Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maonyesho Yenye Kuvutia ya Meli za Matanga

Maonyesho Yenye Kuvutia ya Meli za Matanga

Maonyesho Yenye Kuvutia ya Meli za Matanga

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UFARANSA

MELI ZA MATANGA ZILIZO MARIDADI ZAIDI DUNIANI ZILIKUSANYIKA ROUEN, KASKAZINI MWA UFARANSA, KATIKA JULAI 1999 KWA AJILI YA SHEREHE KUU YA MELI ZA KARNE. MELI 30 MASHUHURI ZENYE MATANGA ZILITIA NANGA KWENYE MAGATI YENYE UMBALI WA KILOMETA SABA YALIYOTAYARISHWA KWA AJILI YA SHEREHE HIYO.

Tukio hilo lilitangazwa kuwa “maonyesho ya ubaharia ya milenia.” Tamasha za muziki, fataki, tamasha za ubaharia, na maonyesho ya michoro na picha za ubaharia zote zilikuwa kwenye ratiba ya sherehe hiyo.

Meli hizo ziliwasili kwa fahari Ijumaa, Julai 9. Siku kumi zilizofuata, mamilioni ya wageni kutoka Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya walifurika magatini.

Baadhi ya meli hizo—kama vile Dar Młodziezy (Poland), Khersones (Ukrainia), Statsraad Lehmkuhl (Norway), na Libertad (Argentina)—ni kubwa kupindukia zikiwa na urefu wa meta 100, huku mlingoti mrefu zaidi ukifikia kimo cha meta 50 juu ya bahari.

Meli ndefu zaidi kutoka nchi 16 zilikuwapo, kutia ndani Ireland, Ubelgiji, Ujerumani, Ureno, Uruguay, Urusi, na Venezuela. Uholanzi ikiwa na meli sita, ndiyo iliyokuwa na meli nyingi zaidi. Miongoni mwake ni Europa meli maridadi yenye milingoti mitatu na Oosterschelde ya kale, meli yenye milingoti mitatu na matanga nchani iliyoanza kuabiri mnamo 1918, ambayo ilisafirisha kuni, heringi waliohifadhiwa kwa chumvi, udongo wa mfinyanzi, nafaka, nyasi kavu, na matunda kati ya Afrika, Mediterania, na kaskazini mwa Ulaya.

Sherehe hizo za Meli zilitokeza fursa bora ya kufurahisha wageni. Mbao za kuingilia melini ziliondolewa, na kila mtu angeweza kutembea apendavyo kwenye sitaha, bila malipo.

Baadhi ya meli hizo zimewahi kutumiwa kwenye sinema. Kwa mfano, meli ya Norway Christian Radich ilitimiza fungu muhimu katika filamu ya Windjammer ya mwaka wa 1958. Meli ya kale ya mbao iitwayo Kaskelot (“nyangumi-shahawa” katika Kidenmark) ilitumiwa katika sinema kadhaa, kutia ndani filamu ya Kifaransa ya Beaumarchais l’insolent na sinema iliyotungwa upya ya Treasure Island.

Meli ya Iskra kutoka Poland yenye milingoti mitatu ni ya pekee kwa sababu milingoti yake mitatu ina matanga tofauti. Mlingoti wa tanga la mbele ni wa mraba, mlingoti mkuu ni tenge, na mlingoti wa tanga la galme ni wa pembe tatu.

Baadhi ya meli za kale zilizokuwa Rouen zilikuwa zimeibuliwa baharini. Kwa mfano, mashabiki wenye kuazimia waliibua meli maridadi ya Capitán Miranda ya Uruguay na kuirekebisha. Meli ya Étoile Molène, iliyozama mapema miaka ya 1980 katika bandari ya Douarnenez, Brittany, iliibuliwa na kuanza tena kuabiri kwa sababu ya kutunzwa vizuri.

Wakati wa sherehe hiyo, shirika moja la wahandisi wapya wa redio liliamua kuunganisha mawasiliano ya redio kati ya meli ya Mir na kituo cha Urusi kinachozunguka angani cha Mir. Hatimaye, saa 4:27 usiku wa Julai 17, kulikuwa na mawasiliano kati ya ile meli yenye milingoti mitatu na “chombo cha angani chenye jina sawa” na meli hiyo. Kapteni Zorokhov aliweza kuzungumza na Kamanda Afanassiev akiwa kwenye kituo hicho cha angani kilicho umbali wa kilometa zipatazo 350.

Sherehe hiyo ya Meli ilifikia upeo Jumapili, Julai 18, kukiwa na msafara wa meli kwenye Mto Seine, kuanzia Rouen hadi baharini. Meli hizo zilipokuwa zikipita karibu na vijiji, nyumba za watawa, na ngome za kale za Wanorman, mamia ya maelfu ya watu walisimama ufuoni kwa umbali wa kilometa 120 na kuwapungia mikono mabaharia.

Baadaye, meli hizo maridadi za matanga zilienda kushiriki kwenye mashindano ya meli, filamu, au maonyesho mengine yenye kuvutia katika bandari ya mbali. Shughuli za kawaida zilirejea kwenye magati. Lakini wakazi wa Rouen watakumbuka kwamba angalau kwa siku kumi, kulikuwa na mkusanyiko wa meli kutoka kotekote ulimwenguni katika mji huo.

[Ramani katika ukurasa wa 10]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Honfleur

Seine

Rouen

[Hisani]

Maps on pages 10, 17, and 31: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Meli ya “Cuauhtemoc” yenye milingoti mitatu kutoka Mexico

[Picha katika ukurasa wa 10]

Meli yenye kuvutia mno ya “Étoile Molène” ilikuwa imeibuliwa kutoka baharini

[Hisani]

© GAUTHIER MARINES/ Photo Jo Gauthier

[Picha katika ukurasa wa 10]

Mchoro wa mwaka wa 1855 wa bandari ya Rouen, wakati meli zenye matanga zilipoabiri kwenye Mto Seine

[Hisani]

Charles-Louis Mozin, Port de Rouen, vue générale © Rouen, Musée des Beaux-Arts

[Picha katika kurasa za 10, 11]

Rouen, “mji wa minara mia moja,” ukawa msitu wa milingoti

[Hisani]

© GAUTHIER MARINES/ Photo Jo Gauthier