Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Baada ya Dhoruba—Kutoa Misaada Huko Ufaransa

Baada ya Dhoruba—Kutoa Misaada Huko Ufaransa

Baada ya Dhoruba—Kutoa Misaada Huko Ufaransa

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UFARANSA

FRANÇOISE alifungua mlango ili achukue kuni za kukoka moto. “Sikuamini macho yangu,” yeye akumbuka. “Maji yalijaa mlangoni, na wimbi kubwa la maji lilikuwa likivuka lango la bustani.” Mumewe, Thierry, alienda kuleta ngazi kutoka kwenye gereji huku maji yakimfika shingoni. Familia yote ilipanda darini naye akatoboa paa. Wenzi hao na watoto wao watatu waliolowa chepechepe na wenye hofu, walisubiri kwa muda wa saa nne ili kuokolewa. Hatimaye, polisi wa Ufaransa waliwaona na kuwaokoa kwa helikopta.

Mito iliyofurika furifuri kutokana na dhoruba hiyo ilibomoa maboma ya kuzuia maji na kuharibu madaraja. Mawimbi ya maji ya tope, nyakati nyingine yakiwa na kina cha meta kumi, yalifagilia mbali kila kitu. Zaidi ya watu 30 walikufa kutokana na dhoruba hiyo—walikwama katika magari yao au wakafa maji wakiwa usingizini. Mtu mmoja aliyeokolewa alilinganisha usiku huo wa kutisha katika mwezi wa Novemba na “mwisho wa ulimwengu.” Jimbo zima la kusini-magharibi mwa Ufaransa—miji na vijiji 329—lilitangazwa kuwa eneo la msiba.

Msiba Mbaya Zaidi Ungezuka Baadaye

Maeneo ya kusini-magharibi yalikumbwa na msiba mwingine punde tu baada ya dhoruba ya kwanza. Kanieneo ya angahewa yenye nguvu isivyo kawaida ilizuka kwenye Bahari ya Atlantiki na kutokeza upepo mkali wa kimbunga. Dhoruba ya kwanza ilipiga kaskazini mwa Ufaransa Desemba 26, 1999, na ya pili ikaleta maafa upande wa kusini usiku uliofuata. Upepo ulivuma kwa kasi ya zaidi ya kilometa 200 kwa saa. Ripoti rasmi zinaonyesha kwamba Ufaransa haijawahi kukumbwa na dhoruba kali ya namna hiyo tangu karne ya 17 hivi.

Hélène alikuwa na mimba ya miezi minane dhoruba hiyo ilipozuka. “Nilihofu kupindukia,” yeye akumbuka. “Mume wangu alikuwa akirejea nyumbani kwa pikipiki, nami ningeweza kuona matawi yakivurumishwa kila mahali. Nilikuwa na wasiwasi kwamba huenda hangemwona kamwe mtoto wake. Punde tu baada ya mume wangu kuwasili maji yalianza kufurika nyumbani mwetu. Ilitubidi kurukia dirishani.”

Angalau watu 90 walikufa Ufaransa. Ama walikufa maji au wakaangukiwa na vigae vya paa, dohani, au miti. Mamia wengine walijeruhiwa vibaya sana, kutia ndani raia na wanajeshi-waokoaji kadhaa. Dhoruba hiyo iliathiri pia nchi jirani, zaidi ya watu 40 walikufa Hispania, Uingereza, Ujerumani, na Uswisi.

Matokeo

Majimbo 69 kati ya 96 ya Ufaransa yalitangazwa rasmi kuwa “maeneo ya msiba wa asili.” Hasara inakadiriwa kuwa faranga bilioni 70 (dola bilioni 11 za Marekani). Uharibifu uliotukia katika miji, vijiji, na bandari fulani uliwakumbusha watazamaji kuhusu eneo lenye vita. Miti au milingoti ya umeme iliyong’olewa ilianguka na kuziba barabara na reli. Paa za majengo ziling’olewa, kreni za ujenzi zikaangushwa, na mashua zikavurumishwa magatini. Maelfu ya wakulima wa mazao ya kuuza walipoteza riziki yao, wakati vibanda vya kukuzia mimea na mashamba ya matunda yalipoharibiwa.

Kwa muda wa saa chache tu, dhoruba hiyo iliharibu kabisa misitu na hifadhi za wanyama za Ufaransa, iling’oa mamia ya maelfu ya ekari za misitu. Ofisi ya Kitaifa ya Misitu ya Ufaransa yasema kwamba takriban miti milioni 300 iliharibiwa. Miti mikubwa ya kuvutia iliyodumu kwa karne nyingi iling’olewa au kuchanwa-chanwa kama vijiti vya kiberiti. Upepo huo mkali ulifagia sehemu kubwa ya misitu ya Aquitaine na Lorraine.

“Nilienda msituni siku iliyofuata dhoruba hiyo,” akasema Bernard, mmoja wa Mashahidi wa Yehova ambaye ni mhifadhi wa misitu. “Nilipigwa na bumbuazi. Mandhari niliyoona haina budi kukushtua! Hapa, asilimia 80 ya washiriki wa kutaniko letu hutegemea msitu huo ili kujiruzuku. Watu, hasa wazee-wazee, wameshtuka sana.” Miti 10,000 katika bustani ya Jumba la Mfalme la Versailles, iling’olewa. “Bustani hiyo itarudia hali yake ya awali baada ya karne mbili,” akalalamika mmojawapo wa watunza-bustani wasimamizi.

Nyaya za umeme zilipokatika, zaidi ya sehemu moja kwa sita ya wakazi wa Ufaransa walikosa umeme. Licha ya jitihada na ujasiri wa kurekebisha huduma za umma, makumi ya maelfu ya watu hawakuwa wamepata umeme au huduma za simu majuma mawili baada ya dhoruba. Vijiji vidogo kadhaa vilikuwa havifikiki. Familia zilizolazimika kuteka maji visimani na kutumia mishumaa ziliona ni kana kwamba zinaishi miaka mia moja iliyopita wala si mwanzoni mwa karne ya 21.

Dhoruba hiyo iliharibu pia majengo ya umma, majumba makubwa, na makanisa. Majengo mengi ya kidini, kutia ndani Majumba ya Ufalme 15 ya Mashahidi wa Yehova yaliharibiwa. Katika sehemu fulani, mikutano ilifanywa kwa nuru ya mishumaa au taa za mafuta.

Mali za takriban familia 2,000 za Mashahidi wa Yehova ziliharibiwa na dhoruba, miti iling’olewa na vigae vya paa za nyumba vikaharibiwa kabisa na hata nyumba zikaharibiwa kabisa mito ilipofurika furifuri. Mashahidi kadhaa walijeruhiwa. Jambo la kusikitisha katika jimbo la Charente, ni kwamba Shahidi mmoja mwenye umri wa miaka 77 alikufa maji huku mkewe asiye na uwezo akitazama. Wengine waliponea chupuchupu. Gilbert mwenye umri wa miaka 70, akumbuka: “Nilinusurika kwa njia ya ajabu. Maji yenye nguvu yaliupasua mlango na kutapakaa nyumbani. Ghafula nilifunikwa na maji yenye kina cha meta moja na nusu. Nilijiokoa kwa kubamba kabati langu la nguo.”

Kutoa Msaada Uliohitajiwa

Dhoruba hiyo ilitokeza umoja wa pekee katika Ufaransa na kotekote Ulaya. Gazeti Le Midi libre lilisema: “Nyakati nyingine kutoa msaada huwa kama wajibu, iwe unatolewa kwa hiari, au kwa sababu ya urafiki au dhamiri.”

Mara baada ya dhoruba, halmashauri za uokoaji za Mashahidi wa Yehova zilianzishwa ili kuwasaidia washiriki wa makutaniko ya karibu hali kadhalika wengine walioathiriwa na msiba huo. Halmashauri za Ujenzi za Mkoa, ambazo kwa kawaida hujenga Majumba ya Ufalme, zilipanga vikundi vya wajitoleaji. Baada ya dhoruba kupiga upande wa kusini-magharibi mnamo Novemba, Mashahidi 3,000 walishiriki katika kazi ya uokoaji na usafishaji, na kuwasaidia wahasiriwa kuondoa matope na maji yaliyofurika nyumbani mwao. Mashahidi walikuwa miongoni mwa wajitoleaji wa kwanza kufika katika baadhi ya vijiji hivyo. Mashahidi walisafisha majengo ya umma, kama vile shule, ofisi za posta, majengo ya baraza la mji, makao ya watu wazee-wazee, hata eneo la makaburi. Mara nyingi walishirikiana na mashirika ya kutoa misaada.

Msaada ulitolewa kwa wote bila kujali itikadi zao za kidini. “Tulimsaidia kasisi wa kijiji. Tulisafisha chumba cha chini nyumbani mwake,” akasema Shahidi mmoja. Kuhusu wengine waliosaidiwa na Mashahidi, aliongezea hivi: “Watu waliona ni kana kwamba tulitoka mbinguni ili kuja kuwasaidia.” Ofisa mmoja alisema: “Huenda ukaiona kuwa njia yao ya kusoma Gospeli na kusaidia jirani zao. Nafikiri kwamba wale waliokuja waliishi kulingana na Gospeli na dini yao.” Mjitoleaji mmoja Shahidi alisema: “Moyo wako unakuchochea kuja kusaidia. Ni jambo lenye kupendeza sana kuweza kuwasaidia jirani zetu.”

Baada ya dhoruba hizo mbili kupiga mnamo mwezi wa Desemba, familia nyingi za Mashahidi hazikuweza kuwasiliana na ndugu zao Wakristo kwa siku kadhaa. Waangalizi wasafirio na wazee walio karibu walielekeza kazi ya kutoa msaada. Nyakati nyingine akina ndugu wanaoishi umbali wa kilometa chache tu hawakuweza kufikiwa kwa sababu barabara ziliziba na pia simu hazikuwa zikifanya kazi. Licha ya hatari kubwa ya kuangukiwa na miti, Mashahidi kadhaa walivuka kwa miguu au kwa baiskeli misitu iliyoharibiwa ili wakawasaidie washiriki wa kutaniko lao wanaoishi mbali. Wajitoleaji walijitahidi tena kusafisha shule, maktaba, kambi, nyumba za jirani zao na kuondoa miti iliyoanguka kwenye vijia msituni.

Kudumisha “Mazingira ya Upendo”

Wahasiriwa wengi wa misiba hiyo, hasa watoto wachanga na wazee-wazee, walishikwa na hofu kwa sababu ya yaliyowapata. Wale waliopoteza makao yao au kufiwa na mpendwa wao watahitaji muda mwingi na utegemezo wa familia na rafiki ili kuanza upya maisha yao. Baada ya mafuriko katika jimbo la Aude, Dakt. Gabriel Cottin, wa halmashauri ya dharura ya tiba ya akili, alisema: “Utegemezo wowote unaotolewa na watu wa dini ya mhasiriwa husaidia sana pia.”

Mashahidi wa Yehova huona kuandaa msaada wa aina hiyo kuwa wajibu wa Kimaandiko na wa kiadili. “Kusiwe na mgawanyiko katika mwili [wa kikundi cha Wakristo wa kweli],” akasema mtume Paulo. “Viungo vyao viwe na utunzaji uleule kimoja na chenzake. Na kiungo kimoja kikiteseka, viungo vingine vyote huteseka pamoja nacho.”—1 Wakorintho 12:25, 26.

“Saa chache baada ya dhoruba kupiga, ndugu na dada Wakristo wapatao 12 walikuja nyumbani kwetu ili kutusaidia kusafisha kila kitu,” asema Hélène, aliyetajwa mapema, ambaye sasa ni mama wa kisichana chenye afya. “Hata Mashahidi walioathiriwa na dhoruba hiyo walikuja kutusaidia. Msaada wao wa hiari na wa kutoka moyoni ulivutia sana!”

Odette, ambaye nyumba yake iliharibiwa na mafuriko, alisema hivi kuhusu Mashahidi wenzake: “Walinifariji sana. Hata huwezi kueleza unavyohisi. Nimeguswa sana moyoni na msaada niliopokea.” Shahidi mwingine alieleza kwa ujumla hisia za wengi kwa kusema hivi kwa uthamini: “Kwa kweli tuko kwenye mazingira ya upendo!”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18, 19]

“MAJI MEUSI YA BAHARI”

Katikati ya mwezi wa Desemba, kabla tu ya dhoruba, meli ya mafuta iitwayo Erika ilizama katika bahari yenye mchafuko kilometa 50 hivi kutoka pwani ya magharibi ya Ufaransa, ikimwaga tani 10,000 za mafuta baharini. Maji yalichafuliwa kwa umbali wa kilometa 400 kutoka kwenye pwani ya Brittany hadi Vendée. Dhoruba ilizidisha msiba huo wa mazingira kwa kusambaza mafuta hayo na kufanyiza utando-utando wenye kunata, na kuchafua eneo kubwa zaidi na hivyo kufanya kazi ya kuyaondoa mafuta hayo iwe ngumu zaidi. Maelfu ya wajitoleaji, vijana kwa wazee, walitoka kotekote Ufaransa ili kushiriki kuondoa mafuta hayo yenye kunata kwenye miamba na mchangani.

Aksidenti hiyo imesababisha uchafuzi mkubwa kupindukia wa mazingira ya baharini. Viwanda vya chaza na samaki-gamba vimeathiriwa sana. Wataalamu wa elimu ya ndege wanasema kwamba ndege wa baharini wapatao 400,000—puffin, vibisi, membe weusi, hasa guillemot—wamekufa. Idadi hiyo ni mara kumi zaidi ya idadi ya ndege waliokufa baada ya meli kubwa ya mafuta iitwayo Amoco Cadiz kuzama karibu na Brittany mwezi wa Machi 1978. Wengi wa ndege hao walitoka Ireland, Scotland, Uingereza na kuhamia pwani ya Ufaransa katika majira ya baridi kali. Mkurugenzi wa Shirika la Kulinda Ndege la Rochefort alisema hivi: “Utando huo wa mafuta ni msiba mkuu. Ni msiba mbaya zaidi kuwahi kutokea. . . . Twahofu kwamba jamii nadra za ndege zitaadimika au hata kutoweka kutoka kwenye fuko za Ufaransa.”

[Hisani]

© La Marine Nationale, France

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mamia ya watu waliokolewa na helikopta, kama ionyeshwavyo hapa katika Cuxac d’Aude

[Hisani]

B.I.M.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Reli iliyoharibiwa ambayo sasa haielekei popote iko katikati ya mashamba ya mizabibu yaliyoharibiwa

[Hisani]

B.I.M.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mamia ya magari yaliyopondwa-pondwa yalitapakaa kila mahali

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mtu huyu alikwama kwa muda wa saa saba huko Villedaigne

[Hisani]

J.-M Colombier

[Picha katika ukurasa wa 17]

Misonobari iliyochanwa-chanwa kama vijiti vya kiberiti katika jimbo la Creuse

[Hisani]

© Chareyton/La Montagne/MAXPPP

[Picha katika ukurasa wa 17]

Miti 10,000 iling’olewa katika bustani ya Jumba la Mfalme la Versailles peke yake

[Hisani]

© Charles Platiau/Reuters/MAXPPP

[Picha katika ukurasa wa 17]

Asubuhi iliyofuata baada ya dhoruba kupiga Saint-Pierre-sur-Dives, Normandy

[Hisani]

© M. Daniau/AFP

[Picha katika ukurasa wa 18]

Vikundi vya Mashahidi wa Yehova wakisafisha makao ya wazee-wazee huko La Redorte (juu) na jengo la baraza la mji wa Raissac d’Aude (kulia)