Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Volkeno Yenye Nguvu Sana Yawa Kisiwa Kitulivu

Volkeno Yenye Nguvu Sana Yawa Kisiwa Kitulivu

Volkeno Yenye Nguvu Sana Yawa Kisiwa Kitulivu

MASHUA yetu ipigapo kona ya mwisho kuelekea bandari ya kisiwa cha Ugiriki cha Santorini, twaona mandhari yenye kupendeza sana. Kuta ndefu za miamba yenye kutisha iliyo na urefu wa meta 300 hivi zinachomoza baharini. Kuna nyumba nyeupe pepepe kwenye majabali. Umbo la kipekee la kisiwa hicho, kutokuwepo kwa fuo zozote za kisiwani, miamba inayoning’inia—mambo hayo yanadokeza kwamba kitu fulani kisicho cha kawaida kilitukia hapa. Kilitukia. Kisiwa cha Santorini ni mabaki ya nusu ya upande wa mashariki wa volkeno iliyolipuka, nasi twaabiri kwenye maji yaliyojaa kwenye shimo lililo katikati yake!

Kutokeza Kisiwa

Katika nyakati za kale kisiwa cha Santorini—ambacho leo pia kinaitwa Santorin au Thíra—kiliitwa Strongyle, yaani “Mviringo.” Na kwa kweli kisiwa hicho kilikuwa cha mviringo. Lakini kulingana na wataalamu, mlipuko mkubwa sana wa volkeno ulibadili umbo la kisiwa hicho yapata miaka 3,500 iliyopita. Huenda mlipuko mkubwa ulipasua shimo kubwa katikati ya kisiwa, na kufanyiza bonde kubwa ambalo lilijaa maji ya bahari mara moja.

Wataalamu fulani wa volkeno wanakisia kwamba mngurumo wa mlipuko huo ulisikika Ulaya, Asia, na Afrika na kwamba uliangusha majengo yaliyokuwa umbali wa kilometa 150. Wanadai kwamba jivu lenye kusonga liliziba nuru ya jua kwenye bonde lote la Mediterania kwa siku kadhaa. Kwa ujumla, eneo la kilometa 80 za mraba la kisiwa hicho lilipotelea angani au kutumbukia baharini. Viumbe vyote vilikufa.

Baada ya muda, ardhi iliyobaki ya Strongyle ikaja kuwa makao ya masetla wa bara, na kisiwa hicho kikapewa jina jipya Calliste, linalomaanisha “Maridadi Zaidi.” Lakini masetla walioishi kwenye volkeno waliishi kwa wasiwasi tu. Kati ya mwaka 198 K.W.K. na 1950 W.K., kulitokea milipuko 14. Kisha, mwaka 1956 tetemeko la dunia liliharibu nyumba nyingi za kisiwa hicho. “Ardhi ilikuwa ikitikisika na kutetemeka kama jeli,” asema Kyra Eleni, mwanamke mzee-mzee aliyeishi wakati wa msiba huo. “Mbele ya ua wa nyumba yangu, iliyokuwa juu ya mwamba, kulikuwa na njia ya changarawe ya miguu. Kwa ghafula njia hiyo iliporomoka baharini na kuacha nyumba yangu ikining’inia hewani! Tulilazimika kuhama nyumba hiyo na kujenga nyingine mpya kwenye ardhi iliyo thabiti.”

Vijiji vilivyoharibiwa vilijengwa upya tena haraka, hasa na wageni. Leo maelfu ya wageni hufurika Santorini kila majira ya kiangazi. Mbali na Santorini, bado kuna kisiwa kidogo zaidi cha Thirasía na kisiwa kisicho na watu cha Aspronísi.

Kwa kuongezea, katikati ya shimo kubwa la Santorini kuna visiwa vidogo viwili vya volkeno—Néa Kaméni na Palaía Kaméni. Bado waweza kuona utendaji wa volkeno kwenye visiwa hivi vidogo vilivyofanyizwa hivi karibuni kwa kuwa ‘jitu lililolala’ huamka pindi kwa pindi na kufuka mawingu ya moshi kwa nguvu. Umbo la ujumla la Santorini linabadilika daima, hivi kwamba lazima ramani yake ichorwe upya pindi kwa pindi.

Kuishi Ukingoni

Kwenye ukingo wa shimo kubwa la Santorini, hakuna miteremko, ni miamba pekee. Ardhi kubwa iliyo wima hufanya iwe rahisi kwa wakazi hao kujenga nyumba: Chimba mtaro wa mlalo ardhini, jenga ukuta kwenye mwingilio, na uhamie ndani. Naam, nyumba nyingi zilizo katika shimo hilo kubwa zimechongwa kutoka kwenye miamba.

Mbele ya kila nyumba kuna ua, au roshani, inayoelekeana na shimo kubwa lililo katikati ya kisiwa hicho. Ua wa nyumba iliyo juu hutumika kama dari ya nyumba iliyo chini yake. Ukiwa kwenye roshani hizo unaweza kufurahia kutazama machweo ya jua yenye kuvutia, kufurahia jua la zambarau linapotua kwenye bahari polepole na kwa fahari. Nyua nyingine pia zina jiko ndogo, kibanda kimoja au viwili vya kuku, na mimea na maua yenye harufu nzuri yaliyopandwa kwenye vyungu.

Jambo la pekee kuhusu vijiji hivi ni kwamba nyumba hizo hazijajengwa katika mstari ulionyooka. Hata ghala za chini hazilingani. Mistari na mipindo hii mingi isiyofuata utaratibu fulani, na ambayo hukutana na kufanyiza maumbo yasiyo ya kawaida, hufanya majengo hayo yaonekane kuwa mahali patulivu, jambo linaloshangaza hasa kwenye kisiwa kilicho na mawe-mawe yenye ncha zilizochongoka.

Kisiwa cha Santorini ni kikavu sana. Maji pekee yanayopatikana hapa ni maji ya mvua yaliyokusanywa na kuhifadhiwa katika matangi. Lakini udongo wa juu una rutuba. Hivyo, bara dogo la kisiwa hicho hutokeza mazao mbalimbali.

Kisiwa cha Santorini humkumbusha mtalii na mwenyeji umaridadi wa sayari yetu kwa njia ya pekee na ya fahari.

[Sanduku katika ukurasa wa 18]

MAMBO YANAYOHUSU ATLANTIS

Ngano ambayo huenda ilianzia Misri, ikatajwa katika fasihi za Kigiriki, na kuandikwa tena na wanajiografia Waarabu katika enzi za kati inahusu bara, kisiwa, au jiji lililopotea la Atlantis. Inadhaniwa kwamba Atlantis lilipotelea baharini baada ya matetemeko ya dunia na mafuriko. Waakiolojia fulani wanadokeza kwamba ngano hiyo ilianza wakati wa mlipuko wa volkeno wa Santorini.

Uchimbuaji ulioanza hapa mwaka 1966/1967 ulifunua kwamba jiji la kifalme lenye utajiri la Minoa lililofukiwa ndani ya vifusi vya volkeno, lilihifadhiwa kama lilivyokuwa wakati wa mlipuko. Yaonekana kwamba maonyo yaliyotolewa mapema yalichochea wakazi waondoke kutoka eneo hilo kwa wakati unaofaa. Watafiti fulani wanakisia kwamba kukataa kwa wakazi hao kukiri kwamba jiji lao lililokuwa maridadi lilikuwa limetoweka kulianzisha ngano ya kwamba Atlantis liliokoka na linasitawi, na maisha ya jijini yanaendelea chini ya bahari.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Santorini

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mashahidi wa Yehova hufurahi kuhubiri katika Santorini

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kutazama Aegea kutoka kwenye ngazi za Santorini