Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Historia Mashuhuri ya Athens na Magumu Yake ya Wakati Ujao

Historia Mashuhuri ya Athens na Magumu Yake ya Wakati Ujao

Historia Mashuhuri ya Athens na Magumu Yake ya Wakati Ujao

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UGIRIKI

NDEGE inapiga kona ya mwisho kabla ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Athens. Baada ya muda wa miaka miwili, narejea tena sehemu niliyoishi kwa miongo miwili. Vitabu vya historia, vinaonyesha kwamba watu wengi huliona jiji hili kuwa chimbuko la demokrasia.

Nichunguzapo sana, nagundua kwamba mbali na historia, sanaa, na nguzo za ukumbusho, jiji kuu mashuhuri la Ugiriki lenye mchanga limesongamana watu wenye bidii na mataraja mema. Pia nagundua kwamba wakazi wake wenye urafiki na tabasamu wanajitahidi sana kusitawisha jiji lao—na hasa wakati huu kwa sababu linatayarishwa kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 2004.

Historia Mashuhuri

Athens lilijengwa mapema karne ya 20 kabla ya Kristo nalo laitwa Athena jina la mungu-mke wa Ugiriki. Bado waweza kutembea kwenye barabara alizopitia Socrates, kuzuru shule alikofundisha Aristotle, au kufurahia mchezo wa tanzia au tamthiliya ya kuchekesha kwenye majukwaa yaliyotumiwa na Sophocles na Aristophanes kuelekezea michezo yao.

Athens lilikuwa mojawapo ya majiji ya kwanza ya Ugiriki na lilishamiri sana, lilipokuwa na ufanisi, katika karne ya tano K.W.K. Wakati huo Athens la kidemokrasia lilitimiza fungu muhimu wakati Ugiriki iliposhinda Uajemi na kuwa kituo cha sanaa na fasihi cha Ugiriki. Nguzo kadhaa mashuhuri za usanifu-majengo zilijengwa pia karibu wakati huo—Parthenon iliyo maridadi ndiyo iliyokuwa mashuhuri zaidi.

Japo Waathene waliwashinda Waajemi, baadaye walisambaratishwa na mashambulizi ya adui wa kale aliye jirani yao—Sparta. Katika karne zilizofuata, jiji la Athene lilitawaliwa katika pindi mbalimbali na Makedonia, Roma, wamaliki wa Byzantine huko Constantinople, dyuki Wafranki wa Krusedi, na Waturuki. Wagiriki walipopata uhuru mnamo mwaka wa 1829, Athene lilikuwa limefifia na kuwa mji mdogo wa kimkoa wenye maelfu machache tu ya wakazi.

Hali Yake ya Sasa

Athene limesitawi haraka sana tangu mwaka wa 1834 lilipokuwa jiji kuu la Ugiriki. Sasa lina eneo la takriban kilometa 450 za mraba, hadi kwenye uwanda wa Attic. Vitongoji vyake vimetapakaa hadi kwenye miteremko ya Mlima Parnes, Pendelikón, na Hymettus. Jiji kuu lina wakazi zaidi ya milioni nne na nusu—asilimia 45 hivi ya idadi ya watu Ugiriki. Lilijengwa hasa pasipo mpango au utaratibu. Kulingana na kadirio moja, zaidi ya thuluthi ya makazi yalijengwa kinyume cha sheria, na leo ni sehemu ndogo tu ya Athens isiyofunikwa kwa saruji.

Viunga vingi vya kisasa vya Athens vimejengwa kwa usanifu-majengo wa kuta za saruji. Jiji hilo huonekana likiwa tambarare juani, kukiwa na nguzo ya kale iliyoinuka hapa na pale, yenye kufunikwa na wingu la moshi wa kijivu kutoka kwa viwanda na magari.

Sawa na miji mingine mingi ya kisasa, Athens lina ukungu wenye moshi. Ukungu huo wenye moshi—uitwao nefos na wenyeji—hupanda kiasi juu ya msitu wa antena za televisheni. Ukungu huo wenye moshi unababua nguzo za kale za ukumbusho haraka sana hivi kwamba wakati mmoja waakiolojia walifikiria kufunika Acropolis kwa kioo. Maonyo ya uchafuzi ni ya kawaida. Ukungu huo wenye moshi wa nefos unaposukumwa na halihewa kwenye milima inayozingira Athens, unaweza kuwa hatari kwa wanadamu. Wakati huo, magari ya kibinafsi hayaruhusiwi mjini, viwanda hupunguza matumizi ya fueli, wazee-wazee hushauriwa wabaki nyumbani, na Wakazi wa Athens huombwa waache magari yao nyumbani.

Wakazi wengi wa Athens hutoka mjini wakati wa miisho- juma. “Pandeni gari lenu,” asema Vassilis—mkazi mzoefu wa Athens—huku akitafuna kitumbua cha karanga chenye ladha ya asali na kikombe cha kahawa chungu kwenye mkahawa mmoja. “Baada tu ya saa chache, mtakuwa milimani au baharini.” Usemi huo wamaanisha kwamba ukiwa garini unaweza kukwama kwenye msongamano wa magari kwa saa chache kabla ya kufika mashambani.

Kusafisha na Kupanga kwa Utaratibu

Hata hivyo, usafi unakaziwa sana Athens, na kuna uthibitisho wa kutosha. Kwa mfano, magari hayaruhusiwi kwenye sehemu kubwa ya eneo la kibiashara jijini. Barabara hizo za madukani zilikuwa mojawapo ya barabara zenye msongamano mkubwa kabla hazijafungwa. Magari yalisonga kwa mwendo wa wastani wa kilometa tano kwa saa, mwendo wa matembezi ya polepole. Sasa miti iliyopandwa imechukua mahali pa milolongo mirefu ya magari, na nyimbo za ndege mahali pa mivumo ya gia zinazosuguana na milio ya skuta. Hata jiji hilo limejaribu kubadili mtindo-maisha wake wa Mediterania, kwa kuwaomba wafanyakazi waache kwenda kupumzika nyumbani wakati wa mchana—zoea ambalo lilitokeza msongamano wa magari wakati huo.

Hali katika ofisi ya naibu w a meya wa Athens, Nikos Yatrakos yaonyesha kwamba wanatarajia maendeleo. Ninapomweleza kwamba imenichukua muda wa saa mbili zenye kuchosha kufika ofisini mwake, yeye atikisa kichwa kwa huruma. “Lakini usisahau,” akazia haraka, “Michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 2004 itakuwa hapa. Tumejitolea kuboresha mji, nasi tutafanikiwa.” Constantine Bakouris, msimamizi mkuu wa michezo hiyo, asema: “Lazima [tuisimamie] ifaavyo Michezo hiyo. Lakini sisi tunaongozwa na wakati ujao. . . . Twahitaji kujenga vifaa tunavyojua vitadumu.”

Jambo la kwamba Michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 2004 itafanywa Athens limeamsha utendaji na maendeleo yasiyo na kifani. Mashine zinachimba kila mahali ili kuboresha miundo-msingi, kujenga barabara na viwanja vya michezo hiyo. Upanuzi wa kilometa 18 wa mfumo wa reli ya chini ya ardhi wakaribia kumalizika. Iwapo kazi itafuata ratiba, ndege ya kwanza itatua kwenye uwanja mpya wa ndege wa kimataifa wa Athens mnamo Machi mwaka wa 2001, uwanja ambao umeitwa kwa utani uwanja wa kisasa zaidi katika Ulaya.

Isitoshe, kufikia mwaka wa 2001, barabara kuu mpya zenye urefu wa kilometa 72 kwa ujumla zitakuwa zimekamilika. Zitaelekeza magari nje ya katikati ya mji wa Athens, na zitazidisha usafirishaji wa umma. Inatumainiwa kwamba hilo litapunguza idadi ya magari katikati ya mji kwa zaidi ya 250,000 kwa siku na kupunguza uchafuzi wa anga kwa asilimia 35. Mpango mpya wa kibiolojia wa kusafisha maji machafu ya jiji la Athens na viunga vyake utaelekea kuboresha mazingira ya bahari kuzunguka jiji kuu. Mradi mkuu wa haraka, ni kufanya Athens liwe jiji kuu jipya, lenye mfumo bora wa usafiri, bustani zaidi, na mazingira safi zaidi katika miaka michache ijayo.

Sehemu ya Athens la Kale

Licha ya majengo mapya yenye orofa za ofisi, njia pana zenye miti na chemchemi zilizofanyiwa ukarabati, maduka maridadi, na barabara zenye watu wachangamfu, wengi huliona Athens kama kijiji tu—chenye vurugu badala ya utaratibu, kilichosambaratika badala ya kuwa na mpango. Mtaa wa kale wa Athens uko katika sehemu za jiji zenye nyumba zenye roshani zilizoezekwa vigae na kufunikwa kwa fito za chuma na zenye vyungu vya maua ya jeraniamu.

Ili kufika sehemu hiyo ya Athens, nazuru Plaka, mtaa wa kale zaidi jijini, ulio pembeni mwa miteremko ya kaskazini mwa Acropolis. Huko kuna barabara nyembamba zenye kuinuka na kujipinda mfano wa mzingile, majengo yaliyoinama, maduka ya divai, paka na mbwa wanaotangatanga, vilabu vya pombe, na mikokoteni. Eneo hilo lingali na uchangamfu na msisimuko wa kale, unaovutia watalii. Vijia vya pambizoni vina meza ambazo nyakati nyingine hazina usawaziko, na viti vidogo isivyo kawaida. Wahudumu wa hotelini wenye orodha za vyakula zilizo wazi, hujaribu kuwavutia wateja.

Milio ya pikipiki huhanikiza muziki wa mpiga-kinanda. Safu ndefu za pochi mpya za ngozi huning’inia kwenye maduka ya hedaya. Majeshi ya kete za marumaru za kuchezea chesi zenye umbo la miungu ya Kigiriki zimepangwa tayari kwa pambano, makaragosi wanacheza dansi za kienyeji, na vinu vya upepo vya kauri vinazunguka. Ni wazi kwamba sehemu hii ya mji inashikilia kwa udi na uvumba mitindo ya kale.

Athens Wakati wa Usiku —Mandhari na Sauti

Kuzuru Athens bila kuchunguza utamaduni mwingi wa jiji hilo hakupendezi. Usiku wa leo, nimeamua kuzuru tamasha ya simfoni na mke wangu katika ukumbi-duara wa kale wa Kiroma wa Herod, kwenye mteremko wa kusini wa Acropolis. Kijia cha miguu kinachoelekeza kwenye ukumbi huo ni kitulivu, kina nuru hafifu na vivuli vya misonobari. Upande wa mbele wa jumba hilo wenye mawe ya ngegu wang’aa ajabu kupitia mitini. Tumekata tiketi za safu ya juu, kwa hiyo twapanda ngazi ya marumaru, kisha twaingia kwenye ukumbi-duara kupitia kwenye mlango wa Kiroma.

Twasita kwa kitambo ili kufurahia mandhari—anga jeusi la mahameli, mwezi unaokaribia kupevuka uliofunikwa na kitita cha mawingu mepesi-mepesi, na taa kubwa zenye mwanga mkali, ambazo zinang’arisha ukumbi wenye umbo la pia nusu. Mamia ya watu—waonekanao kuwa mbali na wadogo katika ukumbi huo mpana, wenye nafasi ya watu 5,000—wanatembea kwenye safu za nusu-duara za marumaru nyeupe ili kutafuta viti vyao. Viti hivyo vya mawe vingali na joto kwa sababu ya jua, mawe hayo yamevumisha mwangwi wa drama, muziki, vicheko na nderemo kwa milenia nyingi.

Usikose pia kuzuru majumba ya makumbusho mengi yaliyo jijini. Jumba mashuhuri zaidi ya yote ni National Archaeological Museum, lenye historia kamili yenye kuvutia ya usanii wa Ugiriki wa karne nyingi. Majumba mengine ya ukumbusho unayostahili kutembelea ni Jumba la Makumbusho la Cycladic Art na Jumba la Makumbusho la Byzantine. Tangu mwaka wa 1991 Jumba la Tamasha la Mégaron huko Athens—jengo maridadi la marumaru lenye vifaa bora sana vya sauti—hutumiwa mwaka wote kwa opera, dansi ya bale, na tamasha za muziki-dhati. Na, bila shaka, unaweza kufurahia muziki wa kitamaduni wa Ugiriki katika vilabu vingi vya pombe vya kienyeji.

Wakaribishwa!

Athens la kisasa lililo na historia mashuhuri lakabili mibano ya magumu ya wakati ujao. Lakini wakazi wake wamejifunza kujipatanisha wawezavyo na hali wakiwa na mwelekeo unaofaa, werevu, na philotimo—kihalisi, kupenda staha. Kwa watalii wengi, Athens ni jiji lenye kuvutia sana la kitamaduni.

[Ramani katika ukurasa wa 13]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Athens

[Picha katika ukurasa wa 14]

Parthenon, hekalu la kale la kipagani, limetumiwa kama kanisa na msikiti

[Picha katika ukurasa wa 15]

Athens lina wakazi zaidi ya milioni nne na nusu

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kilabu cha pombe huko Plaka, kitongoji cha kale zaidi katika Athens

[Hisani]

M. Burgess/H. Armstrong Roberts

[Picha katika ukurasa wa 17]

Baadhi ya maduka ya hedaya huwa na roshani

[Hisani]

H. Sutton/H. Armstrong Roberts