Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kupitia Bahari Zenye Dhoruba Hadi Maji Yenye Utulivu

Kupitia Bahari Zenye Dhoruba Hadi Maji Yenye Utulivu

Kupitia Bahari Zenye Dhoruba Hadi Maji Yenye Utulivu

KAMA ILIVYOSIMULIWA NA HANS STURM

KWA miaka zaidi ya 200, wanaume wa familia yangu walikuwa mabaharia. Tamaa yangu kubwa ilikuwa kumwiga baba yangu, ambaye alikuwa amemwiga babu yangu aliyekuwa baharia.

Mwaka wa 1914, Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ilipoanza, baba yangu aliandikishwa kwa lazima kwenye jeshi la baharini la Ujerumani akiabiri kwenye chombo cha kuondolea mabomu baharini katika Bahari ya Baltiki. Kufikia mwaka wa 1916, Baba alipewa mgawo kwenye merikebu ya biashara ambayo ilitumiwa kuingiza nchini mawe yenye madini ya chuma kutoka Sweden hadi vita vilipokoma. Alikufa mwaka wa 1919, nilipokuwa na umri wa miaka minane tu, lakini nilichochewa nilipomkumbuka.

Ili kutimiza tamaa yangu ya kuendelea katika kazi niliyochagua, ilinibidi nitumike baharini kwa miaka minne, huku nikisafiri kwa merikebu kwa muda wa miezi 20 kati ya miaka hiyo. Ndipo tu ningeweza kujiandikisha katika chuo cha kujifunza kuendesha chombo baharini. Basi, nilipofika umri wa miaka 15, mama yangu alinitoa Stettin (ambayo sasa ni Szczecin, Poland), ambako nilizaliwa, hadi Hamburg, Ujerumani. Tulijua kwamba kampuni ya Laeisz ilikuwa na merikebu kadhaa, nasi tulitumaini kwamba ningejiunga na merikebu moja nikiwa mwanafunzi. Hatungeweza kulipa karo, lakini kwa sababu ya sifa ya baba yangu, kampuni ya Laeisz ilinikubali bila kunitoza.

Mwaka wa 1927, nilianza kuabiri kwa Padua, * chombo cha chuma chenye milingoti minne. Kilisafiri kutoka Hamburg hadi Chile kuchukua mizigo ya shura. Hakikuendeshwa kwa mota—ila matanga tu. Safari hizo za kuvuka Atlantiki zilikuwa jambo lenye kusisimua kwetu sote vijana.

Mara nyingi tulipitia kwenye bahari zenye dhoruba. Nyakati hizo, matanga yalishushwa. Nilihisije kupanda kamba za merikebu ili kushusha matanga wakati merikebu ilipokuwa ikisukwasukwa? Lazima nikubali kwamba niliogopa sana! Lakini nilipoamriwa kupanda, niliacha kufikiria mambo mengine, nikapanda tu na kufanya yale niliyokuwa nimeamriwa nifanye.

Mambo Yaliyopita Uwezo Wangu

Mama yangu alikuwa Mkatoliki, lakini upesi baada ya kifo cha baba yangu, alianza kushirikiana na Ernste Bibelforscher, au Wanafunzi wa Biblia Wenye Bidii, kama walivyojulikana Mashahidi wa Yehova wakati huo huko Ujerumani. Alibatizwa mwaka wa 1923. Sikuvutiwa na dini ya Katoliki, na yale ambayo mama yangu alisema yalikuwa na maana. Kwa hiyo, nikiwa na dada yangu mchanga, Margot, nilikuwa nikiandamana na Mama kwenye mikutano ya funzo la Biblia.

Mwaka wa 1929, niliiacha Padua na kwa miaka mitatu iliyofuata nikaabiri merikebu nyingine za moshi. Merikebu hizo zilinipeleka hadi bandari za kaskazini mwa Ulaya na kwenye Mediterania. Katika safari moja ya baharini, niliabiri kuzunguka ulimwengu. Nilifurahia maisha hayo nami nikawa na hamu ya kujiandikisha katika chuo cha kujifunza kuendesha chombo baharini huko Stettin, kama alivyofanya baba yangu. Mwaka wa 1933, nilianza mtalaa wa miezi 18 ili nihitimu kuwa ofisa wa sitaha merikebuni. Hata hivyo, mipango yangu ilikatizwa na mambo yaliyopita uwezo wangu.

Hitler alipata mamlaka mwaka huohuo, na utukuzo wa taifa ukaenea Ujerumani. Wanafunzi walifurahia kupiga kelele, “Mwokozi Ni Hitler!” Lakini kutokana na yale niliyojifunza kutoka kwa mama yangu nilijua kwamba singeweza kufanya hivyo. Niliulizwa nieleze sababu ya kukataa kufanya hivyo, lakini haikukubaliwa. Nilifukuzwa shuleni. Mkuu wa shule alikuwa mwanamume mwenye fadhili na akanipa barua iliyosema kwamba nilikuwa nimejifunza kwa mwaka mmoja. Kwa kuwa sikuweza kumaliza mtalaa huo, niliondoka bila hati zozote za kufuzu. Maisha yaliniendea mrama.

Msongo Waongezeka

Niliwekwa kwenye orodha ya watu wabaya kwa sababu ya msimamo wangu wa kutokuwemo. Sikuzuiwa kuabiri kwenye merikebu yoyote tu, bali pia sikuweza kupata kazi ya kuajiriwa hata kidogo, kwa hiyo nilikaa nyumbani nikimsaidia mama yangu. Alipata riziki kwa shida kwa kupikia watu, nami nilifurahia kumwoshea vyombo na kumtayarishia mboga. Mwaka wa 1935, miaka minne kabla ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, maisha yangu yalibadilika.

Mjomba wangu Oskar aliishi huko Danzig (ambayo sasa ni Gdansk). Aliposikia kuhusu magumu yangu, alinialika nimfanyie kazi katika mkahawa wake. Mjomba wangu na mkewe, Rosl, walikuwa Mashahidi wa Yehova. Nilikubali mwaliko wao wenye fadhili. Ijapokuwa hawakuweza kunilipa mshahara wa kawaida, nilihisi nikiwa salama kwao.

Baada ya Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, Danzig likaitwa jiji huru, likisimamia eneo kubwa mno chini ya mwelekezo wa Ushirika wa Mataifa. Kusudi lilikuwa kuiwezesha Poland itumie bahari, lakini kwa kweli mpango huo ulitenga kabisa Prussia Mashariki na sehemu zote za Ujerumani. Hitler hakupenda hali hiyo. Kwa hakika, Vita ya Ulimwengu ya Pili ilianza ghafula wakati alivamia Poland na kujitwalia nchi hiyo.

Muda fulani baada ya mimi kufika, mjomba na shangazi yangu walikuwa wanamtunza mwanamume mmoja mchanga ambaye alikuwa amefungwa katika kambi ya mateso kwa sababu alikuwa Shahidi wa Yehova. Aliniambia jinsi alivyotendwa vibaya huko. Muda mfupi baadaye, mjomba na shangazi yangu walikamatwa kwa kukataa kumtukuza Hitler, lakini waliachiliwa. Wakati huu mimi pia nilihojiwa na askari wa Gestapo, ingawa hawakunikamata.

Wakati huohuo, kule Stettin mama alipokea barua ya kunitaka nijiunge na jeshi la Ujerumani. Upesi akaandika barua ya tahadhari, akiniomba nimtembelee shangazi Naomi, ambaye aliishi kaskazini mwa Sweden. Nikatambua alichomaanisha—toka nchini!

Mnyanyaso wa Nazi

Mambo yalikuwa yanaendelea kuwa magumu. Mjomba na shangazi yangu walikamatwa tena. Wakati huu walipelekwa kwenye kambi ya mateso huko Stutthof, safari ya muda wa saa mbili kutoka Danzig. Walizuiwa huko hadi mwisho wa vita, mwaka wa 1945. Kwa kusikitisha, nilipata habari kwamba mjomba wangu alikufa kwenye merikebu iliyokuwa ikiwapeleka wafungwa wa kambi upande wa magharibi ili waepe uvamizi wa askari-jeshi wa Urusi. Hata hivyo, shangazi yangu alinusurika, na akawa mweneza-evanjeli wa wakati wote.

Mjomba na shangazi yangu walipopelekwa Stutthof, mama yangu alikamatwa huko Stettin, naye akakaa gerezani kwa miezi saba. Dada yangu alikuwa ameolewa na mwana wa wenzi fulani Mashahidi, naye alikuwa gerezani wakati mmoja na mama yangu. Mume wake na binti yao walipelekwa kwenye kambi za mateso. Mume wake alifia huko, na binti yake alikaa kwenye kambi mbaya zaidi kutia ndani kambi ya Belsen, kwa miaka minane.

Wakati mmoja, kwa sababu ya kukataa kushonea jeshi kanda za kuwekea risasi, mpwa wangu wa kike na Mashahidi wengine walilazimishwa kusimama nje wakiwa wamevaa mavazi mepesi sana kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni mwezi wa Novemba. Chakula chao cha kila siku kilipunguzwa kuwa kipande cha mkate na jagi ya maji, na wakapewa mchuzi moto baada ya kila siku tatu. Walilala kwenye sakafu ya sementi bila matandiko, wala hata mabua. Hali iliendelea hivyo kwa majuma sita, na wasimamizi wa kambi walishangaa kwamba walinusurika.

Kuponyoka—Nini?

Baada ya mjomba na shangazi yangu kukamatwa mara ya pili, nilijua kwamba ilikuwa ni lazima niondoke Danzig kabla ya askari wa Gestapo kunirudia. Mjomba wangu alikuwa amenikopesha kiasi fulani cha fedha, nami hatimaye nikapata ruhusa ya kusafiri kwenye merikebu ya Poland iliyokuwa ikienda Hull, pwani ya mashariki mwa Uingereza. Nilipofika, nilipewa ruhusa ya kukaa miezi mitatu, muda wa kawaida kwa mgeni.

Upesi nikaenda mtaa wa 34 Craven Terrace huko London, kwenye ofisi ya tawi ya Watch Tower Society. Nilikutana na Pryce Hughes, aliyekuwa msimamizi wa tawi wakati huo. Alipanga nikae na mtu wa ukoo wake Stanley Rogers, huko Liverpool, pwani ya magharibi mwa Uingereza. Stanley alinitendea kwa fadhili sana.

Nilibatizwa katika masika ya mwaka wa 1937 huko Liverpool, nikionyesha wakfu wangu kwa Yehova. Hata hivyo, bado nilitaka kuwa baharia, kwa hiyo nilijiandikisha katika Liverpool Navigation College nami nikapata leseni ya kuwa ofisa wa daraja la pili wa sitaha baada ya miezi miwili. Muda wa kibali changu cha kukaa Uingereza ulikuwa unakaribia kwisha, kwa hiyo marafiki wangu huko Liverpool wakawasiliana na mbunge wao, na muda wangu ukaongezwa kwa miezi mitatu zaidi—muda niliohitaji ili kutimiza mambo yangu.

Kwa sababu ya uzoefu wangu wa kuabiri kwenye merikebu ya Padua, mfunzi wangu wa uanamaji kwenye chuo cha kuendesha chombo baharini alipendezwa nami kipekee. Alipojua kuhusu mashaka yangu, alipendekeza niende kwenye kampuni ya Blue Funnel Line. Kule, nilikutana na mmojawapo wa wakurugenzi wake, Lawrence Holt. Miaka miwili baadaye nilipokutana naye kwenye mojawapo ya merikebu ya kampuni hiyo huko Liverpool, aliniuliza kama nimepata leseni yangu ya ofisa wa daraja la kwanza wa sitaha. Nilimwambia kwamba nilihitaji majuma mawili tu ya uzoefu wa kutumika kwenye jukwaa la meli, kwa hiyo akapanga niabiri kuelekea Port Said, Misri.

Niliporudi Liverpool Julai 7, 1939, nilipanga kufanya mtihani wangu wa leseni ya kuwa ofisa wa daraja la kwanza wa sitaha, lakini jambo hilo halikuwezekana kwa kuwa vita ilikuwa karibu. Badala yake, nilitumwa kwenye merikebu moja huko London. Wenye mamlaka wa serikali walipogundua hilo, waliniondoa kwenye merikebu zote mara moja nao wakataka kunitia gerezani kama adui mgeni kwa sababu nilikuwa Mjerumani. Lakini Bwa. Holt alinitetea, nami nikapewa kazi ya kuwa mtunzaji wa bustani huko Liverpool. Hata hivyo, katika Mei 1940, nilikamatwa, na mwezi wa Juni, nikapelekwa Kanada kwa merikebu ya S.S. Ettrick.

Naenda Kanada

Merikebu Ettrick ilibeba Wajerumani wapatao 5,000, nusu yao wakiwa wakimbizi na nusu nyingine wakiwa wafungwa wa vita. Miongoni mwa wakimbizi alikuwa Count von Lingen, kama tulivyomjua, mjukuu wa aliyekuwa hapo zamani maliki Mjerumani. Barua zetu zote zilikaguliwa, kwa hiyo ofisa alipoona barua kutoka kwa Von Lingen aliyomwandikia Malkia Mary, Mama ya Malkia wa Uingereza, ikiwa na salamu ya ufunguzi “Mpendwa Shangazi Mary,” aliishuku. Hata hivyo, Von Lingen alisema kweli—familia za kifalme za Uingereza na Ujerumani zilihusiana kwa ukaribu. Kwangu mimi, kisa hiki kilikazia tu ujinga na ubatili wa vita.

Stanley Rogers, aliyetajwa mapema, alikuwa ametumikia akiwa pilgrimu (kama walivyoitwa waangalizi wasafirio wa Mashahidi wa Yehova wakati huo) huko Kanada wakati wa vita hivyo viwili vya ulimwengu. Alikutana na Mashahidi akiwa huko, nao wakawasiliana nami na Shahidi mwenzangu Tony Steffens, ambaye alikuwa amefukuzwa nchini. Barua zao na vifurushi vyao vilitutia moyo sana. Nilitiwa kizuizini kwa miaka miwili na nusu katika kambi nane mbalimbali, ambamo nilitumia wakati wangu mwingi kutengeneza meza na benchi za mbao.

Narudi Uingereza na Kuwa Huru!

Vita ya Ulimwengu ya Pili ilipokaribia kwisha, nilirudishwa Uingereza, kwenye kambi ya kizuizi kwenye Kisiwa cha Man. Nikiwa huko, John Barr, kutoka ofisi ya tawi ya Watch Tower Society huko London—ambaye sasa ni mshiriki wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova—alinitembelea akiwa ameandamana na Mashahidi wa hapo. Niliachiliwa huru mwaka wa 1944, nikajiunga tena na Stanley. Wakati huo, Stanley alikuwa ameoa Nita Thomas na alikuwa akiishi Birkenhead, bandari ya mto Mersey iliyoelekeana na Liverpool. Huko ndiko nilikokutana na Olive, dada ya Nita, nasi tukafunga ndoa mwaka uliofuata.

Mara tu tulipopata kibali, Olive na mimi tulisafiri kwenda Ujerumani kumwona mama yangu. Nilivunjika moyo kupitia majiji yaliyoharibiwa kabisa niliyokuwa nimeyajua vizuri sana. Nilitaka hasa kwenda Hamburg kutembelea ofisi ya Laeisz. Nilishangaa kama nini kukutana na Kapteni Piening huko, mtaalamu wa Padua kwenye safari zangu mbili za mwisho mwaka wa 1928 na 1929! Wakati wa vita alifanya kazi wakati wote jeshini, na wana wake wawili waliuawa katika pambano hilo. Alikuwa ameshuka moyo sana. Nilihuzunishwa sana na yale niliyosikia na kuona.

Kampuni ya Blue Funnel Line iliendelea kupendezwa nami nilipokuwa nikiishi Kanada, nao wakaniajiri kwa moyo wote niliporudi. Hatimaye mwaka wa 1947, nikastahili kupata leseni yangu ya ofisa wa daraja la kwanza wa sitaha. Mwaka uliofuata, Olive akawa mweneza-evanjeli wa wakati wote.

Napata Kusudi Langu Maishani

Nilianza kuabiri tena, na wakati wa safari zangu nilikutana na wamishonari kadhaa Mashahidi katika nchi za Mashariki ya Mbali. Lakini mkusanyiko huko London mwaka wa 1947 uligusa sana moyo wangu, kwa kuwa ulinisaidia niazimie kuweka mradi wa kumtumikia Yehova wakati wote. Waajiri wangu walitamaushwa. Lakini mwaka wa 1952 kwa fadhili walinipa kazi ya muda ofisini ili niweze kuhubiri wakati wote na Olive. Tamaa yangu kubwa ya kutumia maisha yangu baharini ilishindwa na tamaa yenye kuchochea zaidi.

Mimi na Olive tulifurahia sana kuhubiri pamoja na tulikuwa na pendeleo la kusaidia watu wengi wapate ujuzi sahihi wa kweli za Biblia. (2 Wakorintho 3:2, 3) Miaka baada ya miaka, nimefurahia mapendeleo ya ziada kwenye mikusanyiko ya wilaya na kwenye makusanyiko ya mzunguko. Leo hii naendelea kutumika nikiwa mzee katika Wirral Peninsula, karibu na Birkenhead.

Mpenzi wangu Olive alikufa mwaka wa 1997. Nikikumbuka ya nyuma, naweza kuona kwamba katika maisha yangu ya mwanzoni, niliokoka bahari zenye msukosuko mwingi. Lakini hatimaye, kwa mwelekezo wenye upendo wa Yehova, niliabiri, kwa kusema kitamathali, na mwenzi mwenye upendo katika maji yenye utulivu kwa miaka 50 katika kazi-maisha kuu kuliko zote—ile ya kumtumikia Yehova.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Mwaka wa 1946 Muungano wa Sovieti ulipewa merikebu Padua na ikabadilishwa jina ikawa Kruzenshtern.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Nikiwa na baba na mama yangu, mwaka wa 1914

[Picha katika ukurasa wa 19]

Kitabu changu cha Kijerumani, kilichorekodi safari zangu za baharini kwenye merikebu “Padua” yenye milingoti minne

[Picha katika ukurasa wa 21]

Pamoja na mke wangu, Olive, kwenye mkusanyiko wa London mwaka wa 1974