Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mkataji-Miti wa Awali Angali Anafanya Kazi

Mkataji-Miti wa Awali Angali Anafanya Kazi

Mkataji-Miti wa Awali Angali Anafanya Kazi

WANADAMU wamebuni vyombo vya aina nyingi vya kukata miti, kutia ndani mashoka, kabari, chembeo, na misumeno. Vilevile kuna tingatinga kubwa sana zenye visu vikali vyenye uwezo wa kukata mashina ya miti minene. Lakini vyombo vya kukata miti vya zamani zaidi havikubuniwa na mwanadamu. Vyombo hivyo ni meno yenye ncha kali—ya buku, yule mkataji-miti wa awali.

Buku aliyekomaa aweza kuwa na urefu wa meta moja na nusu kutoka katika pua hadi mkiani na uzito wa kilogramu 27. Kwa sababu meno yake ya mbele huendelea kukua daima, buku hulazimika kuyakwaruza kwa ukawaida. Gamba gumu huwa kwenye sehemu ya juu ya meno ya mbele, ikiyafanya kuwa yenye ncha kali. Yakiwa yamepindika kuelekea upande wa ndani wa kinywa chenye taya zenye misuli yenye nguvu nyingi, patasi hizi za asili zaweza kuukata mti mgumu sana kwa urahisi.

Manyoya Yenye Joto, Mkia Wenye Matumizi Mbalimbali

Watu wanaoishi sehemu zenye baridi wanathamini koti lenye joto, lisilopenya maji. Kwa hakika, buku hana uhitaji kamwe wa kununua koti la aina hiyo, kwa kuwa mwili wake umevikwa vazi nene la manyoya. Manyoya ya buku yamepangwa katika safu mbili na rangi yake huwa kati ya hudhurungi na kahawia iliyoiva. Manyoya ya ndani, yana nywele nyingi laini zenye vishore vidogo vinavyoshikamana kumlinda buku dhidi ya maji na baridi. Manyoya mengine marefu na manene hulinda manyoya hayo ya ndani na kumsaidia buku kupukusa maji. Ukijumlisha hayo pamoja na mng’ao na ulaini wake, si ajabu kwamba watu wengi huyaona mavazi yenye kutengenezwa kwa ngozi ya buku kuwa yenye fahari! Pindi fulani katika Kanada, ngozi za mabuku hata zilitumika kama pesa!

Buku wa aina zote wana jozi mbili za matezi zisizo za kawaida chini ya mkia. Jozi moja hutoa mafuta ya aina ya pekee, na ile nyingine hutoa castoreum, umajimaji wenye manukato yenye harufu kali lakini isiyo ya kuchukiza. Buku hutumia umajimaji huu kwa njia mbalimbali, kutia ndani kuyafanya manyoya yake yawe yasiyoweza kupenya maji na kuwavutia buku wenzake. Umajimaji huo wa Castoreum ni wenye mafaa kwa binadamu pia, kwa kuwa hutiwa kwenye baadhi ya marashi na watengenezaji wa manukato.

Mkia wa buku ni wa kipekee. Ni wenye umbo la kafi na wenye urefu wa sentimeta 30, nao hutumika kwa mambo mbalimbali. Kwa mfano, ndani ya maji, mkia wa buku hutumika kama usukani wa uongozaji. Kwenye nchi kavu mkia huo hutumika kama nguzo wakati buku anapoiguguna miti. Hatari ikiwepo buku hupiga uso wa maji kwa mkia wake ili kuwaonya wenzake wajifiche mahali salama. Ingawa hivyo, tuondoe dhana moja isiyo ya kweli, buku hatumii mkia wake kama mwiko wa mwashi kuweka udongo kwenye bwawa analojenga.

Chakula na Maji

Buku hula nini? Sehemu nyororo ya maganda ya ndani na chipukizi za mipopla na miti aina ya willow ndicho chakula anachopenda sana. Kwa hiyo, buku akiwa kwenye kukata mti kwa madhumuni ya ujenzi aweza kufurahia mlo pia. Nyakati fulani huku buku mmoja akiwa anabambua shina la mti, buku mwingine hunyemelea na kuiba ganda tamu upande ule mwingine bila kuonekana.

Wakati wa majira ya baridi kali buku hutumia njia ya kipekee kuhifadhi chakula. Kwanza, huchimba shimo refu chini ya maji—jambo ambalo si tatizo kwa sababu buku anaweza kukaa chini ya maji kwa dakika 15. Halafu, buku huweka rundo la matawi ya mipopla, willow, na miti mingineyo juu ya maji kwenye sehemu iliyoko shimo hilo. Miti hiyo inapozidi kuwa mingi huzama na kufikia shimo lile. Baadaye, maji yakiwa yameganda na kuwa barafu na theluji kuzuia utendaji juu ya nchi, jamii ya mabuku huwa na “ghala” la chini ya maji lililojaa chakula cha kutosha.

Ni wanyama wachache sana wa nchi kavu ambao wamezoea kukaa majini kama vile buku. Zaidi ya manyoya yenye kusongamana na ambayo yamefanywa kuwa yasiyopenya maji kwa mafuta, buku anayo mafuta ya mwili ambayo humkinga na baridi kali anapokuwa ndani ya maji baridi sana. Naam, buku hata hujamiiana wakiwa chini ya maji! Kwa kuwa maji ni muhimu sana katika maisha ya buku, wao huyafanya makao yao kando ya maziwa na mito.

Mabuku na Wanadamu

Mabuku ni waelekevu, na huwa tayari kufanya urafiki na wanadamu wanaowatendea kwa fadhili. Wanyama hawa huyasafisha manyoya yao kwa ukawaida na kubaki wakiwa safi. Katika nyakati za kale, ilikuwa kawaida kwa wenyeji wa Marekani kuishi na mabuku kwenye kambi zao wakiwa wanyama kipenzi. Hata hivyo, usifanye haraka kumwalika buku nyumbani mwako. Tatizo ni kwamba hawakomi kujenga. “Wanapowekwa ndani ya nyumba,” mtaalamu wa mazingira Alice Outwater aandika, “watakatakata miguu ya meza na viti na kuitumia kujenga mabwawa madogo katikati ya fanicha.” Wao huharibu pia miti na nguzo za ua.

Lakini tatizo kubwa hata zaidi limezuka kati ya mabuku na wanadamu. Kwa mfano, baadhi ya wenye mashamba hulalamika kwamba mabwawa hufanya maji ya mito kufurika na kuharibu mali. Hata hivyo, wanasayansi na watu wengine wamekanusha malalamiko hayo kwa kuonyesha faida zinazotokana na utendaji wa mabuku. Kwa mfano, mabwawa yanayofanyizwa na mabuku huhifadhi na kuchuja maji na kufanyiza hali zinazofaa kuendeleza uhai wa aina nyingi. Baadhi ya watu hata husema kwamba mabwawa ya mabuku hupunguza athari za ukame.

Wataalamu wa viumbe hukadiria kwamba sasa kunao mabuku wapatao milioni 10 katika bara lote la Marekani. Hata hivyo, baadhi yao hukadiria kuwa zaidi ya mabuku milioni 200 waliishi kwenye eneo hilo miaka 500 iliyopita. Ebu wazia: Makumi ya mamilioni ya “wakataji-miti” huenda walikuwa wakifanya kazi kwenye misitu ya Amerika Kaskazini kabla ya kufika kwa Wazungu wa kwanza. Ingawa hivyo, badala ya masetla hao wa mapema kupata ardhi tupu isiyo na miti, walikuta misitu mikubwa yenye kusitawi. Kwa wazi buku ni muhimu katika ikolojia ya sayari yetu. Hivyo, twapaswa kushukuru kwa vile mkataji-miti wa awali angali anafanya kazi!

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 22, 23]

“Mwenye Shughuli Nyingi Kama Buku”

Yule mtu aliyetunga maneno hayo yaelekea alikuwa amewatazama mabuku wakiwa katika shughuli za kufanyiza bwawa penye mto au wakijenga makao yao. Kwa kweli, wanyama hao huonekana wasiochoka wanapokata miti na kusafirisha vipande kwenye sehemu ya ujenzi. Nyakati nyingine, hata huwa wanachimba mitaro ili vifaa vya ujenzi viweze kuelea hadi vinapohitajika.

Mabuku hujengaje bwawa zao? Kwanza, wao hupanga matawi chini ya mto ili kuufanya mjengo kuwa imara. Iwapo mto ni mpana, mabuku hupinda mjengo ukate maji ili kuuimarisha dhidi ya mkondo. Wao huongezea miti na kujaza upana wote hadi ufikie kimo kinachofaa, halafu huziba matundu kwa matope na mawe. Ili kulifanya bwawa liwe imara, mabuku huegemeza matawi upande wa kufuata mkondo wa maji yakiwa yamekitwa kwenye sehemu ya chini ya mto. Viumbe hawa wenye bidii ya kazi hata hufanyia ujenzi wao marekebisho kwa ukawaida!

Baada ya muda usio mrefu bwawa tulivu hufanyiza upande wa juu wa mto. Hapa ndipo mabuku hujenga makao yao yenye usalama—hayo huanza kama shimo chini ya mto wakati bwawa linapojengwa na baadaye nyumba mfano wa kuba hujengwa kwa matope na vijiti kando ya bwawa. Ili kujilinda dhidi ya wanyama wawindaji, mabuku hutumia miingilio iliyoko chini ya maji. Wakiwa kwenye sehemu hiyo salama, wao hupumzika na kuwalea wachanga wao.

Buku ni mwenye bidii ya kazi kwelikweli. Wanasayansi katika Wyoming, huko Marekani, waliwaachilia mabuku kumi—watano wa kike na watano wa kiume—kwenye eneo ambalo mabuku hawakuwa wameonekana kwa muda mrefu. Mwaka mmoja baadaye, watafiti hao walirudi na kuwapata mabuku hao wakiwa wameanzisha jamii tano tofauti na kujenga mabwawa 55!

[Picha katika ukurasa wa 24]

Buku kazini; makao ya buku na bwawa; kitoto cha buku