Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kudumisha Imani Chini ya Mnyanyaso wa Kimabavu

Kudumisha Imani Chini ya Mnyanyaso wa Kimabavu

Kudumisha Imani Chini ya Mnyanyaso wa Kimabavu

KAMA ILIVYOSIMULIWA NA MICHAEL DASEVICH

“Huko Ujerumani sisi huwapiga risasi Mashahidi wa Yehova. Je, waiona ile bunduki?” ofisa wa Gestapo akasema huku akiashiria bunduki iliyokuwa pembeni. “Naweza kukudunga kwa singe yake bila kuhisi majuto yoyote.”

Nilikuwa na umri wa miaka 15 tu nilipokabili tisho hilo wakati wa kumilikiwa kwa nchi yangu na Wanazi katika mwaka wa 1942.

NILIZALIWA mnamo Novemba 1926 katika kijiji kidogo karibu na Stanislav (sasa inaitwa Ivano-Frankivs’k), iliyokuwa hapo zamani sehemu ya Poland. Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, iliyoanza Septemba 1939 hadi Mei 1945, eneo letu lilimilikiwa kwanza na Muungano wa Sovieti, kisha kwa kipindi fulani na Ujerumani, na hatimaye kurudi mikononi mwa Sovieti. Baada ya vita eneo hilo likaja kuwa sehemu ya Jamhuri ya Ukrainia ya Muungano wa Kisoshalisti wa Sovieti, na hatimaye iliunganishwa na Ukrainia muungano huo ulipovunjika katika mwaka wa 1991.

Baba yangu ambaye ni Mpolandi na mama yangu wa kutoka Belorussia walikuwa wafuasi wa Kanisa Katoliki la Ugiriki. Lakini, katika mwaka wa 1939, wanawake wawili kutoka kutaniko la Mashahidi wa Yehova lenye washiriki 30 katika kijiji jirani cha Horyhliady walituachia kijitabu Universal War Near. Kijitabu hicho kilisimulia matukio niliyokuwa nikiona yakitendeka. Kwa hiyo, nilipoona swali hili katika kijitabu hicho, “Kwa nini mataifa yanafanya haraka kwenda vitani?” nilitia maanani maelezo ya Kibiblia yaliyokuwa yameonyeshwa humo.

Vita haikuwa tatizo pekee tulilokuwa nalo katika Ukrainia. Njaa kali ilikuwepo. Sera za Joseph Stalin, Waziri Mkuu wa Sovieti zilisababisha watu wengi kuhamishwa kinguvu na kupelekwa Urusi. Kuteseka nilikoshuhudia kulinifanya nichunguze Biblia kwa makini. Nilimwomba Shahidi mmoja kutoka Horyhliady anifunze Biblia.

Kijiji chetu cha Odajiv kinaelekeana na Horyhliady ng’ambo ya Mto Dniester, na mara kadhaa katika juma, nilivuka mto huo kwa mashua ndogo ili kuhudhuria funzo langu la Biblia. Mnamo Agosti 1941, mimi na dada yangu Anna tulibatizwa kwenye mto huo tukiwa pamoja na watu wengine wawili.

Kuhojiwa na Gestapo

Wajerumani walianza kumiliki mwaka wa 1941, na licha ya tisho la kuadhibiwa, tuliendelea na utendaji wetu wa Kikristo. Nilianza kupainia mwaka uliofuata kwa kutumia baiskeli. Muda si muda nilikutana na Gestapo Wajerumani kama inavyoelezwa kwenye utangulizi. Mambo yalitendeka hivi.

Siku moja nilipokuwa nikirejea nyumbani kutoka katika huduma, niliwatembelea Wakristo wenzangu wawili, mama na binti yake. Mume wa binti huyo alipinga imani yetu na alikuwa na hamu ya kutaka kujua mke wake alipokea vichapo vya Biblia kutoka wapi. Siku hiyo nilikuwa nimebeba si vichapo tu bali pia ripoti ya utumishi ya Wakristo wenzangu. Huyo mume aliniona nilipokuwa nikiondoka kutoka nyumba ile.

“Simama!” akasema kwa hasira. Niliunyakua mfuko wangu na kukimbia.

“Simama! Mwizi!” akapaaza sauti. Watu waliokuwa wakifanya kazi kwenye mashamba walifikiri lazima iwe nilikuwa nimeiba kitu fulani, hivyo wakanishurutisha kusimama. Mwanamume huyo alinipeleka hadi kituo cha polisi ambapo tulimkuta ofisa wa Gestapo.

Yule ofisa kuona tu vile vichapo vilivyokuwa ndani ya mfuko wangu, alifoka kwa Kijerumani na kusema: “Rutherford! Rutherford!” Sikuhitaji mfasiri anieleze sababu ya hasira yake. Jina la Joseph F. Rutherford, aliyekuwa hapo awali msimamizi wa Watch Tower Bible and Tract Society, lilikuwa kwenye ukurasa wa pili wa vichapo vilivyochapishwa na Mashahidi wa Yehova. Kisha yule mwanamume alitoa shtaka la kuwa mimi nilikuwa mpenzi wa mke wake. Polisi na yule ofisa wa Gestapo waliona shtaka hilo kuwa la upuuzi kwa sababu mke wake alikuwa na umri wa kutosha kuwa mama yangu. Kisha wakaanza kunihoji.

Walitaka kujua mimi nilikuwa nani, ninaishi wapi, na hasa nilitoa wapi vichapo hivyo. Lakini nilikataa kuwaambia. Walinipiga mara kadhaa na kunidhihaki, halafu wakanifungia ndani ya chumba kilicho chini ya ardhi. Nilihojiwa kwa siku tatu zilizofuata. Halafu nikapelekwa katika ofisi ya yule ofisa wa Gestapo aliyetisha kunidunga kwa singe. Sikujua kama angefanya alivyotishia. Niliinamisha kichwa changu na kukawa kimya. Kisha akasema ghafula: “Waweza kwenda.”

Kama unavyoweza kung’amua, ilikuwa vigumu sana kuhubiri na pia kufanya mikutano yetu siku hizo. Tuliadhimisha Ukumbusho wa kila mwaka wa kifo cha Kristo katika Aprili 19, 1943, katika vyumba viwili vya nyumba moja huko Horyhliady. (Luka 22:19) Kabla tu ya kuanza mkutano wetu, tulisikia onyo kwamba polisi walikuwa wakija kwenye nyumba hiyo. Baadhi yetu tulijificha kwenye bustani, lakini dada yangu Anna na wanawake wengine watatu waliteremka kwenye chumba kilichokuwa chini ya ardhi. Polisi waliwapata huko na kuburuta mmoja baada ya mwingine kutoka huko ili kuwahoji. Waliteswa kwa masaa mengi, na mmoja wao alijeruhiwa vibaya.

Matukio ya Ulimwengu Yabadilika

Katika kiangazi cha 1944, Wajerumani waliondoka na Wasovieti wakamiliki tena eneo letu. Tukiwa watumishi wa Yehova, tulishikilia kanuni za Biblia zilezile tulizokuwa tumeshikilia tulipokuwa chini ya utawala wa Nazi. Tulikataa katakata kujiunga na harakati zozote ama za kijeshi au za kisiasa. Uaminifu-mshikamanifu wetu kwa kanuni hizo za Biblia ulijaribiwa punde tu baada ya hapo.—Isaya 2:4; Mathayo 26:52; Yohana 17:14.

Siku chache baadaye, Wasovieti walianza kuwakusanya vijana wote wanaume kwa utumishi wa kijeshi. Mambo yakawa magumu zaidi kwa kuwa si Wasovieti peke yao waliokuwa wakihitaji wanajeshi wapya. Wazalendo wapiganaji wa Ukrainia walikuwa wakiwasaka wavulana katika eneo lote, kisha kuwapeleka msituni ili kuwazoeza kupigana. Sisi Mashahidi tulijikuta katika hali ngumu ya kusadikisha vikundi viwili vyenye kuzozana juu ya kutokuwemo kwetu—Wasovieti na wazalendo wa Ukrainia.

Vikundi hivyo viwili vilipigana katika kijiji chetu, na wazalendo wawili wakauawa nje ya nyumba yetu. Maofisa wa Kisovieti walifika kwetu wakitaka kujua kama tuliwajua watu hao waliouawa. Maofisa hao waliokuja kwetu waliamua kunichukua ili nijiunge na jeshi lao, ambalo lilikuwa likiunda kikosi cha wanajeshi wa Poland. Walitaka kuniandikisha kikosini kwa sababu nilikuwa wa asili ya Poland.

Mimi, pamoja na Mashahidi wengine wanne tulikataa kuandikishwa katika jeshi, kwa hiyo tulisafirishwa kwa garimoshi hadi Dnipropetrovs’k, mji uliokuwa kilometa 700 hivi upande wa mashariki. Tulipofika huko na baada ya kueleza kwamba sisi hatuwezi kutumikia katika jeshi kwa sababu ya imani yetu ya Biblia, tuliwekwa kizuizini na kusubiri mashtaka yatayarishwe. Tulipofikishwa mahakamani, tuligundua kuwa mchunguzi wa kesi yetu alikuwa Myahudi. Katika kujitetea, tulieleza juu ya itikadi zetu huku yule mchunguzi akisikiliza kwa makini. Tuligusia mambo tuliyojua yangempendeza, kutia ndani kunyanyaswa kwa Waisraeli na kukombolewa kwao kutoka Misri kupitia Musa.

Miezi tuliyokuwa tukisubiri mahakama itoe hukumu, tuliwekwa katika seli pamoja na wafungwa wengine 25. Walipofahamu kuwa tulikuwa tumekataa kujiunga na jeshi walipaaza sauti na kusema: “Ninyi ni ndugu zetu!” Punde si punde, tulifahamu kuwa hawakuwa mashahidi bali Wabaptisti. Walikuwa tayari kujiunga na jeshi lakini walikamatwa walipokataa kubeba silaha.

Mnamo Mei 1945, tukiwa bado kizuizini huko Dnipropetrovs’k, tuliamshwa usiku wa manane na milio ya risasi na makelele kutoka kambi ya wanajeshi na kutoka huko nje barabarani. Tulishindwa kutambua kama ilisababishwa na ghasia, mapigano, au hata nderemo. Tulipata kujua sababu ya kelele hizo kutoka kwa kinyozi siku iliyofuata tulipokuwa tukipata kiamsha-kinywa: Vita ilikuwa imekwisha! Punde baada ya hapo mahakama ilitangaza hukumu ya kesi yetu. Sisi pamoja na Wabaptisti tulipewa hukumu ileile—miaka kumi katika kambi za jela.

Kambi ya Jela Huko Urusi

Mashahidi watano tuliokuwapo tulipelekwa kwenye kambi ya jela huko Urusi. Baada ya safari ya majuma mawili kwa garimoshi, hatimaye tulifika Sukhobezvodnoje, kilometa 400 hivi mashariki ya Moscow. Kituo cha Sukhobezvodnoje kilikuwa makao makuu ya usimamizi wa kambi 32 za kazi ngumu zilizokuwa kando-kando ya reli. Kila kambi ilikuwa na maelfu ya wafungwa. Baada ya miezi sita huko Sukhobezvodnoje, nilipelekwa katika Kambi Namba 18. Wengi wa wafungwa waliokuwa katika kambi hiyo walikuwa ama wahalifu au wafungwa wa kisiasa.

Wenye mamlaka walitupa kazi ngumu sana ya kukata miti. Nyakati nyingine ilitubidi kutembea ndani ya theluji iliyotufika kiunoni, halafu kukata miti kwa msumeno na kisha kuiburuta katika theluji hiyo. Mara moja kila juma, siku ya Jumapili baada ya kiamsha-kinywa, niliweza kushiriki angalau jambo fulani kutoka kwa Biblia pamoja na Mashahidi wengine wanne waliokuwa humo kambini. Hiyo ndiyo iliyokuwa mikutano yetu. Hata tuliadhimisha Ukumbusho wa Kifo cha Yesu ndani ya bafu la kuogea mwaka fulani. Wakati huo tulitumia maji ya forosadi kuwa mfano wa damu ya Yesu kwa sababu hatukuwa na divai.

Nililemewa sana na hisia za upweke. Nikamweleza Yehova yaliyokuwa moyoni mwangu, naye akanitia nguvu kama alivyokuwa amemtia nguvu Eliya wakati nabii huyo alipokuwa akisumbuliwa na hisia kama hizo. (1 Wafalme 19:14, 18) Mungu alinisaidia kutambua kwamba sikuwa peke yangu. Kwa kweli alikuwa nguzo imara katika maisha yangu, hata katika hali hizo ngumu.

Kulikuwa na Mashahidi wachache katika kambi nyinginezo zilizokuwa karibu na Sukhobezvodnoje, na tuliweza kuwasiliana nao mara kwa mara kupitia Shahidi mmoja ambaye kazi yake ilimruhusu kuzuru kambi zote. Kwa njia ya siri alipeleka vichapo kutoka kambi moja hadi nyingine. Kupitia mpango huo tuliweza kushiriki pamoja vichapo vichache tulivyokuwa navyo. Hilo lilithibitika kuwa kitia-moyo kama nini!

Kurudi Ukrainia

Kutokana na msamaha uliotangazwa na Serikali, kifungo changu kilipunguzwa kutoka miaka kumi hadi miaka mitano. Kwa hiyo, mnamo Aprili 1950, niliungana tena na kutaniko langu la nyumbani katika Horyhliady. Hata hivyo, bado kazi yetu ilikuwa imepigwa marufuku huko Ukrainia, na kushiriki katika huduma kulikuwa na hatari kubwa. Lakini thawabu ilikuwa kubwa pia.

Punde tu baada ya kurudi, nilizungumza na mtu aitwaye Kozak, aliyekuwa akiishi katika kijiji cha Zhabokruky kilichoko kilometa 20 kutoka kwetu. Nilimuuliza kuhusu hali ya maisha yake na ya familia yake. Nilifahamu kwamba wafanyakazi wa mashamba ya umma walikuwa na shida za fedha na hivyo nilijua kuwa swali hilo lilifaa katika kuanzisha mazungumzo. Nilimweleza kuwa Biblia ilitabiri kuwepo kwa njaa na vita katika siku zetu. (Mathayo 24:3-14) Alikuwa na hamu ya kujua zaidi. Kwa hiyo nikamtembelea tena. Kila juma nilitembea umbali wa kilometa 40 hivi ili nijifunze Biblia na familia ya Kozak. Hatari za kufanya hivyo, na kiasi kikubwa cha wakati nilichokuwa nimetumia vyote vilisahaulika washiriki wa familia ya Kozak walipobatizwa mnamo Agosti 1950.

Punde tu baada ya kubatizwa, washiriki wa familia hiyo ya Kozak walipelekwa uhamishoni pamoja na maelfu ya Mashahidi wengine. Wote walikamatwa kwa ghafula na askari wenye silaha mapema mwezi wa Aprili 1951 na—bila kupelekwa mahakamani au kusikizwa—walihamishwa hadi Siberia. Huko familia ya Kozak pamoja na marafiki wangu wengine walilazimishwa kujenga makao mapya. *

Kati ya familia 15 zilizokuwa katika kijiji cha Horyhliady ni 4 tu zilizopelekwa uhamishoni. Hata hivyo, katika makutaniko mengine idadi ya Mashahidi waliohamishwa ilikuwa kubwa zaidi. Uhamisho huo mkubwa ulipangwaje? Wenye mamlaka walikuwa na orodha ya majina ya Mashahidi na hivyo ikawa rahisi kukamata wengi wao wakati wowote ule. Inaonekana orodha hiyo ilikuwa imetayarishwa katika mwaka wa 1950, nikiwa ningali gerezani huko Urusi, na kwa hiyo jina langu halikupatikana humo. Mwezi mmoja mapema, mnamo Machi 1951, nilikuwa nimefunga ndoa na Fenia, mtumishi mwaminifu-mshikamanifu wa Yehova. Washiriki wote wa familia ya Fenia walikuwa wamepelekwa uhamishoni, lakini yeye aliponyoka kwa sababu aliitwa kwa jina langu baada ya ndoa, na jina hilo halikuwa kwenye orodha hiyo.

Majaribu Magumu ya Imani

Baada ya Mashahidi hao kuhamishwa, sisi tuliobaki tulihitaji kupanga upya kazi yetu. Niliombwa kusimamia kazi katika makutaniko ya eneo la karibu la Ivano-Frankivs’k, ambako hata baada ya Mashahidi kuhamishwa bado kulikuwa na Mashahidi 30 hivi katika kila moja ya makutaniko 15 yaliyokuwapo. Nikiwa seremala mwenye kujiajiri, nilikuwa na ratiba yenye kubadilikana, hivyo nilikutana kwa siri na akina ndugu kutoka kila kutaniko mara moja kwa mwezi.

Mara nyingi tulifanya mikutano yetu usiku makaburini, mahali tulipokuwa na uhakika wa kuwa peke yetu. Jambo kuu katika mazungumzo lilikuwa kuhakikisha kwamba angalau kila kutaniko lina vichapo kadhaa vya Biblia. Nyakati nyingine tuliweza kupokea gazeti la karibuni la Mnara wa Mlinzi katika Kipolandi au Kirumania na kulitafsiri katika Kiukrainia. Hata hivyo, wenye mamlaka walituandama sana, wakijaribu kuzitafuta na kuziharibu mashine zetu kuukuu za kunakili.

Lakini tatizo letu kubwa lilikuwa ukosefu wa mawasiliano pamoja na ndugu zetu Wakristo katika nchi nyingine, kutia ndani wale walio Brooklyn, New York, ambao walikuwa wakisimamia utendaji wetu wa Kikristo. Tokeo likawa kwamba makutaniko yetu mara nyingi yalitatizwa na mafarakano, porojo, na watu kuchimbana. Baadhi ya Mashahidi walijitenga na tengenezo na kuanzisha makundi ya wapinzani. Hata hadithi zisizofaa na za uwongo kuhusu ndugu waliosimamia utendaji huko Brooklyn zilienezwa.

Hivyo, wengi wetu tuligundua kwamba majaribu magumu zaidi ya imani hayakuwa yakitokana na mnyanyaso wa wapinzani bali yalitokana na mizozano kutanikoni. Ingawa baadhi yao waliacha kuabudu nasi, tulifahamu kwamba lilikuwa jambo muhimu kushikamana na tengenezo na kumsubiri Yehova anyooshe mambo. Inapendeza kwamba wengi wa Mashahidi katika eneo letu walibaki waaminifu. Nafurahi kwamba wengi wa wale walioacha tengenezo walighairi na kuanza tena kumtumikia Yehova pamoja nasi.

Hata kwenye kipindi hicho kigumu tulipokuwa bila mawasiliano, bado tulikuwa wenye shughuli nyingi katika huduma ya peupe na tulibarikiwa sana. Tumepata thawabu iliyoje! Kila ninapohudhuria Funzo letu la Kitabu, mimi hukumbuka baraka za Yehova. Kila mmoja wa hao watu 20 au zaidi wanaohudhuria funzo hilo amejifunza kweli kupitia kwa mshiriki wa familia yangu.

Wazazi wangu na dada yangu Anna tayari wamekufa, lakini walidumu wakiwa waaminifu kwa Yehova. Mimi na Fenia bado tunamtumikia Yehova kadiri tuwezavyo. Muda umepita upesi. Katika miaka 30 iliyopita, mambo mengi yenye kusisimua yametokea kwa Mashahidi wa Yehova katika Ukrainia ambayo hayawezi yote kusimuliwa katika habari fupi kama hii. Lakini nimeridhika tu kuangalia nyuma kwenye miaka yangu mingi niliyomtumikia Yehova, nikiwa na uhakika kwamba yeye atadumu akiwa nguzo imara na tegemezo langu, maana yeye mwenyewe asema: “Mimi, BWANA, sina kigeugeu.”—Malaki 3:6.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 32 Ona makala “Zaidi ya Miaka 40 Chini ya Marufuku ya Ukomunisti,” katika toleo la Mnara wa Mlinzi la Machi 1, 1999, ukurasa wa 24-29, na “Twapelekwa Uhamishoni Siberia!,” katika toleo la Amkeni!, la Aprili 22, 1999, ukurasa wa 20-25.

[Blabu katika ukurasa wa 21]

Walitaka kujua mimi nilikuwa nani, ninaishi wapi, na hasa nilitoa wapi vichapo hivyo. Lakini nilikataa kuwaambia

[Blabu katika ukurasa wa 22]

Nililemewa sana na hisia za upweke. Nikamweleza Yehova yaliyokuwa moyoni mwangu, naye akanitia nguvu

[Picha katika ukurasa wa 20]

Mimi na Fenia mwaka wa 1952

[Picha katika ukurasa wa 23]

Nikiwa pamoja na Fenia leo