Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Noah Alienda Pamoja Na Mungu—Jinsi Vidio Hiyo Ilivyotayarishwa

Noah Alienda Pamoja Na Mungu—Jinsi Vidio Hiyo Ilivyotayarishwa

Noah Alienda Pamoja Na Mungu—Jinsi Vidio Hiyo Ilivyotayarishwa

“HUAMKA asubuhi akizungumza juu yake. Huitazama mara tatu au nne kwa siku na mara nyingine tena kabla hajaenda kulala.” Mama huyo wa California anazungumza juu ya nani? Mwana wake mwenye umri wa miaka miwili na jinsi anavyopenda ile vidio ya Noah—He Walked With God. * Aongezea hivi: “Anapocheza huko nje, huzungumza kuhusu kujenga safina ya kuokoa uhai, akiwa na nyundo yake mkononi.”

Mama mwingine aliandika hivi: “Lazima nitoe shukrani nyingi sana kwa ajili ya jitihada zote, wakati, na upendo uliohusika katika kutayarisha vidio ya Noah. Nina mtoto mwenye umri wa miaka mitatu ambaye amekariri karibu vidio nzima, kutia ndani mapambo ya sauti! Ndiyo vidio anayoipenda zaidi, naye huomba kuiona kila siku, mara mbili au tatu kwa siku.”

Msichana mmoja mdogo, Danielle, aliandika hivi: “Naipenda, na nataka kufuata mambo aliyofanya Noa. Natumaini mtatayarisha vidio nyingine zaidi kwa ajili ya watoto.”

Bila shaka, inachukua muda kutayarisha vidio za Biblia. Kwa nini huwa hivyo?

Vidio ya Noah Ilitayarishwaje?

Muda mrefu kabla picha zozote za maonyesho hazijatayarishwa au kuchorwa, mwandishi wa mswada alitayarisha hadithi inayotegemea simulizi la Biblia. Hatimaye hiyo ingekuwa mfuatano wa maonyesho na kisha mswada wa mchezo wa kuigiza. Mfuatano wa maonyesho ni mfululizo wa michoro midogo, inayosaidia wasanii kuanzisha na kubuni picha za maonyesho ya hadithi. Watu kadhaa, kutia ndani wasanii, walizungumzia jinsi historia ya Noa ingeweza kuelezwa—ni sehemu zipi ambazo waigizaji wangetumiwa na ni zipi ambazo zingewakilishwa na picha. Mifuatano ya picha za maonyesho zilizoigizwa husaidia kukazia uhalisi wa simulizi katika akili ya mtoto. Huonyesha kwamba Biblia huzungumza juu ya watu halisi waliomtumikia Yehova maelfu ya miaka iliyopita. Hatua ya pili ya utayarishaji ni gani?

Waigizaji walichaguliwa kuwakilisha Noa na familia yake. Mavazi yao yalishonwa, na rangi ambazo zingetumiwa kwa kila onyesho zikachaguliwa. Hayo yote yalikuwa ya lazima kwa sababu wasanii hawangechora Noa na mke wake na wana wake na binti-wakwe zake kabla hawajajua waigizaji watakuwa na sura gani wanapovalia mavazi yao. Rangi zilipasa kupatana na maonyesho yanayoonyesha maisha halisi. Lakini mandhari hayo yangetayarishwa wapi?

Denmark ilichaguliwa kwa sababu ofisi ya tawi ya Watch Tower Society katika nchi hiyo ilikuwa na wajenzi stadi wa vitu vinavyotumiwa kwenye michezo ya kuigiza na kulikuwa na nafasi ya kutosha kwa ajili ya maonyesho yaliyohitaji kuigizwa ndani ya nyumba. Kikundi cha wapiga-picha walisafiri kutoka Idara ya Huduma za Sauti na Vidio ya Kituo cha Elimu cha Watchtower Patterson, New York, ili kupiga picha, ambao walitia ndani wafanyakazi kutoka Denmark. Hadithi hiyo imetolewa kwa njia ya simulizi. Jambo hilo limefanya iwe rahisi zaidi kutokeza programu hiyo katika lugha nyingine kwa sababu haihusishi hatua ngumu ya kunakili katika lugha nyingine, yaani kuingiza mazungumzo yaliyotafsiriwa na kupatanishwa. Lakini kazi ngumu ya sanaa ilitayarishwaje?

Sanaa na Kamera ya Pekee

Wasanii walitayarisha mamia ya picha zilizochorwa kwa rangi ya maji zenye msingi wa mfuatano wa maonyesho uliokuwa umetayarishwa na kikundi chenye ubunifu. Picha hizo hazikulazimika kuwa za mraba au za mstatili. Nyakati nyingine zilikuwa zimepindika au zilikuwa na umbo la yai, ikitegemea pembe ya kamera ambayo ingetumiwa. Hakuna picha iliyokuwa na ukubwa wa sentimeta 56 kwa 76, na nyingi zilikuwa na udogo wa sentimeta 28 kwa 38.

Kamera ya pekee inayodhibiti mwendo ilihitajiwa ili kupiga picha hizo. Ili kuwe na mapambo ya pande tatu, picha hizo zilipangwa kwa matabaka matatu—la mbele, la kati, na la nyuma. Kwa njia hiyo mandhari ingeweza kutokezwa katikati ya miti, katikati ya miguu ya tembo, au chochote kilichohitajiwa ili kutokeza kina. Kamera hiyo ilielekezwa na kompyuta na ingeweza kuzungushwa kwenye pande zote za mandhari au kuletwa karibu au kupelekwa mbali ili kutokeza mapambo ya sauti. Hilo hutoa wazo la kwamba mandhari inasonga, japo kwa kweli, ni kamera tu inayosonga.

Kwa kuwa Watch Tower Society haina ustadi au uwezo wa kutengeneza katuni zilizo hai, njia ya vyombo vingi vya habari ya kutumia picha za maonyesho yaliyoigizwa pamoja na picha zilizochorwa hutimiza kusudi hilo. Watoto wenye umri wa miaka 3 hadi 12, ambao vidio hii ilibuniwa kwa ajili yao, wamefurahia njia hiyo. Na vidio hiyo hutaja waziwazi masomo mengi tuwezayo kujifunza kutokana na kielelezo cha Noa. Zaidi ya hilo, maswali yaliyo kwenye kifuniko cha vidio hii husaidia wazazi wapitie mambo makuu ya hadithi hiyo pamoja na watoto wao.

Mapambo mengine ya sauti, kama vile kuongezeka kwa mvua wakati wa Furiko, yaliwezekana kwa sababu ya tekinolojia ya kompyuta. Ni rahisi kuona kwamba wakati mwingi na jitihada za ubunifu zilihusika katika kutokeza vidio ya Noah.

Kwa kuwa masimulizi ya Biblia hayabadiliki, sikuzote vidio ya Noah—He Walked With God itakuwa ya kisasa na inaweza kusaidia kufundisha kila kizazi cha vijana. Wazazi na watoto wameandika mamia ya barua za uthamini wakiomba vidio zaidi. Mtu mmoja aliandika hivi: “Nina umri wa miaka 50 na nililea watoto wangu zamani sana. Lakini nafikiri maktaba ya vidio za hadithi za Biblia ni chombo chenye thamani sana leo kwa wazazi walio na watoto wachanga.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Vidio hii ilitolewa mwaka wa 1997 na imetafsiriwa katika Kicheki, Kichina, Kidenmark, Kifaransa, Kifinland, Kigiriki, Kihispania, Kiholanzi, Kihungaria, Kiitalia, Kijapani, Kikorea, Kikroatia, Kilatvia, Kinorway, Kireno, Kiserbia, Kislovaki, Kisweden, na Kithai. Kuna mipango ya kuitafsiri katika lugha nyingine kumi.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kamera ya kudhibiti mwendo hupiga picha huku ikisogea, na kuhuisha picha hizo

[Picha katika ukurasa wa 22, 23]

Utayarishaji ulianza kwa mfuatano wa maonyesho

[Picha katika ukurasa wa 23]

Picha nyingi za maonyesho yaliyoigizwa zilitayarishwa huko Denmark

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Wasanii walichora na kupaka rangi mandhari mbalimbali 230

[Picha katika ukurasa wa 25]

Kuhariri kwa kutumia kompyuta, mapambo ya sauti, masimulizi, muziki, na sauti vilikamilisha vidio hiyo