Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ukumbi wa Michezo ya Kuigiza wa Epidaurus—Haujabadilika kwa Karne Nyingi

Ukumbi wa Michezo ya Kuigiza wa Epidaurus—Haujabadilika kwa Karne Nyingi

Ukumbi wa Michezo ya Kuigiza wa EpidaurusHaujabadilika kwa Karne Nyingi

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UGIRIKI

JE, WEWE hupenda michezo ya kuigiza? Je, wewe huvunjika mbavu kwa kicheko utazamapo mchezo wa kuchekesha? Je, wewe huchangamshwa au hata kuelimishwa na mchezo wa kuigiza wenye masomo unaogusa hisia au kukuelimisha juu ya utu wa binadamu? Basi waweza kupendezwa kujifunza kuhusu ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Epidaurus. Hutajwa kuwa chimbuko la uigizaji katika Ugiriki ya kale.

Mwanajiografia Mgiriki Pausanias, wa karne ya pili W.K., aliandika kwamba ‘kuna ukumbi mashuhuri wa kale katika Epidaurus. Japo kumbi za Kiroma ni bora na kubwa mno, hakuna msanifu-ujenzi awezaye kushindana na umaridadi na mpangilio bora wa ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Epidaurus.’

Umehifadhiwa kwa Njia Bora Zaidi

Kijiji kidogo cha Epidaurus kiko kilometa 60 hivi kusini mwa mji wa Corinth huko Ugiriki. Karne 25 zilizopita, kilikuwa kituo muhimu cha kibiashara na kidini.

Baadaye, ukumbi huo mkubwa ulifunikwa kabisa na safu laini ya vilima, mashamba, na mizeituni. Hata hivyo, Panagís Kavadías, mwakiolojia maarufu wa Ugiriki wa karne ya 19, alikuwa na hakika kwamba vilima hivyo vilificha siri fulani. Maelezo ya Pausanias yaliyonukuliwa mwanzoni yalimchochea kufanya uchunguzi, na alijua kwa hakika kwamba angegundua ukumbi maridadi katika ardhi hiyo. Na kwa kweli aliugundua katika masika ya 1881.

Kavadías alifukua ukumbi huo maridadi usiobadilika sana baada ya kufanya kazi ngumu kwa miaka sita. Waakiolojia husema kwamba ukumbi huo ulijengwa na Polyclitus Mdogo, mchongaji na msanifu-ujenzi hodari kutoka jiji jirani la Argos yapata mwaka wa 330 K.W.K. Msanifu-ujenzi wa kisasa Mános Perrákis afunua maoni ya watafiti wengi anapouita ukumbi wa Epidaurus “ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Ugiriki ulio maarufu zaidi na uliohifadhiwa kwa njia bora zaidi.”

Ugunduzi wa ukumbi wa Epidaurus umekuwa muhimu sana kwa akiolojia na kwa usanifu-ujenzi. Huku kumbi nyingi za kale zilizopo zikiwa zimeharibika sana au kujengwa upya, ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Epidaurus haujabadilika kwa karne nyingi kwa sababu ulifunikwa kwa udongo wenye kina cha meta sita.

Watalii waweza kuona waziwazi sehemu muhimu za ukumbi huo leo. Jukwaa la dansi na uigizaji lina sakafu ya duara ambayo imezingirwa na mstari mwembamba wa marumaru. Sakafu yake imetengenezwa kwa udongo ulioshindiliwa, na kuna madhabahu katikati. Kuna mabaki ya msingi wa chumba cha nyuma ya jukwaa la dansi na uigizaji. Mwanzoni, waigizaji walitumia jukwaa la dansi na uigizaji, na mandhari zilifanyizwa kwa paneli zenye michoro zilizowekwa pembeni mwa jukwaa kwenye mabamba ya pembe tatu yanayozunguka. Baadaye, waigizaji walianza kutumia jukwaa kuu, na wachezaji-dansi wakaachiwa jukwaa la dansi, na paneli za mandhari zilitiwa kwenye ukuta wa ukumbi.

Mwanzoni, ukumbi huo wa Epidaurus ulikuwa na viti 6,000. Katika karne ya pili K.W.K., sehemu ya juu ilipanuliwa na kuongezwa safu 21 za viti, ikawa na zaidi ya viti 13,000. Viti vilivyoko kwenye safu ya mbele, vilivyohifadhiwa kwa ajili ya wageni waheshimiwa, vilitofautiana na vinginevyo kwa kuwa vilitengenezwa kwa jiwe jekundu na vilikuwa na kiegemeo.

Ukuzaji wa Sauti wa Kustaajabisha

Ukumbi wa Epidaurus ni mashuhuri kwa ajili ya ukuzaji-sauti bora. “Sauti ndogo sana—kuvuta pumzi au kurarua kipande cha karatasi—yaweza kusikiwa vizuri katika safu ya juu kabisa ya viti,” asema profesa wa akiolojia S. E. Iakovídis.

Wanapozuru ukumbi huo, watalii wengi hupenda kusimama katikati ya jukwaa na kukariri mashairi, kuimba nyimbo, au hata kuwanong’onezea marafiki wao wanaoketi katika safu za juu kabisa za viti. Wao huvutiwa na jinsi ambavyo sauti hukuzwa kwa njia bora kufikia kila pembe ya ukumbi huo mkubwa.

Ukuzaji huo bora wa sauti hutokana na umbo la nusu-duara la ukumbi huo wa Epidaurus unaoshabihi uwanja-duara. Hilo hutukumbusha mahubiri ya Yesu kwa umati wa watu katika viwanja-duara vya asili—mara nyingi kwenye miteremko ya milima—ili aweze kusikiwa wazi na kila mtu.—Mathayo 5:1, 2; 13:1, 2.

Isitoshe, mwinamo wa safu za viti katika ukumbi wa Epidaurus hupunguza umbali wa safu za juu kutoka jukwaani. Mawimbi ya sauti husikika vizuri katika safu hizo za juu.

Jambo jingine linalochangia ukuzaji bora wa sauti ni nafasi ifaayo toka safu moja hadi nyingine. Hilo husaidia sauti inayosikika wazi isambazwe kila mahali kwa kiasi kilekile. Mambo mengine yanayochangia hutia ndani mrudisho wa sauti inapogonga ukuta mgumu wa ukumbi na viti, marumaru bora iliyotumiwa, bustani tulivu, na upepo unaovuma daima kutoka jukwani kuelekea kwenye umati.

Ukumbi—Mahali Pafaapo pa Michezo ya Kuigiza

Watazamaji wangeweza kuona na kusikia vizuri michezo ya kuigiza kwa sababu Wagiriki wa kale walijenga kwa uangalifu na kwa ustadi mno kumbi kama huo wa Epidaurus. Michezo hiyo ya kuigiza ilitokana na karamu za uzalishaji za kusherehekea mavuno na mazao ya zabibu na vilevile dhana ya kifo na kutokeza tena uhai. Karamu hizo za ulevi na ulafi zilikusudiwa kumheshimu Dionysus, mungu wa kihekaya wa divai na uzalishaji. Sherehe hizo zilitia ndani kusifu miungu ya kihekaya na uigizaji wa matukio. Aina tatu za michezo zikaibuka: michezo ya tanzia, michezo ya kuchekesha, na michezo ya dhihaka. Watawala wa jiji waliunga mkono michezo hiyo iliyopendwa sana ili wajipatie mamlaka zaidi ya kisiasa.

Baada ya muda, uvutano wa sherehe za Dionysus kwa uigizaji na umashuhuri wa karamu murua za ulafi na ulevi ukadidimia. Waigizaji mashuhuri wa karne ya tano K.W.K., kama vile Aeschylus, Sophocles, na Euripides, walitafuta vichwa vipya vya michezo yao katika historia na hekaya za Ugiriki. Uhitaji wa kumbi kubwa kama ule wa Epidaurus ulitokezwa na ongezeko kubwa la wapenzi wa michezo ya kuigiza. Ustadi na uangalifu mkubwa sana ulihitajiwa katika ujenzi wa kumbi kwa sababu wasikilizaji walihitaji kusikia kila neno katika michezo hiyo—ambayo mara nyingi ilihusisha mchezo wa maneno na mijadala.

Kila mchezo wa kuigiza ulihitaji kikundi cha waimbaji (kwa kawaida watu 10 hadi 15) na waigizaji (kila sehemu ikiwa na waigizaji-wasemaji watatu tu). Waigizaji waliitwa hy·po·kri·taiʹ, wale wanaoitikia nyimbo na uchezaji. Baada ya muda, neno hilo likaanza kutumiwa kama sitiari kuhusu mtu anayetenda kwa udanganyifu au kwa unafiki. Gospeli ya Mathayo ilitumia neno hilo kuwaeleza jinsi walivyokuwa waandishi na Mafarisayo wadanganyifu katika siku za Yesu.—Mathayo 23:13.

Michezo ya Kale ya Kuigiza Leo Katika Epidaurus

Uigizaji wa michezo ya kale umeibuka tena katika Epidaurus huko Ugiriki na kwingineko. Kufikia mwanzoni mwa karne ya 20, michezo ya kale ya kuigiza ya Ugiriki, hasa michezo ya tanzia, ilipendwa tu na wasomi. Lakini kuanzia mwaka wa 1932 na kuendelea, tangu kuanzishwa kwa Chama cha Kitaifa cha Sanaa katika Ugiriki, michezo ya waigizaji wa kale imetafsiriwa katika Kigiriki cha kisasa.

Tangu mwaka wa 1954, sherehe ya michezo ya kuigiza ya Epidauria hufanywa kila mwaka. Kila kiangazi, vikundi vingi vya sanaa kutoka Ugiriki na nchi nyingine hukusanyika katika ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Epidaurus ili kuonyesha michezo yao ya kale. Maelfu ya watalii na wapenzi wa sanaa huzuru ukumbi huo ili kutazama uigizaji wa kisasa wa michezo iliyoandikwa yapata miaka 2,500 iliyopita.

Kwa hiyo, wakati ujao uzurupo Ugiriki, unakaribishwa Epidaurus. Baada ya kutazama ukumbi wake wenye kuvutia, huenda ukasema kama alivyosema Pausanias: ‘Hakuna msanifu-ujenzi awezaye kushindana na umaridadi na mpangilio bora wa ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Epidaurus.’

[Sanduku katika ukurasa wa 13]

Ukumbi wa Michezo ya Kuigiza na Wakristo wa Mapema

“Tumekuwa kitu cha kutazamwa mahali pa michezo kwa ulimwengu, na kwa malaika, na kwa wanadamu,” ndivyo mtume Paulo alivyowaandikia Wakristo katika Korintho, walioishi karibu na Epidaurus. (1 Wakorintho 4:9; Waebrania 10:33) Alimaanisha kwamba kwa sababu ya kuaibishwa na kunyanyaswa, ilikuwa ni kana kwamba walikuwa katika ukumbi wa maonyesho wakitazamwa na ulimwengu wote. Katika siku za Paulo, uigizaji wa michezo katika kumbi ulikuwa tafrija iliyopendwa sana. Hata hivyo, Wakristo wa mapema walionywa wajiepushe na ukosefu wa adili na jeuri ya kikatili, ambazo zilionyeshwa kwa kawaida katika michezo ya sanaa ya wakati huo. (Waefeso 5:3-5) Nyakati nyingine Wakristo walikokotwa kwenye kumbi au viwanja vya maonyesho vya Milki ya Roma ili wawatumbuize watu, hata wakilazimishwa wakabiliane na hayawani.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Sophocles

Aeschylus

Euripides

[Hisani]

Waigizaji Wagiriki: Musei Capitolini, Roma

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 11]

Courtesy GNTO