Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Maiti Zaidi Zilizotiwa Mumiani Zavumbuliwa

“Waakiolojia katika Misri wametangaza kuvumbuliwa kwa maiti zilizotiwa mumiani 200 hivi, baadhi yazo zikiwa na vizuizui vya usoni vya dhahabu, katika sehemu kubwa mno ya makaburi huko Western Desert,” yasema ripoti moja ya Habari ya BBC. Eneo hilo la maziko liko karibu na oasisi moja ya jangwani na katika jiji la Bawiti, zapata kilometa 300 kusini-magharibi ya Cairo. Kulingana na Shirika la Habari la Middle East, sehemu hiyo ya makaburi ina maiti zilizotiwa mumiani zaidi ya 10,000. Imebadilishwa jina ikawa Bonde la Maiti Zilizotiwa Mumiani. Sehemu hiyo ya makaburi yenye urefu wa kilometa kumi ni ya miaka 2,000 iliyopita, hadi kurudi nyuma kwenye enzi ya Wagiriki na Waroma. Baadhi ya maiti zilizotiwa mumiani ambazo zilichimbuliwa kufikia wakati huo zilikuwa zimefunikwa kitani au kupakwa plasta, na nyinginezo zilivikwa vizuizui vya dhahabu “vilivyo na ubuni mbalimbali wenye fahari vifuani, wa miungu ya kale ya Misri,” asema mwelekezi wa mambo ya kale Zahi Hawass.

Tauni ya Magonjwa ya Kuambukiza Yakumba Afrika

Jitihada za Shirika la Afya Ulimwenguni za kumaliza kabisa ugonjwa wa kupooza katika Afrika kufikia mwisho wa mwaka zimekosa kufua dafu, laripoti Cape Times. Vita ya Angola imesababisha ugonjwa wa kupooza ambao umefikia kuwa ugonjwa wa mlipuko nchini humo. Kulingana na Neil Cameron, mwelekezi wa kudhibiti maradhi ya kuambukiza kwenye Wizara ya Afya ya Afrika Kusini, inaweza kuchukua muda wa miaka kumi kabla ya kumaliza kabisa ugonjwa wa kupooza nchini Angola. Kwa kuongezea, majirani wa Angola, Namibia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wanajaribu kukabiliana na milipuko ya kidingapopo cha kuvuja damu kilicho kama Ebola na tauni. Pia ukoma ungali tatizo katika Kongo, Ethiopia, Msumbiji, Niger, na Nigeria. Hayo yote, kuongezea uhakika wa kwamba malaria imeenea kotekote katika bara hilo, yasababisha hangaiko kubwa kwa sababu, kama alivyosema Cameron, “mipaka si vizuizi vya maradhi.”

“Kitu Muhimu Zaidi kwa Uhai”

“Maji ni kitu cha muhimu zaidi kwa uhai, kwa sababu sehemu kubwa ya mwili imefanyizwa na uowevu,” laripoti gazeti Toronto Star. “Hata upungufu wa asilimia 20 wa maji mwilini waweza kufisha.” Maji hayadhibiti halijoto ya mwili wetu tu, bali pia “huchukua na kupeleka virutubishi na takataka kutoka kwenye viungo kupitia mkondo wa damu na mifumo ya mwili. Pia hulainisha maungo na utumbo mpana, yakiusaidia kuzuia kufunga choo.” Mtu mzima huhitaji lita mbili hadi tatu hivi za maji kila siku. Kunywa kahawa, kinywaji chenye kaboneti, au kileo kwa kweli kwaweza kuongeza uhitaji wa maji safi kwa sababu vinywaji hivyo vyaweza kuchangia katika kuishiwa maji. Kulingana na mwanalishe mmoja, kiu haipasi kuwa kikumbusha cha kunywa maji kwa sababu kufikia wakati unapohisi kiu, yaelekea tayari umeishiwa na maji. Gazeti hilo lasema kwamba “kunywa bilauri moja ya maji baada ya kila saa kwa siku, kutatosheleza uhitaji wa maji wa watu wengi zaidi.”

Kulala Kidogo Kazini

“Wafanyabiashara fulani Wakanada wanatambua manufaa za kulala kidogo kazini,” lasema gazeti Toronto Star. Waajiri wametokeza “vyumba vya kusaidia watu kuwa macho” kwa wafanyakazi wa usiku. “Vyumba hivyo vina taa zisizoangaza sana, ni baridi, kimya na vina saa zenye kengele, kochi au viti vya kulalia,” lasema Star. Lakini “ni vigumu kuondoa mawazo ya kale. Makampuni ambayo huandaa sehemu za kulala hayatangazi habari hizo.” Mary Perugini, mtaalamu wa usingizi katika Royal Ottawa Hospital’s Sleep Disorders Centre, asema hivi: “Tunafanya kazi muda wa saa nyingi zaidi, mkazo wetu wa akili ni mwingi nasi twaendelea kuuongeza. Kuweza kutumia dakika 20 kila siku kulala kungenufaisha. Bila shaka kungeongeza matokeo mengi (na) kupunguza mkazo wa akili.”

Tisho Kutokana na Mito ya Barafu Inayopungua

Barafu kubwa zaidi ulimwenguni nje ya maeneo ya nchani itapotea katika miaka 40 ikiwa kiwango cha uyeyukaji cha sasa kitaendelea, laripoti The Sunday Telegraph la London. Mchanganyiko wa halijoto inayoongezeka na latitudo ya chini ya Himaleya yatisha mito ya barafu 15,000 ya eneo hilo. Ule mto wa barafu Gangotri, ambao ni mojawapo ya vyanzo vya Mto Ganges, umepungua kwa karibu thuluthi moja ya urefu wake katika miaka 50 iliyopita. Syed Hasnain, mwanasayansi ambaye huchunguza mito ya barafu, aonya kwamba kiwango hicho cha upungufu kikiendelea, “mito kama vile Ganges, Indus na Brahmaputra, ambayo hupokea asilimia 70 hadi 80 ya maji yake kutoka katika theluji na kuyeyuka kwa barafu, itakauka.” Matokeo yatakuwa “msiba wa kiikolojia,” aonya. Kwa wakati uliopo, hatari ya furiko kubwa yaendelea. Mito ya barafu inapopungua, maziwa hufanyizwa ambayo huzungukwa na kuta za barafu zilizo rahisi kuvunjika, majabali, na changarawe. Kuyeyuka kunapoendelea, kuta hupasuka, na kupeleka mafuriko yenye kuangamiza kwenye mabonde yaliyoko chini.

Hatari za Tumbaku kwa Watoto

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lakadiria kwamba afya ya watoto wapatao asilimia 50 imo hatarini kwa sababu ya moshi wa tumbaku, laripoti gazeti la London Guardian. Magonjwa yanayohusianishwa na kuvuta moshi wa mwenye kuvuta sigareti yanatia ndani ugonjwa wa pumu na matatizo mengine yanayohusiana na upumuaji, kifo cha ghafula cha kitoto, maradhi ya sikio, na kansa. Utafiti pia waonyesha kwamba watoto wa wavutaji-sigareti huumia kimasomo na wana matatizo mengi ya tabia. Ikiwa wazazi wote wawili wanavuta sigareti, watoto wao wanaelekea kupatwa na matatizo ya afya kwa asilimia 70, na hata mvutaji-sigareti mmoja katika familia atazidisha uwezekano huo kwa asilimia 30. Shirika la WHO lasihi kuwe na elimu ya afya kwa wazazi ili kuwasaidia watambue hatari ambazo tabia yao ya tumbaku huletea familia yao na wapige marufuku uvutaji wa sigareti shuleni na mahali penginepo palipo na watoto mara nyingi.

Ushindi wa Utalii

Kulingana na matabiri yaliyofanywa na Shirika la Utalii Ulimwenguni (WTO), “watalii wa kimataifa wataongezeka kutoka milioni 625 za sasa kwa mwaka hadi bilioni 1.6 mwaka wa 2020,” laripoti The UNESCO Courier. Watalii hao wanatazamiwa kutumia dola za Marekani zaidi ya trilioni mbili, “ikifanya utalii kuwa biashara inayoongoza.” Kufikia sasa, Ulaya imekuwa sehemu yenye kupendwa zaidi. Ufaransa ndiyo nchi inayotembelewa zaidi, ikiwa na wageni milioni 70 mwaka wa 1998. Hata hivyo, kufikia mwaka wa 2020, China inatazamiwa kuchukua mahali pa kwanza. Ingawa hivyo, safari za kimataifa, zabaki kuwa haki ya nchi chache zilizopendelewa. Mwaka wa 1996, ni asilimia 3.5 tu ya idadi ya watu ulimwenguni waliosafiri ng’ambo. Shirika la WTO latabiri kwamba idadi hii itafikia asilimia 7 kufikia mwaka wa 2020.

Je, Kuna Hatari ya Likizo Fupifupi?

Likizo fupifupi, pumziko la mwisho-juma ambalo hivi karibuni limekuwa likichochewa na biashara ya usafiri ya Ulaya kuwa njia ya haraka na rahisi ya kustarehe mbali na mikazo ya akili ya maisha, kwa kweli huenda “ikatokeza madhara zaidi badala ya kuleta manufaa,” laripoti gazeti Guardian la London. Kulingana na mtaalamu wa maradhi ya moyo Dakt. Walter Pasini, wa Shirika la Afya Ulimwenguni, kufunga mizigo, kukimbia kwenye uwanja wa ndege, kusafiri kwa ndege, pamoja na mabadiliko ya halihewa, chakula, na hali zenye kuchosha za saa tofauti-tofauti, huchangia uchovu na zinaweza kusababisha hatari. Mwili huhitaji siku chache kustarehe na kujirekebisha kulingana na tabia ya nchi na mtindo wa maisha, na jambo hilo linapokosa kutokea, mzunguko na utaratibu wa usingizi huathiriwa vibaya. Uchunguzi wa Dakt. Pasini “ulipata kwamba wale waliochukua siku chache kupumzika walielekea kupatwa na mshtuko wa moyo kwa asilimia 17 zaidi na walielekea kupata aksidenti ya gari kwa asilimia 12 zaidi kuliko wale ambao walichukua juma moja au zaidi,” gazeti hilo likasema. “Maana yake si kusema kwamba likizo fupifupi ni zenye hatari kiasili, bali kwamba watu wanapaswa kujihadhari na kujitayarisha vema,” akasema Dakt. Pasini, aliyenukuliwa katika Daily Telegraph la London. “Sasa watu huchukua likizo fupi zaidi na kukimbia wakijaribu kukusanya pamoja kila kitu kwa siku chache, lakini hiyo si njia nzuri ya kustarehe. Kwa kweli, ni njia yenye kuleta mkazo wa akili sana.”

Kisasi cha Nyokakayamba

“Nyokakayamba wanaweza kukuuma hata baada ya kuuawa—na kioja hicho cha kisasi cha baada ya kufa kwa kushangaza ni cha kawaida,” laripoti New Scientist. Kati ya wagonjwa 34 wanaotibiwa kwa sababu ya kuumwa na nyokakayamba huko Arizona, Marekani, zaidi ya kipindi cha miezi 11, watano walisema kwamba nyoka huyo aliwashambulia baada ya kuuawa, ndivyo wanavyosema madaktari wawili wanaojifunza juu ya tukio hilo. Mtu mmoja aliyeumwa aliiua nyoka, akakata kiwiliwili chake kwenye shingo, akangoja aache kusonga, kisha akaokota kichwa hicho. Kilimrukia kwa ghafula na kumuuma mikono yote miwili. Uchunguzi wa hapo awali umeonyesha kwamba kichwa kilichokatwa cha nyokakayamba “kitajaribu kushambulia vitu vinavyopeperushwa mbele yake kwa karibu muda wa saa moja baada ya kufa,” gazeti hilo likasema. Wataalamu wa wanyama watambazi huamini kwamba “tendo la kujiendesha, linalochochewa na vipima-hisi vyenye miali isiyoonekana katika ‘kiungo mvungu,’ kiungo kilicho kati ya mwanzi wa pua na jicho ambacho hugundua joto la mwili.” Dakt. Jeffrey Suchard aonya kwamba nyokakayamba aliyekatwa kichwa apasa kuonwa kama “nyoka mfupi sana.” “Ikiwa ni lazima umshike,” akasema, “nadokeza utumie kijiti kirefu sana.”