Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Wayeswiti Wanyimwa Usajili Huko Urusi

Wizara ya Haki ya Urusi imekataa ombi la kusajili Society of Jesus ikiwa shirika huru la kidini, laripoti National Catholic Reporter. Shirika la Society of Jesus, lijulikanalo sana kama Wayeswiti, lilianzishwa mwaka wa 1540. Chini ya sheria mpya ya dini huko Urusi, mashirika mengi ya kidini yanahitajika kujiandikisha upya ili yaweze kutambuliwa kisheria. Vikundi ambavyo vinanyimwa usajili haviwezi kuchapisha au kugawanya fasihi za kidini, kukaribisha wakazi wa kigeni kwa ajili ya shughuli za kidini, au kuanzisha nyenzo za kielimu. Mashahidi wa Yehova waliandikishwa upya kitaifa mnamo Aprili 29, 1999.

Kujiua Kwaongezeka Japani

Katika Japani watu wengi zaidi walijiua katika mwaka wa 1998 kuliko mwaka mwingine wowote uliotangulia, laripoti The Daily Yomiuri. Kulingana na Wakala wa Polisi wa Kitaifa wa Japani, watu 32,863 walijiua katika 1998—zaidi ya mara tatu ya idadi ya watu waliokufa kutokana na aksidenti za barabarani katika Japani. Ongezeko hilo linatokana na matatizo ya kifedha yanayosababishwa na kukosa kazi za kuajiriwa, jambo ambalo limeiathiri nchi hiyo baada ya mshuko wa kiuchumi wa hivi majuzi. Kujiua ni kisababishi namba sita cha kifo katika Japani.

Uchafuzi wa Hewa Wenye Kufisha

“Magari ya barabarani ndiyo chanzo kinachoendelea kukua haraka zaidi cha uchafuzi katika Ulaya na katika nchi fulani watu wengi zaidi wanakufa kutokana na uchafuzi wa hewa kuliko wale wanaokufa kutokana na aksidenti [za barabarani],” laripoti shirika la habari la Reuters. Kulingana na uchunguzi mmoja uliofanywa na Shirika la Afya Ulimwenguni, watu 21,000 katika Austria, Ufaransa na Uswisi hufa kabla ya wakati kila mwaka kutokana na magonjwa ya kupumua na ya moyo yanayosababishwa na uchafuzi wa hewa. Katika ripoti nyingine tofauti, inakadiriwa kwamba katika miji 36 ya India, watu 110 hufa kabla ya wakati kila siku kwa sababu ya uchafuzi wa hewa.

Mfumo wa Kielektroni wa Kuhifadhi Data Wafifia Upesi

Kwa miaka mingi wanasayansi wa kompyuta walisema kwamba kuhifadhi habari katika mfumo wa kielektroni ilikuwa njia yenye kutegemeka zaidi kuliko kutumia karatasi. Hata hivyo, sasa wasimamizi wa maktaba na wahifadhi-nyaraka wana maoni tofauti. “Tunapoteza idadi kubwa sana ya nyenzo muhimu za kisayansi na kihistoria kwa sababu ya kuchanguka au kuwa zisizofaa kwa sasa,” lasema gazeti la Newsweek. Mifumo ya kielektroni kama vile diski za kompyuta zinaathiriwa na joto, unyevu, kutiwa oksijeni na miale ya sumaku. Na ikitegemea hali za kuhifadhi, tepu ya kuhifadhia data za kielektroniki yaweza kudumu kwa mwongo mmoja tu, gazeti hilo lasema. Pingamizi jingine kwa wanaojaribu kuhifadhi habari kielektroniki ni kule kubadilika haraka kwa tekinolojia. Vifaa vinavyotumiwa kuhifadhia data hubadilika haraka sana hivi kwamba mifumo hiyo inakuwa haifai baada ya muda mfupi. Abby Smith wa Council on Library and Information Resources asema: “Habari haiwezi kudumu sana isipokuwa ihifadhiwe katika jumba la makumbusho la mashine za kuchezea tepu na kompyuta za kibinafsi.”

Idadi ya Watu Huko India Yapita Bilioni Moja

Kulingana na United Nations Population Division, idadi ya watu huko India ilipita bilioni moja katika Agosti 1999. Miaka 50 tu iliyopita, idadi ya watu huko India ilikuwa thuluthi ya ilivyo sasa. Ikiwa idadi hiyo itaendelea kukua kwa kiwango cha sasa cha asilimia 1.6 kwa mwaka, katika muda wa karibu miongo minne, India itapita China ikiwa nchi yenye watu wengi zaidi. “Tayari India na China zina thuluthi ya idadi ya watu ulimwenguni pote,” laripoti gazeti la The New York Times. Katika muda upunguao nusu karne matarajio ya muda wa kuishi katika India umeongezeka kutoka miaka 39 kufikia miaka 63.

Kiwango cha Ndoa Chapunguka Marekani

Uchunguzi uliofanywa na Mradi wa Ndoa katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Rutgers, ulionyesha kwamba kiwango cha ndoa katika Marekani kimepungua sana katika historia yote, gazeti la The Washington Post laripoti katika Web site yake ya Internet. Pia uchunguzi huo ulionyesha kwamba baada tu ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, asilimia 80 ya watoto katika taifa hilo walikuwa wakilelewa katika familia zilizokuwa na wazazi wawili halisi. Hata hivyo, leo idadi hiyo imepungua kufikia asilimia 60. “Asilimia ya wasichana matineja waliosema kwamba kuzaa mtoto nje ya ndoa ni ‘mtindo unaofaa’ iliongezeka kutoka asilimia 33 kufikia asilimia 53 katika miongo miwili iliyopita,” ripoti hiyo yasema. Haishangazi kwamba ripoti hiyo ilisema: “Ndoa iko katika hali yenye taabu sana”!

Matatizo ya Elimu Katika Afrika

Zaidi ya watoto milioni 40 wenye umri wa kwenda shule katika eneo lililo karibu na jangwa la Sahara katika Afrika hawaendi shule, laripoti Shirika la Habari la All Africa News. Matatizo fulani yamekumba mfumo wa elimu katika eneo hilo. Kwa kielelezo, likiwa tokeo la matatizo ya kiuchumi, shule nyingi hazina maji na zina vyoo vichache au hazina vyoo. Kuna uhaba wa vitabu vya mafunzo, na walimu hawajazoezwa vizuri. Kwa kuongezea matatizo ya kiuchumi, kuna visa vingi vya wasichana matineja wanaopata mimba, jambo ambalo ni kisababishi kikuu cha kuacha shule. UKIMWI pia umeathiri sana uhudhuriaji wa shule. “Wabalehe wengi wameambukizwa UKIMWI kwa sababu ya kufanya ngono mapema,” lasema Africa News. Katika visa fulani, wasichana ambao hawajaambukizwa UKIMWI wanahitajiwa kukaa nyumbani na kutunza jamaa zao ambao wameambukizwa ugonjwa huo. Dakt. Edward Fiske ambaye ni mtaalamu wa elimu ya msingi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa asema hivi: “Bila elimu, wakati ujao wa nchi nyingi zilizo karibu na jangwa la Sahara katika Afrika haujulikani.”

Maiti Aliyetiwa Mumiani Apatwa Akiwa na Kidole Bandia cha Mguu

“Maiti alipatikana akiwa ametiwa kidole bandia cha mguu na yaonekana alikitumia alipokuwa hai kabla hajazikwa akiwa nacho miaka 2,500 iliyopita,” laripoti The Sunday Times la London. Kidole hicho bandia, kilifanyizwa kwa kitani iliyochanganywa na gundi ya wanyama na plasta ya jasi, Dakt. Nicholas Reeves anakieleza kuwa “bidhaa tata iliyobuniwa vizuri, kwa ustadi na kutengenezwa kwa uthabiti, na kwa wazi ni agizo la pekee.” Kidole hicho cha mguu kilikuwa na ukucha na kilipakwa rangi iliyofanana na nyama. Mashimo manane yalitobolewa ili kukiunganisha. Mashimo hayo yafanana kwa ukaribu na muundo wa Y wa kamba za makubazi ili kwamba wakati kidole hicho kimevaliwa mashimo hayo yangefichwa na kamba za makubazi.

Maumivu ya Kichwa Yaletwayo na Dawa za Kutuliza Maumivu!

Watu wanaomeza dawa mara tatu au zaidi kwa juma kwa sababu ya maumivu ya kichwa wanaweza kuwa wanaathiriwa na maumivu ya kichwa yaletwayo na matumizi mabaya ya dawa (MMH). Yafikiriwa kuwa mtu 1 kati ya 50 ameathiriwa, MMH husababishwa na vitulizo sahili kama vile aspirini, vilevile dawa za kutuliza maumivu zinazoagizwa na daktari. Wakati hali ya kutohisi maumivu inapokwisha, dawa hiyo yaweza kusababisha maumivu ya kichwa ambayo huonwa na mgonjwa kuwa maumivu ya kawaida au kipandauso. Mgonjwa humeza dawa zaidi za kutuliza maumivu na hali yake huwa mbaya tena. Dakt. Tim Steiner wa Chuo cha Imperial, London, aeleza kwamba “mgonjwa yeyote anayelalamika kuumwa kichwa sana kila siku apaswa kufikiriwa kuwa ana MMH.” Pia ataja kwamba hata ingawa hali hiyo imejulikana kwa miaka fulani sasa, madaktari wengi wa kibinafsi hawaifahamu na wao huagiza dawa za kutuliza maumivu zenye nguvu zaidi, huku jambo tu linalohitajika kwa upande wa mgonjwa ni kuacha kumeza dawa hizo, laripoti The Sunday Telegraph la London.

Utunzaji wa Ulimi

Bakteria zinazojificha nyuma ya ulimi wako zaweza kutokeza gesi za salfa ambazo zaweza kusababisha harufu mbaya ya mdomoni yasema ripoti moja katika gazeti la Prince George Citizen. “Bakteria husitawi katika mazingira makavu, yasiyo na oksijeni hii ikiwa ndiyo sababu hizo huishi katika mianya na mashimo mbali na hewa tunayopumua mapafuni,” ripoti hiyo yasema. Kupiga mswaki na kutoa uchafu katikati ya meno husaidia, lakini ni karibu asilimia 25 tu ya bakteria humalizwa kwa kupiga mswaki. Daktari wa meno Allan Grove aamini kwamba kukwaruza ulimi, utamaduni wa kale katika Ulaya, ndilo “jambo la maana zaidi unaloweza kufanya ili kuzuia harufu mbaya ya mdomoni.” Kutumia kikwaruzo cha plastiki “ni bora zaidi kuliko kutumia mswaki ili kuweka ulimi wako ukiwa safi,” lasema Citizen.

Jicho Jipya la Kuchunguza Ulimwengu

Darubini-upeo ya Gemini North, iliyoko juu ya mlima Mauna Kea, huko Hawaii, ilichunguza ulimwengu mara ya kwanza mnamo Juni 1999. Kioo chake chenye kukusanya nuru, ambacho kina kipenyo cha meta 8.1, kitawawezesha waastronomia kuona vitu hafifu zaidi katika anga pana, laripoti gazeti la Independent la London. Darubini-upeo ya Gemini North na ya Hubble zilizo angani husaidia waastronomia kuchunguza matukio ya zamani za kale na hivyo “kuchunguza wakati uliopita.” Ubora wa darubini-upeo ya Hubble ni kwamba imewekwa angani. Ingawa Gemini, imewekwa ardhini, inategemea mtambo wa kompyuta ili kuzuia kubadilika kwa umbo kunakosababishwa na michafuko ya angani, na hutokeza picha safi kama zile za Hubble—au zilizo bora zaidi.