Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HABARI KUU

Majanga Yanapotokea​—Unachoweza Kufanya Ili Uokoke

Majanga Yanapotokea​—Unachoweza Kufanya Ili Uokoke

“Kulikuwa na mlipuko mkubwa ambao karibu uniangushe chini. Moshi uliingia kupitia matundu ya hewa, na ofisi yetu iliyokuwa juu ikawaka moto.”Joshua.

Matetemeko ya ardhi . . . vimbunga . . . mashambulizi ya kigaidi . . . mauaji shuleni. Ni jambo la kawaida kuona maneno hayo kwenye vichwa vya habari. Bila shaka, kusoma tu kuhusu majanga hakuwezi kulinganishwa na kupatwa na majanga kihalisi. Unaweza kufanya nini kabla, wakati wa tukio, na baada ya janga kutokea ili ubaki salama?

KABLA​—JITAYARISHE!

MAJANGA yanaweza kumkumba yeyote yule. Ili uokoke, ni muhimu sana ujitayarishe mapema. Lakini, kujitayarisha kunahusisha nini?

  • Jiandae kiakili. Kubali ukweli wa kwamba majanga hutokea na yanaweza kukupata wewe na wale unaowapenda. Ukisubiri mpaka janga likupate, utakuwa umechelewa mno.

  • Jifunze kuhusu majanga ambayo yanaweza kulikumba eneo lenu. Hakikisha unafahamu mahali pa kukimbilia. Chunguza ikiwa nyumba yako imejengwa vizuri na ikiwa ipo mahali salama. Ondoa vitu vinavyoweza kusababisha moto, kama vile, koili za kufukuzia mbu, sigara, mishumaa, viberiti, na mafuta ya taa. Pia, nyakati zote hakikisha kuna mtu jikoni chakula kinapopikwa.

  • Andaa mahitaji ya dharura. Huduma za umeme, maji, simu, na usafiri zinaweza kuathiriwa. Ikiwa una gari, hakikisha kwamba nyakati zote lina mafuta angalau nusu tanki, na wakati wote hakikisha una chakula, maji, na sanduku la dharura nyumbani mwako.—Soma sanduku “ Je, Una Kile Kinachohitajika Wakati wa Dharura?

    Ili uokoke, ni muhimu sana ujitayarishe mapema

  • Weka karibu namba za simu za marafiki zako wa mbali na walio karibu.

  • Fanya mazoezi ya jinsi utakavyofanya janga likitokea. Hakikisha unajua sehemu za karibu zaidi za kutokea nje ya jengo, na mipango ambayo shule ya wanao imeweka endapo janga litatokea. Pangeni sehemu za kukutania mkiwa familia, kama vile kwenye shule au bustani ya umma. Sehemu moja iwe karibu na mnapoishi na nyingine nje ya eneo lenu. Wenye mamlaka hupendekeza kutembelea maeneo hayo kama njia ya kufanya mazoezi ya kile mtakachofanya janga likitokea.

  • Panga kuwasaidia wengine, kutia ndani wazee na wasiojiweza.

WAKATI WA TUKIO​—CHUKUA HATUA HARAKA

Joshua aliyetajwa kwenye utangulizi anasema: “Moto ulipotokea, watu wengi hawakushtuka, bali walisuasua. Wengine walikuwa wakizima kompyuta au kujaza maji kwenye chupa zao. Mwanamume mmoja alisema, ‘Labda ingefaa tusubiri kwanza.’” Licha ya kwamba wengine walikuwa wanasuasua, Joshua alisema hivi kwa sauti kubwa: “Tunapaswa kutoka humu ndani sasa hivi!” Hiyo ilifanya wafanyakazi wenzake wachukue hatua haraka na kumfuata alipokuwa akishuka ngazi. Joshua aliendelea kuwaambia: “Yeyote akianguka, mnyanyue na mwendelee kusonga. Sisi sote tutaokoka!”

  • Moto unapotokea. Lala chini na utambae haraka kuelekea mahali pa karibu zaidi pa kutokea nje. Moshi hufanya iwe vigumu kuona, na vifo vingi vya moto husababishwa na kuvuta hewa yenye moshi. Usihangaike kuchukua vitu vyako. Sekunde chache tu zinaweza kukugharimu uhai.

  • Tetemeko la ardhi. Ingia uvunguni mwa fanicha iliyo imara au kaa karibu na ukuta ulio ndani ya nyumba. Kumbuka kutakuwa na matetemeko mengine madogo madogo. Kwa hiyo, toka nje mara tu tetemeko linapotulia na usikae karibu na jengo lolote. Huenda saa nyingi zikapita kabla ya waokoaji stadi kufika, kwa hiyo jitahidi kuwaokoa wengine ikiwa unaweza.

  • Tsunami. Ukiona maji ya bahari yanarudi nyuma ghafla, kimbilia kwenye maeneo ya juu. Hiyo ni ishara ya kwamba mawimbi mengine mengi makubwa zaidi yanakuja.

  • Vimbunga. Kimbilia kwenye vyumba vilivyo chini ya ardhi au orofa ya chini zaidi katika jengo. Ikiwa hakuna, nenda katikati ya nyumba.

  • Mafuriko. Usikae karibu na majengo yaliyoathiriwa na mafuriko. Usijing’ang’anize kupita kwenye maji ukiwa na gari. Maji ya mafuriko yanaweza kuwa na uchafu na kuficha hatari kama vile, mabaki ya vitu, mashimo, na nyaya za umeme zilizoanguka.

  • Je, wajua? Maji yanayotembea yenye kina cha futi mbili [au mita 0.6] yanaweza kulisomba gari. Vifo vingi wakati wa mafuriko hutokea watu wanapojaribu kupita na gari kwenye maji yanayotembea.

  • Mkiagizwa na serikali kuondoka, fanyeni hivyo bila kukawia! Wajulishe rafiki zako mahali ulipo ili wasihatarishe uhai wao wakikutafuta.

    Mkiagizwa na serikali kuondoka, fanyeni hivyo bila kukawia!

  • Je, wajua? Janga linapotokea, uwezekano wa ujumbe mfupi kufika ni mkubwa kuliko kumpata mtu kwa kumpigia simu.

  • Serikali ikiagiza wananchi wabaki ndani, usitoke. Iwapo kuna aksidenti au janga lililosababishwa na silaha za kemikali, za biolojia, au nyuklia, baki ndani na uzibe matundu ya hewa, kutia ndani milango na madirisha yote. Katika janga la nyuklia, lala chini ndani ya nyumba ili usiathiriwe na miale. Sikiliza taarifa za habari kwenye redio au televisheni. Baki ndani mpaka serikali itakapotangaza kwamba hali ni shwari.

BAADA YA JANGA​—JITUNZE!

Ili kujilinda dhidi ya magonjwa na hatari mbalimbali, fuata mapendekezo yafuatayo:

  • Ishi na rafiki zako, ikiwezekana, badala ya kuishi kambini.

  • Dumisha usafi mahali unapoishi.

  • Tumia vifaa vya kujilinda unapoondoa takataka. Ikiwezekana vaa glavu, viatu imara, kofia ngumu, na vichuja hewa. Jihadhari na nyaya za umeme na moto ambao haujazima kabisa.

  • Endelea na ratiba yako ya kila siku kwa kadiri unavyoweza. Watoto wako wanahitaji kuona kwamba umetulia na hujakata tamaa. Soma nao vitabu vya shule, na pia mcheze na kuabudu pamoja. Usifuatilie sana habari kuhusu janga lililowapata, na usiruhusu mahangaiko au mkazo ulio nao uathiri jinsi unavyoitendea familia yako. Kubali msaada, na uwasaidie wengine.

    Baada ya janga, endelea na ratiba yako ya kila siku kwa kadiri unavyoweza

  • Kubali ukweli wa kwamba majanga hutokeza hasara kubwa. Lengo la serikali na mashirika mbalimbali ya kutoa misaada ni kuandaa mahitaji ya msingi, na si kuwarudishia watu kila kitu walichopoteza. Mahitaji ya msingi ni maji safi, chakula, mavazi, na makazi salama.—1 Timotheo 6:7, 8.

  • Chunguza madhara ya kihisia uliyopata na utafute msaada. Mara nyingi madhara ya kihisia huonekana baada ya hali kutulia. Dalili zinaweza kutia ndani mahangaiko, huzuni, hisia kubadilika badilika, na pia kushindwa kufikiri, kufanya kazi, na kulala kwa urahisi. Zungumza na marafiki wanaokujali.

Ingawa Joshua aliokoka janga la moto lililotokea kazini kwake, wafanyakazi wenzake wengi walikufa. Wazee Wakristo na wataalamu wa afya ya akili walimsaidia sana. Anasema hivi: “Walinihakikishia kwamba ni kawaida kuwa na huzuni baada ya kupatwa na janga na kwamba ingeisha hatimaye. Baada ya miezi sita, ndoto zenye kushtua zilipungua. Madhara mengine yamechukua muda mrefu zaidi.”

Majanga hutuumiza kwa sababu yanafanya watu wasio na hatia wateseke. Matokeo ni kwamba, wengine humlaumu Mungu kwa jambo ambalo hajafanya. Wengi, kama ilivyokuwa kwa Joshua, huhisi hatia kwa sababu wameokoka ilhali wengine wamekufa. Anasema: “Bado huwa nawaza ikiwa ningeweza kuokoa watu wengi zaidi. Kuamini kwamba hivi karibuni Mungu ataleta haki kwa ukamili na kuondoa matatizo yote, hunifariji sana. Kwa sasa, ninathamini kila siku ninayoishi na kufanya kile ninachoweza ili kujitunza.”—Ufunuo 21:4, 5. *

^ fu. 33 Kwa habari zaidi kuhusu ahadi za Mungu za wakati ujao na kwa nini ameruhusu kuteseka, soma kitabu Biblia Inafundisha Nini Hasa? Unaweza kukipakua kwenye www.jw.org/sw.