Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Wana Mkazo

“Karibu nusu ya Wakanada hulalamika kwamba wanapatwa na mkazo wa kiasi au mkali sana wanapojaribu kusawazisha kazi zao na maisha ya nyumbani,” laripoti gazeti la Vancouver Sun. “Idadi hiyo ni maradufu ya idadi ya mwongo mmoja uliopita.” Mbona kuna ongezeko? Uchunguzi uliotangazwa na Conference Board of Canada ulionyesha ongezeko katika asilimia ya wafanyakazi Wakanada wanaotunza washiriki wa familia. Wengi zaidi wanapata watoto baadaye maishani, na mara nyingi wanakabili ugumu “wa kutunza watoto wao na wazazi wakati uleule.” Ijapokuwa asilimia 84 ya watu waliohojiwa walihisi wameridhika na kazi zao, ripoti hiyo yaonyesha kwamba inapokuwa vigumu kusawazisha mahitaji ya nyumbani na ya kazini, “wengi hupunguza wakati wa mahitaji ya binafsi, kutia na wakati wa kulala.” Baraza la Conference Board lasema: “Hutokeza mkazo, na afya hudhoofika.”

Kuwafunza Watoto Wastahi Mamlaka

“Wazazi wa leo hawadai staha kwa ajili ya mamlaka ya wazazi hivi kwamba twaweza kuwa tunapunguza staha ya watoto wetu,” yasema ripoti moja katika gazeti la The Toronto Star. “Watoto wanapojua mipaka yao wanafahamu mambo ya kutarajia na huhisi wakiwa salama—jambo ambalo huwafanya wajistahi zaidi,” asema mtaalamu wa mazoea Ronald Morrish. “Watoto wasiotambua sheria na uwajibikaji ndio wanaokua wakijihisi wakiwa bila usalama na ujasiri.” Yeye aongezea: “Ninajua watoto wenye umri wa miaka sita wanaojiamulia wakati wa kulala. Mimi huona watoto wenye umri wa miaka mitatu wenye utovu wa nidhamu ambao wanaendekezwa na mama zao.” Watoto wanahitaji kujifunza kutii sheria za familia, na wazo la kwamba ni kawaida kukosa kushirikiana wanapokuwa wakubwa ni kosa, asema Morrish. “Sisi hutarajia watoto waongeze ujuzi wao wa kielimu hatua kwa hatua kila mwaka. Basi, kwa nini tusitarajie pia tabia ya watoto iwe bora zaidi kila mwaka?” yeye auliza. “Ikiwa huwezi kutumia mamlaka yako kumfanya mtoto anayeanza kutembea aokote mwanasesere, basi hatatii sheria ya wazazi ya kurudi nyumbani kwa wakati uliowekwa anapokuwa tineja.”

Mirekodi ya Banda la Kulia la Wanyama

Wanasayansi Wakanada wamegundua kwamba mifugo wachanga waweza kuchochewa wale chakula kwa kuwachezea mirekodi ya sauti, laripoti gazeti la New Scientist. “Tulirekodi sauti inayotokezwa na kuku anapopata mlo wa kuwapa vifaranga wake,” asema Luis Bate wa Chuo Kikuu cha Prince Edward Island. Mirekodi hiyo ilipochezwa kwa vipaza-sauti vilivyowekwa karibu na chakula, vifaranga walikula ingawa mama yao hakuwapo. Lakini ni sharti sauti hizo ziwe sawa kabisa. Bate asema: “Tulipowachezea sauti ya kuku ambaye ameangua, vifaranga walibaki tuli ingawa nilifikiri ni sauti ya kuwaitia mlo.” Lengo la wanasayansi ni kuharakisha ukuzi wa wanyama, na katika majaribio ya kwanza vifaranga walikua kwa asilimia 20 katika majuma matatu ya kwanza zaidi ya ilivyo kawaida. Katika majaribio kama hayo, vifaranga wa batamzinga na watoto wa nguruwe wangeweza kuchochewa wale mara nyingi zaidi.

Maagizo ya Dawa Yaliyo Hatari

“Mwaka uliopita watu wengi walikufa kutokana na dawa kuliko aksidenti za barabarani huko Ujerumani,” likaripoti gazeti la Stuttgarter Nachrichten. Iliripotiwa kwamba watu wapatao 25,000 walikufa mnamo mwaka wa 1998, kwa sababu ya maagizo ya dawa yenye kosa. Idadi hiyo ni mara tatu zaidi ya idadi ya watu waliokufa katika aksidenti za barabarani wakati huohuo. Yasemekana kwamba kujitibu kulichangia kidogo. Yaonekana tatizo kubwa ni madaktari wasioelimishwa na kuzoezwa kuhusu dawa na athari zake. Mtaalamu wa dawa Ingolf Cascorbi alisema kwamba kulingana na kadirio moja, “vifo 10,000 na visa 250,000 vya watu walioathiriwa vibaya sana na dawa mwaka uliopita huko Ujerumani, vingeweza kuepukwa endapo utafiti na mazoezi yangezingatiwa,” yasema ripoti hiyo.

Vivyo hivyo, gazeti la Kifaransa la Sciences et avenir laripoti kuhusu uchunguzi wa karibuni huko Ufaransa uliofunua kwamba kati ya maagizo 150,000 ya dawa yaliyotolewa kwa watu wenye umri unaozidi miaka 70, maagizo 10,700 ama yalikuwa na kosa au hayakuwa na matokeo. Agizo 1 kati ya maagizo 50 hivi yalikuwa hatari sana kwa sababu ya kuathiriwa na dawa nyingine zilizoagizwa au na hatari nyingine. Huko Ufaransa wazee-wazee hulazwa hospitalini kwa muda wa takriban siku milioni moja kila mwaka kwa sababu ya athari za dawa.