa juu ya jukwaa kubwa. Sanduku hilo linashabihi chombo cha angani au buibui mkubwa sana.

Mara uingiapo unahisi kana kwamba umeingia ndani ya chumba cha rubani katika ndege halisi. Utaona vidude vyote vinavyoonyesha vipimo, taa za indiketa, geji mbalimbali, swichi tofauti-tofauti, na nyenzo zimepangwa sawa kama zilivyo kwenye ndege halisi. Terry Bansept, anayenitembeza, ni fundisanifu wa vyombo hivyo vya kuiga hali halisi ya usafiri na aliniambia kwamba vielekezi vingi katika vyombo hivyo ni vyombo halisi vya ndege.

Terry alieleza kwamba vyombo hivyo vimejengwa vikiwa na vipimo, umbo na uwezo sawasawa na chumba halisi cha rubani katika ndege mbalimbali. Kadiri ambavyo usitawi wa ufundi huu wa kuiga hali umesonga mbele, ndivyo wajuzi wa usafiri wa ndege wamegundua kwamba vyombo vyenye kuiga hali halisi ya usafiri hutoa mazoezi ya hali ya juu kwa wafanyakazi wa ndege. Zaidi ya kuwazoeza marubani kuendesha ndege, mpango huo hutia ndani pia mafunzo ya hatua za kuchukua wakati wa dharura.

Iwapo kuiga hali halisi ya usafiri chafikia kiwango fulani cha usahihi, marubani hurekodi wakati ambao wamekuwa ndani ya chombo hicho, kama tu wafanyavyo katika safari ya ndege halisi. Katika hali fulani, huenda mafunzo na mitihani yote ya rubani ikafanywa kwenye chombo hiki.

Kwa Nini Vyombo Hivi Vitumiwe?

Vyombo hivi hutimiza makusudi kadhaa yenye faida. Kuvitumia badala ya ndege halisi huokoa gharama ya petroli na mafuta. Pia hupunguza msongamano wa ndege angani, kelele na uchafuzi wa hewa, na gharama za kutoa na kuendesha mafunzo. “Kuangusha” chombo hicho hakugharimu chochote na hakuna mtu anayejeruhiwa.

Terry alisema kwamba “Vyombo hivyo vyenye kuiga hali halisi ya usafiri vyaweza kupunguza aksidenti za ndege wakati wa mazoezi. Hutoa mafunzo juu ya kushughulikia hali ya dharura, kama vile injini kushika moto, mtambo wa kutua unapokwama, kupasuka kwa gurudumu, kupunguka kabisa kwa nguvu, hali mbaya ya hewa, ubadilifu wa ghafula wa mwendo wa upepo, barafu, na kutoweza kuona mbali kwa sababu ya ukungu.” Vivyo hivyo, mafunzo mengi juu ya kushughulikia mifumo ya mitambo yaweza kutolewa, na hitilafu na kukwama kwa mitambo zaweza kurekebishwa pasipo mtu kujeruhiwa au kuharibu ndege.

Akitoa maoni yake juu ya jambo hilo, rubani mwenye uzoefu mwingi, J. D. Whitlatch alisema hivi: “Mpangilio wa mambo katika vyombo vya kuiga usafiri hukisia hali na matukio zaidi ya milioni sita. Haiwezekani kamwe kutoa mafunzo mengi jinsi hiyo kwa kutumia ndege halisi.”

Katika Marekani vyombo vya kuiga usafiri hukaguliwa na Shirika la Usimamizi wa Safari za Ndege, marubani wenye kufanyia ndege majaribio, na mafundisanifu. Kila siku kabla ya kuanza mafunzo, mafundisanifu hurekebisha, hukagua na “kuendesha” vyombo hivyo ili kuhakikisha kwamba mashine hizo zitaiga ndege kwa ukaribu iwezekanavyo. Iwapo ndege halisi inafanyiwa mabadiliko fulani, mabadiliko hayo hufanywa katika vyombo hivyo pia. Kila baada ya miezi sita, wawakilishi wa Shirika la Usimamizi wa Safari za Ndege, huendesha vyombo hivyo ili kuhakikisha viko sahihi.

Kujifunza Kutokana na Misiba Iliyopita

Wakitumia habari kutoka kwa vifaa vya kurekodi safari za ndege na vya kurekodi sauti katika chumba cha rubani vya ndege iliyokumbwa na aksidenti, wahandisi wanaweza kutia programu katika chombo cha kuiga hali halisi ya usafiri na kuiga hali na hitilafu zote zilizotukia wakati wa aksidenti fulani hususa. Habari hiyo pamoja na uigaji huo huwawezesha wachunguzi kuamua visababishi vya aksidenti mbalimbali za ndege. Zaidi ya hayo, habari hizo zaweza kutumiwa kufundisha marubani wa wakati ujao namna ya kutenda itokeapo dharura. Habari hiyo pia hutumiwa na watengenezaji wa ndege na vifaa vyake ili kutokeza ndege na vilevile vipuri bora zaidi.

Iwapo uchunguzi unafunua kwamba aksidenti au nusura yake ilitokana na makosa ya rubani, basi mafunzo yanapangwa ili kuepuka hali kama hiyo wakati ujao. Lew Kosich, rubani mwenye ujuzi asema hivi: “Matukio tunayoonyesha si ya kubuniwa bali ni mambo yaliyowahi kutokea.” Katika jitihada ya kuboresha utendaji wa marubani wakati wa dharura, programu za mafunzo na pia usalama wa umma, wataalamu wa usafiri wa ndege daima hukagua na kutokeza hali halisi ili kuona vile rubani angetenda iwapo ajikuta katika hali kama hizo.

Ninapojaribu “kuishusha” ndege aina ya “Boeing 747” katika “Uwanja wa Ndege wa Charles de Gaulle”—chini ya mwelekezo wa rubani msaidizi, Terry—ninatarajia kusikia magurudumu yakigusa ardhi. Lakini lo! Nimekosea jambo fulani na utendaji katika skrini wakwama! Nimegongesha hili “dude kubwa la chuma” kwenye mnara wa kuongozea ndege!

Tuna furaha kama nini kwamba marubani wanaoendesha ndege za kubeba abiria ni wataalamu kwelikweli—kwa kadiri fulani ni kwa sababu ya vyombo vyenye kuiga hali halisi ya usafiri. Utakaposafiri tena kwa ndege, uwe na uhakika kwamba wewe na abiria wenzako mko mikononi mwa rubani hodari.—Imechangwa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Alama g inatumiwa katika kukadiria kiasi cha kani zinazoathiri watu wakiwa ndani ya aina yoyote ya chombo cha usafiri. Nguvu ya uvutano ya dunia hutokeza mchapuko wa wastani wa 1 g. Wakati ambapo rubani anaelekeza ndege juu, yeye huhisi kani ya ziada ikimsukuma kwenye kiti chake. Iwapo kani hiyo ni mara mbili ya nguvu ya uvutano, basi inapewa alama ya 2 g.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kupaa katika chombo cha kuiga usafiri wa ndege kutoka San Francisco

kupaa katika anga la New York City

[Picha katika ukurasa wa 26]

Chombo cha kuiga hali halisi ya usafiri huko Denver, Colorado