Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Mwezi Huathiri Maisha Yako?

Je, Mwezi Huathiri Maisha Yako?

Je, Mwezi Huathiri Maisha Yako?

KWA maelfu ya miaka, watu wameamini kwamba mwezi huathiri viumbe duniani. Imedhaniwa kwamba sura za mwezi huathiri mimea, wanyama, na hata wanadamu. Ingawa dhana fulani za kale zenye kupendwa sana zimepingwa na utafiti wa kisasa wa sayansi, itikadi nyingine zingalipo leo. Mambo hakika hufunua nini?

Watu fulani wanasadiki kwamba kuna uhusiano kati ya sura za mwezi na ukuzi wa mimea. Kwa hiyo, wao hutumia kalenda na vitabu vya matukio ili kuamua wakati wa kupanda maua, kutia mbolea, kuweka divai kwenye chupa, au kuhifadhi vyakula makoponi. Hilo hufanywa kuambatana na itikadi ya kwamba endapo kazi fulani zitafanywa wakati wa sura isiyofaa ya mwezi, ubora wa bidhaa utapungua. Kichapo kimoja chawashauri hivi wakulima: “Mboga mbichi za kuliwa zapasa kuvunwa hasa mwezi unapokuwa mpevu, ilhali mboga za kuhifadhiwa zapasa kuvunwa mwezi unapodidimia.” Je, zoea hilo lina msingi wowote wa kisayansi?

Uchunguzi fulani huhusianisha ukuzi wa mimea na mwendo wa mwezi. Hata hivyo, wanasayansi wengi hawasadiki jambo hilo. Wanasema kwamba mwendo wa mwezi ni tata, si wa kawaida kabisa, na athari zake si wazi, kwa hiyo ni vigumu kurudia majaribio yanayotegemeza uchunguzi huo.

Lakini athari fulani za mwezi zimethibitishwa. Kwa mfano, imethibitishwa kwamba utendaji, ulaji, uzalishaji, na utendaji wa kibiolojia wa viumbe wengi huhusiana na kujaa na kupwa kwa maji, ambayo huathiriwa moja kwa moja na nguvu za uvutano za mwezi.

Watu wengine hudai kwamba ikiwa mwezi huathiri kujaa na kupwa kwa maji, basi lazima uathiri wanadamu vilevile, kwa kuwa sehemu kubwa ya mwili wa mwanadamu ni maji. Lakini vipi juu ya ule unaodhaniwa kuwa uhusiano baina ya sura za mwezi na magonjwa ya kiakili, wakati wa kuzaliwa, na hata hedhi, ambayo inachukua karibu muda sawa na mwezi-mwandamo?

Uchunguzi umefanywa katika taaluma na tiba ya magonjwa ya akili, elimu-nafsia, na elimu-uzazi ili kupata ukweli wa jambo hilo. Matokeo hayaridhishi. Watafiti fulani hudai kwamba wamepata uhusiano mdogo baina ya utendaji wa wanadamu na mwendo wa mwezi, lakini wengine hukiri waziwazi kwamba hakuna uhusiano wowote. Wao husema kwamba kama mwendo wa mwezi ungekuwa unaathiri waziwazi uzazi wa wanadamu, uhusiano huo ungekuwa umethibitishwa zamani za kale. Isitoshe, wanasayansi kwa ujumla hawajasadikishwa na nadharia yoyote inayoeleza zile zinazoitwa eti athari za mwezi kwa mwanadamu. *

Japo sayansi imethibitisha kwamba mwezi huathiri kwa kiasi fulani viumbe mbalimbali duniani, kadiri ya athari hizo haiwezi kuamuliwa kwa urahisi. Ulimwengu wetu mzima ni tata, na angalau kwa sasa, mifumo mingi ya kustaajabisha inayouongoza bado haijulikani.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Baadhi ya nadharia hizo hutia ndani mbalamwezi, nguvu za uvutano, nguvu za sumaku za dunia, na sumaku-umeme.

[Picha katika ukurasa wa 19]

Mungu wa kike Selene, aliabudiwa na Wagiriki na Waroma wa kale akiwa mfano wa mwezi

[Hisani]

Musei Capitolini, Roma