Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 JE, NI KAZI YA UBUNI?

Umbo la Magamba ya Moluska

Umbo la Magamba ya Moluska

MAGAMBA huwawezesha moluska kubaki salama licha ya misukosuko mingi ya baharini. Uwezo wa magamba ya moluska wa kuwalinda viumbe hao umewachochea wahandisi kuchunguza muundo wake ili waunde magari na kujenga nyumba zinazoweza kuwalinda wale waliomo ndani.

Fikiria jambo hili: Wahandisi walichunguza aina mbili za magamba. Aina moja ni ile ya magamba ya chaza (koambili) na ya pili ni magamba yenye umbo la pia.

Wachunguzi walitambua kwamba miinuko iliyopo katika koambili huelekeza msukumo kwenye muungano wa koa hizo na pia kwenye kingo zake. Kwa upande mwingine, kujipindapinda kwa magamba yenye umbo la pia huelekeza msukumo kwenye mhimili wa koa na katika sehemu ya juu iliyotanuka. Katika visa vyote viwili, ilionekana kwamba muundo wa magamba uliyawezesha kuelekeza msukumo kwenye maeneo imara, hivi kwamba hata ikiwa gamba lenyewe lingeharibika, kiumbe aliye ndani hangedhurika.

Watafiti pia walilinganisha uwezo wa kuhimili msukumo wa magamba halisi na mengine yaliyotengenezwa kwa mashine lakini yasiyokuwa na madoido yoyote. Uchunguzi huo ulionyesha kwamba muundo tata wa magamba halisi ulifanya yawe na uwezo wa kuhimili msukumo mara mbili zaidi ya yale yaliyotengenezwa kwa mashine.

Tovuti ya Scientific American ilisema hivi kuhusu matokeo ya utafiti huo: “Ikiwa utaendesha gari lililo na umbo la magamba [ya moluska] siku moja, litakuwa la kisasa na pia lililoundwa kwa njia ya pekee ili kuwalinda wale walio ndani.”

Una maoni gani? Je, umbo la magamba ya moluska lilijitokeza lenyewe? Au lilibuniwa?