Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

El Niño Ni Nini?

El Niño Ni Nini?

El Niño Ni Nini?

Mto Apurímac ulio karibu na Lima, Peru, ambao kwa kawaida huwa umekauka, ulipofagilia mbali karibu kila kitu alichomiliki Carmen, aliomboleza hivi: “Wengi wetu wamepatwa na jambo hilo, wengi sana. Si mimi peke yangu.” Mbali zaidi kaskazini, mvua za majira ya baridi ziligeuza kwa muda sehemu fulani ya pwani ya Jangwa la Sechura kuwa ziwa la pili kwa ukubwa katika Peru, lenye ukubwa wa takriban kilometa 5,000 za mraba. Kwingineko ulimwenguni pote, mafuriko yaliyovunja rekodi, tufani kuu, na ukame mkali zilisababisha njaa kuu, magonjwa ya kuambukiza, mioto ya mwituni, na kuharibiwa kwa mazao, mali, na mazingira. Ni nini kilichosababisha yote hayo? Wengi hulaumu El Niño, ambayo ilianza kwenye Bahari ya Pasifiki ya kitropiki, au ya ikweta, kuelekea mwisho wa mwaka wa 1997 na kuchukua muda wa miezi minane hivi.

El Niño ni nini hasa? Huanzaje? Kwa nini athari zake huenea kwa mapana? Je, yawezekana kutabiri kwa usahihi wakati itakapotukia tena, na labda kupunguza hasara ya uhai na mali?

Huanza Maji Yawapo Moto

“Kwa usahihi, El Niño ni mkondo wa maji moto ambao hutokea karibu na pwani ya Peru kila baada ya miaka miwili hadi saba,” lasema gazeti la Newsweek. Kwa zaidi ya miaka mia moja, mabaharia walio kandokando ya pwani ya Peru wamegundua hali hiyo ya joto. Kwa kuwa mikondo hiyo moto kwa kawaida hutukia karibu na wakati wa Krismasi, iliitwa El Niño, neno la Kihispania kwa kitoto kichanga Yesu.

Mvua huongezeka Peru maji yanapokuwa moto karibu na pwani ya nchi hiyo. Mvua hufanya majangwa yachanue maua na mifugo inawiri. Mvua inapokuwa nyingi, huleta mafuriko pia kwenye eneo hilo. Isitoshe, tabaka ya juu ya maji moto ya bahari huzuia maji yaliyo baridi zaidi ya chini yaliyojaa virutubishi yasibubujike. Kwa sababu hiyo, viumbe wengi wa baharini na hata ndege wengine huhama wakitafuta chakula. Hatimaye maeneo mengine yaliyo mbali na pwani ya Peru hupatwa na matokeo ya El Niño. *

Husababishwa na Upepo na Maji

Ni nini husababisha ongezeko lisilo la kawaida la halijoto ya bahari karibu na pwani ya Peru? Ili kuelewa hilo, kwanza fikiria mzunguko mkubwa unaojulikana kuwa Walker Circulation, ulio katika angahewa kati ya Pasifiki ya kitropiki ya mashariki na magharibi. * Jua linapopasha joto maji mengi upande wa magharibi, karibu na Indonesia na Australia, hewa yenye joto na unyevu hupaa kwenye angahewa, na kusababisha kanieneo ya chini karibu na maji. Hewa inayopaa hupoa na kupoteza unyevu, huku ikileta mvua kwenye eneo hilo. Hewa kavu husukumwa na upepo upande wa mashariki katika angahewa la juu zaidi. Inaposafiri kuelekea mashariki, hewa hiyo huwa baridi na nzito zaidi na huanza kushuka inapofika Peru na Ekuado. Kama tokeo kunakuwa na kanieneo ya juu karibu na bahari. Na, kwenye miinuko isiyo mirefu, mikondo ya hewa inayoitwa pepo kali zinazovuma daima huelekea nyuma upande wa magharibi mwa Indonesia, hivyo ikikamilisha mzunguko huo.

Pepo zinazovuma daima huathirije halijoto ya Pasifiki ya kitropiki? “Kwa kawaida pepo hizi huwa kama upepo mwanana ndani ya dimbwi ndogo mno,” lasema gazeti la Newsweek, “zikisukuma maji moto hadi kwenye Pasifiki ya magharibi hivi kwamba usawa wa bahari hupanda kwa sentimeta 60 na joto kwa nyuzi 8 Selsiasi katika nchi kama vile, Ekuado.” Katika Pasifiki ya mashariki, maji baridi kutoka chini yaliyojaa virutubishi hububujika, na kusababisha viumbe wa baharini wasitawi. Hivyo, katika miaka ya kawaida isiyo na El Niño, halijoto ya bahari huwa baridi zaidi upande wa mashariki kuliko upande wa magharibi.

Ni mabadiliko gani ya angahewa ambayo hutokeza El Niño? “Kwa sababu ambazo hata wanasayansi wenyewe hawazielewi,” lasema gazeti la National Geographic, “kila baada ya miaka michache pepo kali zinazovuma daima hupungua au hata hutoweka.” Pepo hizo zinapopungua, maji moto yaliyojikusanya karibu na Indonesia hurudi upande wa mashariki, na kuongeza halijoto ya bahari huko Peru na sehemu nyingine katika mashariki. Halafu mfumo wa angahewa huathiriwa na msogeo huo. “Bahari ya Pasifiki ya kitropiki iliyo upande wa mashariki inapopashwa joto, hudhoofisha mzunguko wa Walker Circulation na kusababisha kanda la joto lenye mvua nyingi lielekee mashariki, kutoka magharibi hadi kwenye Pasifiki ya kitropiki ya kati na mashariki,” chasema kichapo kimoja cha marejezo. Hivyo, mifumo ya halihewa kandokando ya Pasifiki ya ikweta yote huathiriwa.

Kama Jabali Katika Kijito

Pia El Niño inaweza kubadili mifumo ya tabia ya nchi iliyo mbali sana na mikondo ya maji ya Pasifiki ya kitropiki. Jinsi gani? Kwa kutumia mfumo wa kuzunguka wa angahewa. Matokeo yanayoenea mbali ya kuvurugwa kwa mzunguko wa angahewa yaweza kufananishwa na jinsi jabali moja lililo katikati ya kijito liwezavyo kutokeza mawimbi katika kijito chote. Mawingu mazito ya mvua yanayopaa juu ya maji ya bahari ya tropiki yenye joto hutokeza kizuizi kama jabali kwenye angahewa, ambacho huathiri mifumo ya halihewa iliyoko umbali wa maelfu ya kilometa.

Kwenye latitudo za juu, El Niño huimarisha na kuchukua mahali pa mikondo ya upepo inayosafiri kwa kasi kuelekea mashariki inayoitwa mikondo mirefu ya pepo zinazovuma kwa kasi. Mikondo mirefu ya pepo huelekeza dhoruba nyingi kwenye latitudo hizi. Kuimarika na kubadilika kwa mikondo ya pepo zinazovuma kwa kasi kwaweza pia kuongezeka au kudhibiti hali za hewa za kimsimu. Kwa mfano, majira ya baridi kali ya El Niño kwa kawaida huwa afadhali zaidi katika sehemu za kaskazini mwa Marekani, ilhali huwa na mvua nyingi na baridi kali zaidi katika majimbo fulani ya kusini.

Yaweza Kutabiriwa Jinsi Gani?

Athari za dhoruba mojamoja zaweza kutabiriwa tu siku kadhaa kimbele. Je, ni namna moja na jitihada za kutabiri El Niño? La. Badala ya kuhusisha matukio ya muda mfupi ya halihewa, El Niño huhusisha hali zisizo za kawaida za tabia ya nchi katika maeneo makubwa kwa miezi kadhaa kwa wakati mmoja. Na watafiti wa tabia ya nchi wamefanikiwa kwa kiasi fulani kutabiri El Niño.

Mathalani, utabiri wa El Niño ya mwaka wa 1997 hadi 1998 ulitolewa Mei 1997—miezi sita hivi kabla ya kutokea. Kuna boya 70 zilizotia nanga ambazo zimeenea katika Pasifiki ya kitropiki nazo hupima hali ya upepo kwenye bahari na halijoto ya bahari kufikia kina cha meta 500. Habari hizi zinapotiwa ndani ya kompyuta za tabia ya nchi, husaidia katika utabiri wa hali ya hewa.

Maonyo ya mapema yahusuyo El Niño kwa kweli yanaweza kusaidia watu wajitayarishie mabadiliko yanayotarajiwa. Kwa mfano, tangu 1983, utabiri wa El Niño katika Peru umewatia moyo wakulima wengi wafuge ng’ombe na kukuza mazao yanayositawi kwenye mvua nyingi, nao wavuvi wameacha kuvua samaki na kuanza kuvua uduvi ambao hupatikana kwenye maji yaliyo moto zaidi. Naam, utabiri sahihi pamoja na matayarisho ya mapema yanaweza kupunguza sana hasara ya vifo na ya kiuchumi inayoletwa na El Niño.

Utafiti wa kisayansi kuhusu mambo yanayodhibiti tabia ya nchi ya dunia huthibitisha usahihi wa maneno yaliyopuliziwa yaliyorekodiwa na Mfalme Solomoni wa Israeli ya kale yapata miaka 3,000 iliyopita. Aliandika hivi: “Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake.” (Mhubiri 1:6) Mwanadamu wa kisasa amejifunza mengi kuhusu mifumo ya halihewa kwa kuchunguza mikondo ya upepo na ya bahari. Na tunufaike na ujuzi huo kwa kusikiza maonyo yanayohusu matukio kama vile El Niño.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Kinyume cha hilo, La Niña (Neno la Kihispania kwa “msichana mdogo”) ni kupozwa kwa halijoto ya maji karibu na pwani ya magharibi mwa Amerika Kusini. La Niña pia huathiri sana halihewa.

^ fu. 8 Mzunguko huo ulipewa jina la Bwana Gilbert Walker, mwanasayansi Mwingereza aliyechunguza mfumo huo katika miaka ya 1920.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

HISTORIA YA UHARIBIFU WA EL NIÑO

1525: Historia ya mapema zaidi ya kuzuka kwa El Niño huko Peru.

1789-1793: El Niño ilisababisha zaidi ya vifo 600,000 katika India na kusababisha njaa kuu kusini mwa Afrika.

1982-1983: Tukio hili ndilo lililosababisha vifo zaidi ya 2,000 na hasara ya mali yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 13 za Marekani, hasa katika maeneo ya kitropiki.

1990-1995: Matukio matatu yaliungana kwa kufuatana na kufanyiza mojawapo ya visa virefu zaidi vya El Niño vilivyopata kurekodiwa.

1997-1998: Licha ya utabiri wa kwanza wa mkoa uliofanikiwa zaidi kuhusu mafuriko na ukame wa El Niño, karibu watu 2,100 walikufa, na kukatokea hasara ya dola bilioni 33 za Marekani ulimwenguni pote.

[Michoro/Ramani katika ukurasa wa 24, 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

KAWAIDA

Mfumo wa Walker Circulation

Pepo kali zenye nguvu zinazovuma daima

Maji moto ya bahari

Maji baridi ya bahari

EL NIÑO

Mkondo wa pepo zinazovuma kwa kasi wabadili njia

Pepo kali zinazovuma daima zilizo hafifu

Maji moto yaelekea mashariki

Joto zaidi au ukame usio wa kawaida

Baridi au mvua nyingi zaidi isivyo kawaida

[Michoro/Picha katika ukurasa wa 26]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

EL NIÑO

Rangi nyekundu kwenye tufe lililo juu zawakilisha halijoto ya maji iliyo na joto zaidi isivyo kawaida

KAWAIDA

Maji moto yakusanyika Pasifiki magharibi, yakisababisha maji yenye virutubishi yaliyo baridi zaidi yatokee mashariki

EL NIÑO

Pepo kali zinazovuma daima ambazo ni hafifu zasababisha maji moto yaelekee tena mashariki, zikizuia maji baridi zaidi yasibubujike

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

PERU

Jangwa la Sechura lililofurika

MEXICO

Kimbunga Linda

CALIFORNIA

Maporomoko ya matope

[Hisani]

Ukurasa wa 24-25 kushoto hadi kulia: Fotografía por Beatrice Velarde; Image produced by Laboratory for Atmospheres, NASA Goddard Space Flight Center; FEMA photo by Dave Gatley