Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Akina Baba Wanaotoroka Wajibu—Je, Kweli Waweza Kutoroka?

Akina Baba Wanaotoroka Wajibu—Je, Kweli Waweza Kutoroka?

Vijana Huuliza . . .

Akina Baba Wanaotoroka Wajibu—Je, Kweli Waweza Kutoroka?

“Aliposema, ‘Nitazaa mtoto wako,’ nilishtuka. Ni nani atakayemtunza mtoto huyo? Sikuwa tayari kutunza familia. Nilihisi kana kwamba ningetoroka.”—Jim. *

“KILA mwaka,” yasema ripoti moja kutoka Taasisi ya Alan Guttmacher, “takriban wanawake matineja milioni 1 . . . hupata mimba.” “Asilimia [ipatayo] 78 ya watoto wanaozaliwa na matineja, huzaliwa nje ya ndoa.”

Zamani, iliwabidi wanaume watwae daraka la watoto waliowazaa. Lakini kama kisemavyo kitabu Teenage Fathers, “mimba nje ya ndoa haiaibishi na kutweza tena kama ilivyokuwa wakati fulani.” Vijana wengine katika jumuiya fulani-fulani hata huona kuzaa mtoto kuwa hadhi ya kijamii! Hata hivyo, ni wanaume wachanga wachache wanaojifunga wajibu wa muda mrefu kwa watoto wanaozaa. Wengi hutoroka hatimaye. *

Lakini je, mwanamume kijana aweza kukwepa kabisa matokeo ya mwenendo usio wa adili? Sivyo, kulingana na Biblia. Huonya hivi: “Msiongozwe vibaya: Mungu si wa kudhihakiwa. Kwa maana lolote lile mtu analopanda, hilo atavuna pia.” (Wagalatia 6:7) Kama tutakavyoona, ukosefu wa adili katika ngono mara nyingi huleta matokeo ya kudumu kwa wavulana na wasichana pia. Vijana wanaweza kuepuka matokeo hayo kwa kutii shauri la Biblia lililo wazi la kuepuka ukosefu wa adili katika ngono.

Kutoroka—Si Rahisi

Ili kumtunza mtoto lazima udhabihu sana wakati, fedha, na uhuru. Kitabu Young Unwed Fathers chasema: “Wanaume fulani wachanga hawapendi ‘kumtunza mtu mwingine,’ ikiwa wataishiwa na fedha.” Hata hivyo, wengine hupata hasara kubwa kwa sababu ya uchoyo wao. Kwa mfano, mahakama na watunga-sheria katika nchi nyingi wamekuwa wakiwashuku wanaume wanaoshindwa kuwategemeza watoto wao. Inapothibitishwa kisheria ni nani aliye baba, akina baba wachanga waweza kulazimishwa walipie gharama kwa miaka mingi itakayofuata—ikiwa hatua inayofaa. Vijana wengi hulazimika kuacha shule au kufanya kazi ya mshahara mdogo ili kutimiza wajibu huo. “Mvulana akiwa mzazi akiwa na umri mchanga sana,” chasema kitabu School-Age Pregnancy and Parenthood, “basi hupata elimu rasmi kidogo zaidi.” Mtu akikosa kulipa gharama za kutunza mtoto, madeni makubwa sana yaweza kurundamana.

Bila shaka, si wanaume wote wachanga walio na mtazamo sugu kwa watoto wao. Wengi huanza wakiwa na makusudio mema. Kulingana na uchunguzi mmoja, asilimia 75 ya akina baba walio matineja walitembelea mtoto wao alipokuwa hospitalini. Lakini, baada ya muda mfupi baba wengi wachanga hulemewa na madaraka ya kumtunza mtoto.

Wengi huona kwamba hawana stadi wala uzoefu ili kupata kazi inayofaa. Wanapoaibika kwa kushindwa kuandaa utegemezo wa kifedha, baada ya muda wanakwepa wajibu wao. Hata hivyo, maumivu makali yenye majuto yaweza kumpata kijana mara kwa mara kwa miaka mingi itakayofuata. Baba mmoja mchanga akiri hivi: “Nyakati nyingine mimi hujiuliza mtoto wangu amepatwa na nini. . . . Sifurahii [kumwacha], lakini sasa nimempoteza. Labda atakutana nami siku moja.”

Madhara Yaletwayo kwa Watoto

Huenda pia akina baba wanaotoroka wajibu wakahitaji kukabiliana na aibu kubwa sana—aibu ya kumdhuru mtoto wako mwenyewe. Kwani, Biblia huonyesha kwamba mtoto ahitaji kuwa na mama na baba. (Kutoka 20:12; Mithali 1:8, 9) Mwanamume amwachapo mtoto wake, anamletea mtoto huyo matatizo chungu nzima. Ripoti moja ya Wizara ya Afya na Huduma za Jamii ya Marekani yasema hivi: “Watoto wachanga kutoka familia zilizo na mama peke yake hupata maksi za chini katika mtihani wa lugha na hesabu. Wanapofikisha umri wa kati ya miaka 7 hadi 10, watoto waliolelewa na mzazi mmoja hupata maksi za chini, hupatwa na matatizo zaidi ya kitabia, na hupatwa sana na magonjwa ya kudumu na kasoro za kiakili. Miongoni mwa wabalehe na vijana, kulelewa katika familia yenye mama peke yake kwahusishwa na hatari kubwa ya kuzaa mtoto ukiwa tineja, kuacha shule ya sekondari, kufungwa jela, na kufukuzwa shuleni na kazini.”

Gazeti Atlantic Monthly lamalizia hivi: “Kwa sababu ya ushuhuda unaoongezeka wa kijamii na kisayansi, watoto wanaotoka katika familia zilizovurugwa na talaka na waliozaliwa nje ya ndoa hufanya vibaya katika mambo mbalimbali yahusuyo hali njema kuliko watoto wanaotoka kwa familia zenye wazazi wawili. Uwezekano wa watoto kutoka familia yenye mzazi mmoja kuwa maskini ni mara sita zaidi ya watoto kutoka familia yenye wazazi wote. Pia huelekea kubaki katika hali ya umaskini.”

Kumbuka kwamba hatari hizi zategemea takwimu za vikundi na si lazima ziwe zahusu mtu mmoja-mmoja. Watoto wengi hatimaye huwa wazuri, watu wazima wenye usawaziko licha ya hali mbaya za kimalezi za familia. Ijapokuwa hivyo, mwanamume kijana aliyeacha mtoto wake aweza kusumbuliwa sana na hatia. “Nasikitika kwamba nimevuruga maisha yake kabisa,” asema baba mmoja asiyefunga ndoa.—Teenage Fathers.

Ugumu wa Kuandaa Utegemezo

Si baba wote wachanga hutoroka wajibu wao. Kwa haki wanaume fulani wachanga hutambua wajibu wa kiadili walio nao kwa watoto wao na hutaka kikweli kusaidia kuwalea. Hata hivyo, mara nyingi, wanaonyesha hivyo kwa maneno tu. Kwanza, baba asiyefunga ndoa aweza kuwa na haki chache kisheria, akimwacha msichana na wazazi wake waamue atawasiliana na mtoto wake kwa kadiri gani. “Unang’ang’ana daima ili uwe na mamlaka ya kufanya maamuzi kumhusu mtoto,” asema Jim aliyenukuliwa mwanzoni. Hivyo kwaweza kuwa na maamuzi ambayo baba mchanga atayapinga kwa ukali, kama vile kuasilishwa—au hata kutoa mimba. * “Naona ugumu kuwaruhusu wampe mtu yeyote mtoto huyo,” aomboleza baba mmoja mchanga, “lakini nafikiri sina uchaguzi mwingine.”

Wanaume fulani wachanga hujitolea kuoa mama ya mtoto wao. * Kwa wazi, ndoa ingemwondolea msichana aibu kwa kiasi fulani na kumwezesha mtoto alelewe na wazazi wawili. Huenda hata ikawa kwamba licha ya mwenendo wao usiofaa, wenzi hao wachanga wanapendana kikweli. Hata hivyo, haimaanishi kwamba mvulana amekomaa kiakili na kihisia-moyo ili kuwa mume na baba eti kwa sababu tu aweza kuzaa. Wala haimaanishi kwamba anaweza kutegemeza mke na mtoto kifedha. Uchunguzi waonyesha kwamba ndoa zinazofungwa kwa sababu ya mimba hudumu kwa muda mfupi. Kwa hiyo, sikuzote si jambo la busara kukimbilia ndoa.

Wanaume wengi wachanga hujitoa kutegemeza watoto wao kifedha. Kama ilivyotajwa mapema, lazima baba mchanga awe ameazimia kikweli ili aendelee kutoa utegemezo kwa muda mrefu—labda miaka 18 au zaidi! Lakini msaada wa kifedha unapotolewa kwa kuendelea, unaweza kuzuia mama na mtoto huyo wasiishi maisha ya umaskini.

Vipi juu ya kushiriki kihalisi kulea mtoto? Kwaweza kuwa na ugumu pia. Nyakati fulani wazazi wa wenzi hao huhofu kwamba huenda kukawa na uhusiano zaidi wa kingono na hivyo kujaribu kuuepusha kwa kukataza wenzi hao wasiwe wakitembeleana. Huenda msichana mwenyewe akaamua kwamba hataki mtoto wake “awe na uhusiano wa karibu” na mtu ambaye si mume wake. Kwa vyovyote vile, ikiwa baba aruhusiwa kuonana na mtoto wake kwa ukawaida, litakuwa jambo la busara familia kuhakikisha kwamba kuna mtu anayesimamia ziara hizo, ili kuzuia mwenendo usiofaa usiendelee zaidi.

Kwa sababu ya kutamani kuwa na uhusiano wa karibu na watoto wao, baba fulani wasiofunga ndoa wamejifunza kufanya kazi fulani za wazazi, kama vile kuosha, kulisha, au kusomea watoto wao. Mwanamume kijana anayethamini viwango vya Biblia huenda hata akajaribu kufunza mtoto wake baadhi ya kanuni za Neno la Mungu. (Waefeso 6:4) Lakini ingawa kupata uangalifu fulani wenye upendo kutoka kwa baba bila shaka ni bora kwa mtoto kuliko kukosa wowote, hakulingani na kuwa na baba mnayeishi naye. Na iwapo mama ya mtoto huyo atapata kuolewa, huenda baba mchanga akakosa jambo la kufanya ila kutazama tu mwanamume mwingine akichukua daraka la kulea mtoto wake.

Kwa hiyo ni wazi kwamba kuzaa mtoto nje ya ndoa huongoza kwenye taabu nyingi—kwa wazazi na mtoto pia. Mbali na mahangaiko ya kiutendaji, kuna hatari ya kupoteza upendeleo wa Yehova Mungu, anayelaumu ngono haramu. (1 Wathesalonike 4:3) Ingawa yawezekana kufanya yote uwezayo ili kukabiliana na hali isiyofaa kama vile mimba ya utineja, yapasa iwe wazi kwamba hatua inayofaa ni kujiepusha na mwenendo usio wa adili tokea mwanzo. Baba mmoja mchanga akiri hivi: “Unapozaa mtoto nje ya ndoa, maisha yako hubadilika daima dawamu.” Kwa kweli, huenda baba mchanga akalazimika kuishi na matokeo ya kosa lake muda wote wa maisha yake. (Wagalatia 6:8) Kwa mara nyingine tena shauri la Biblia limethibitika kuwa la hekima linaposema: “Ukimbieni uasherati.”—1 Wakorintho 6:18.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Baadhi ya majina yamebadilishwa.

^ fu. 5 Ona makala “Vijana Huuliza . . . Kuzaa Watoto—Je, Humfanya Mtu Awe Mwanamume?” katika toleo la Amkeni!, Aprili 22, 2000. Kwa mazungumzo kuhusu athari za kuwa mama zinazowapata wanawake wachanga, ona makala “Vijana Huuliza . . . “Umama wa Bila Ndoa—Je, Ungeweza Kunipata Mimi?” katika toleo la Machi 8, 1987.

^ fu. 16 Ona makala “Vijana Huuliza . . . Je, Utoaji-Mimba—Ndio Suluhisho?” katika toleo la Amkeni! la Machi 8, 1995.

^ fu. 17 Sheria ya Kimusa ilitaka mwanamume aliyemshawishi bikira amwoe. (Kumbukumbu la Torati 22:28, 29) Hata hivyo, ndoa ingeweza kuepukwa, kwa kuwa baba ya msichana angeweza kukataa. (Kutoka 22:16, 17) Ijapokuwa Wakristo leo hawako chini ya Sheria hiyo, hiyo hukazia uzito wa dhambi ya kufanya ngono kabla ya ndoa.—Ona “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika toleo la Mnara wa Mlinzi, Novemba 15, 1989.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Ni jambo linalonufaisha kujiepusha na mwenendo usio wa adili tokea mwanzo