Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hatari za Kuomba Lifti

Hatari za Kuomba Lifti

Hatari za Kuomba Lifti

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

Katika siku moja ya kiangazi chenye joto mwaka wa 1990, raia mmoja wa Uingereza mwenye umri wa miaka 24 Paul Onions, aliyekuwa amebeba mfuko mgongoni, alikuwa akiomba lifti katika Barabara Kuu ya Hume, kusini ya Sydney, Australia. Paul alishukuru wakati mtu asiyemjua aliposimama na kumpa lifti. Hakujua kabisa kwamba angeponea chupuchupu kwa kuikubali. *

PASIPO kutambua hatari, Paul aliketi kwenye kiti cha mbele cha gari hilo na kupiga gumzo na dereva. Baada ya dakika chache dereva huyo aliyeonekana kuwa mkarimu akawa mchokozi tena mbishani. Kisha kwa ghafula dereva akaelekeza gari kando ya barabara, huku akisema kwamba alitaka kuchukua kanda fulani za muziki chini ya kiti. Akatoa bunduki badala ya kanda—na kuielekeza kifuani mwa Paul.

Paul alipuuza amri ya dereva ya kuendelea kuketi, akafungua upesi mkanda wa usalama, na kuruka nje ya gari, huku akikimbia kwa nguvu zake zote kwenye barabara kuu. Dereva alimkimbiza kwa miguu, akionekana waziwazi na wasafiri wengine wa magari. Hatimaye alimpita, akambamba kwenye T-shati, na kumwangusha chini. Alipojinasua, Paul alikimbia mbele ya gari lililokuwa likija, huku akimlazimisha dereva huyo aliyekuwa ameshtuka, mama na watoto wake, kusimama. Baada ya Paul kumsihi, mama huyo alimruhusu kuingia, akageuza gari katikati ya barabara na kutoroka mbiombio. Baadaye mshambuliaji wa Paul alitambulishwa kuwa muuaji sugu aliyekuwa ameua watu saba wenye kubeba mifuko mgongoni, ambao baadhi yao walikuwa wakiomba lifti wakiwa wawili-wawili.

Kwa nini muuaji huyo alivutiwa na watu hao? Wakati wa kusikizwa kwa kesi ya muuaji huyo, hakimu alisema: “Wahasiriwa wote walikuwa vijana. Walikuwa na umri wa kati ya miaka 19 hadi 22. Kila mmoja wao alikuwa akisafiri mbali na nyumbani, akikata kauli kwamba watu wake hawangejishughulisha naye iwapo angepatwa na jambo fulani.”

Uhuru wa Kutangatanga

Watu wengi zaidi leo hufunga safari za kimataifa kuliko ilivyokuwa miaka michache iliyopita. Kwa mfano, katika kipindi cha miaka mitano, idadi ya Waaustralia waliozuru Asia ilikuwa zaidi ya maradufu. Huku wakitafuta kujifunza mambo mapya au kujasiria, vijana wengi sana husafiri kwenda nchi za mbali. Wengi wa wasafiri hao hupanga kuomba lifti ili kupunguza gharama. Kwa kusikitisha, katika sehemu nyingi za ulimwengu, kuomba lifti si namna ya usafiri yenye kupendeza na iliyo salama kama ilivyokuwa zamani—kwa wanaoomba lifti au kwa wale wanaowapa.

Mtazamo unaofaa na shauku ya kusafiri hazipasi kuchukua mahali pa hekima inayofaa na itumikayo. “Mara nyingi hamu ya kusafiri humaanisha kwamba vijana huondoka bila kujitayarisha vyakutosha kwa ajili ya safari na bila kuelewa kikamili hatari au madaraka yao,” chasema kijitabu kilichoandikwa kwa ajili ya familia zinazotafuta watoto waliopotea.

Kijitabu hicho chaongezea hivi: “Watu ambao husafiri katika kikundi cha watalii kilichopangwa, au wanaofuata utaratibu mzuri wa safari hawapotei kwa urahisi. Iwe ni katika Australia au katika nchi nyingine, watu wengi ambao hatimaye huorodheshwa kuwa wamepotea, huwa ni wale wenye kubeba mifuko mgongoni na wanaosafiri kwa gharama ya chini zaidi.”

Iwe mtu anaomba lifti au la, kusafiri bila ratiba ya safari—ijapokuwa huvutia wengine wasiotaka kuelekezwa na ratiba hizo—kwaweza kumfanya mtu ashambuliwe kwa urahisi zaidi. Marafiki na jamaa wasipojua mahali alipo msafiri, hawawezi kusaidia hali ya dharura itokeapo. Mathalani, vipi ikiwa msafiri aishia hospitalini bila fahamu na hakuna yeyote nyumbani ajuaye mahali alipo?

Kuwasiliana

Katika kitabu chake Highway to Nowhere, mwandishi-habari Mwingereza Richard Shears aliandika kuhusu watu saba wenye kuomba lifti waliopotea ambao “waliacha kwa ghafula kuwasiliana na marafiki na familia zao.” Bila shaka, huenda hapo mwanzoni, familia zisiwe na hakika kama jamaa zao wamepotea au wameacha kuwasiliana tu. Hilo laweza kuwafanya wasitesite kufahamisha wenye mamlaka wanapokosa kusikia habari zozote kutoka kwa wasafiri hao.

Mara nyingi mmojawapo wa waombaji lifti alikatisha mazungumzo na wazazi wake katika simu kwa sababu ya kuishiwa na sarafu. Kwa sababu hiyo, wazazi wake walisihi familia ziwape watoto wao kadi za kupigia simu au njia fulani ya kupiga simu nyumbani. Ingawa kufanya hivyo labda hakungemwokoa mwanamke huyo kijana, mara nyingi mawasiliano ya kawaida yanaweza kusaidia msafiri aepuke au angalau asikabili matatizo mengi.

Huenda ikawa wale wasafiri saba wenye kubeba mifuko mgongoni waliouawa walisoma vitabu vya usafiri vinavyosema kwamba Australia ni mojawapo ya nchi zilizo salama zaidi ulimwenguni kwa waombaji lifti. Hata hivyo, kwa mara nyingine tena kuomba lifti kulithibitika kuwa kujihatarisha bure—hata mnapokuwa wawili-wawili na hata katika nchi zilizo “salama zaidi.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Yapasa itambuliwe kwamba katika sehemu fulani ni haramu kuomba lifti.

[Picha katika ukurasa wa 27]

Wazazi wanaweza kuepuka wasiwasi usiofaa kwa kuwapa watoto wao kadi za kupigia simu au njia fulani ya kupiga simu nyumbani