Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 MAHOJIANO | RAJESH KALARIA

Mtaalamu wa Ubongo Anaeleza Kwa Nini Anamwamini Mungu

Mtaalamu wa Ubongo Anaeleza Kwa Nini Anamwamini Mungu

PROFESA Rajesh Kalaria, wa Chuo Kikuu cha Newcastle, Uingereza, amechunguza ubongo wa mwanadamu kwa miaka zaidi ya 40. Awali, aliamini nadharia ya mageuzi. Lakini baadaye alibadili maoni yake. Mwandishi wa Amkeni! alimhoji kuhusu kazi na imani yake.

Tafadhali tueleze kuhusu historia yako ya kidini.

Baba yangu alizaliwa nchini India, na mama ingawa pia ni Mhindi alizaliwa nchini Uganda. Hivyo, wote walifuata sana desturi za Kihindu. Mimi ni wa pili kuzaliwa kati ya watoto watatu. Tuliishi katika jiji la Nairobi, nchini Kenya. Majirani zetu wengi walikuwa Wahindu.

Kwa nini ulipendezwa na sayansi?

Nilipenda wanyama, na mara nyingi tulienda kupiga kambi na kupanda milima tukiwa na rafiki zangu ili tujionee wanyama pori. Mwanzoni nilitaka kuwa daktari wa mifugo. Lakini baada ya kuhitimu katika chuo cha ufundi jijini Nairobi, nilienda nchini Uingereza kusomea udaktari katika Chuo Kikuu cha London. Baadaye, niliamua kusomea ubongo wa mwanadamu.

Je, masomo yaliathiri imani yako ya kidini?

Ndiyo. Kadiri nilivyosoma sayansi, nilianza kutilia shaka hekaya na tamaduni za Kihindu, kama vile kuabudu wanyama na sanamu.

Kwa nini ulikubaliana na nadharia ya mageuzi?

Watu wengi ambao nilishirikiana nao nilipokuwa mdogo waliamini kwamba mageuzi ya wanadamu yalianzia barani Afrika, na hayo yalikuwa mazungumzo ya kawaida shuleni. Pia, walimu na maprofesa wa chuo kikuu walifanya tuwe na maoni ya kwamba wanasayansi wote wanaoheshimika wanaamini nadharia ya mageuzi.

 Baada ya muda ulichunguza upya chanzo cha uhai. Kwa nini?

Nilikuwa nikisomea biolojia na anatomia, mwanafunzi mwenzangu aliponieleza kuhusu habari za Biblia alizokuwa akifundishwa na Mashahidi wa Yehova. Nilitamani kujua mengi zaidi. Hivyo, nilihudhuria kusanyiko la Mashahidi lililofanywa kwenye ukumbi wa chuo chetu huko Nairobi. Baadaye, Mashahidi wawili wamishonari walinifafanulia baadhi ya mafundisho ya Biblia. Imani yao katika Muumba Mkuu ambaye ana majibu ya maswali muhimu maishani haikuonekana kuwa hekaya. Niliona kuwa mambo hayo yanapatana na akili.

Je, elimu yako ya kitiba ilifanya utilie shaka uumbaji?

La hasha! Kadiri nilivyoendelea na masomo yangu niligundua jinsi ambavyo viumbe wamebuniwa kwa njia stadi na tata sana. Niliona kuwa ni jambo lisilopatana na akili kufikiri kwamba miili tata kiasi hicho ilijitokeza yenyewe tu.

Unaweza kutueleza mfano halisi?

Nimekuwa nikichunguza ubongo wa mwanadamu tangu mwaka wa 1971, na bado ninashangazwa na kiungo hicho cha pekee. Ubongo ndio kitovu cha mawazo na kumbukumbu, na huongoza utendaji mwingi mwilini. Pia, ubongo ni chanzo cha hisi zote za mwili, na huchanganua habari zinazotoka ndani na nje ya mwili.

Utendaji tata na muungano wa chembe za neva ndio hasa huuwezesha ubongo wetu kufanya kazi. Kuna mabilioni ya chembe za neva kwenye ubongo wa mwanadamu ambazo huwasiliana kupitia nyuzinyuzi ndefu zinazoitwa aksoni. Chembe moja inaweza kuunganishwa na maelfu ya chembe nyingine kupitia nyuzinyuzi zilizosambaa zinazoitwa dendriti. Hivyo, kuna mamia ya maelfu ya miungano kwenye ubongo. Jambo la kuvutia ni kwamba ingawa miungano hiyo ya chembe za neva na dendriti ni mingi sana, inafanya kazi kwa utaratibu. Ni mfumo wa kustaajabisha sana.

Tafadhali fafanua.

Mfumo huo hukua kwa utaratibu sana kuanzia mtoto anapokuwa kwenye tumbo la uzazi na kuendelea baada ya kuzaliwa. Chembe za neva hutuma nyuzinyuzi kwenye chembe nyingine ambazo huenda zikawa umbali wa sentimita chache tu. Huo ni umbali mrefu sana kwa chembe za neva. Lengo hasa la nyuzinyuzi huenda lisiwe kwenda kwenye chembe fulani tu bali katika sehemu hususa ya chembe hiyo.

Nyuzinyuzi mpya kutoka kwenye chembe ya neva huongozwa na kemikali ambazo hutoa ishara kama vile, “simama,” “nenda,” au “geuka,” hadi ifike pale inapotakiwa. Bila mwongozo ulio wazi, nyuzinyuzi zinazokua zingepotea na kushindwa kufika zinapohitajiwa. Mfumo huo umepangwa kwa njia ya pekee, kuanzia kwenye maagizo yaliyo katika DNA yetu.

Licha ya hayo yote bado hatuelewi kikamili kuhusu ukuzi wa ubongo na jinsi unavyofanya kazi, kutia ndani jinsi unavyofanyiza kumbukumbu, hisia, na mawazo. Wazo tu la kwamba ubongo wetu hufanya kazi, bila kujali jinsi unavyofanya kazi hiyo kwa njia ya pekee na ukuzi wake wenye kustaajabisha, hunithibitishia kuna Muumba mwenye akili zaidi kuliko zetu.

Kwa nini uliamua kuwa Shahidi wa Yehova?

Mashahidi walinithibitishia kwamba Biblia ni Neno la Mungu. Kwa mfano, Biblia si kitabu cha sayansi, lakini inapogusia mambo ya sayansi inaeleza kwa usahihi. Pia, inatoa unabii ulio sahihi. Jambo lingine ni kuwa inaboresha maisha ya wale wanaofuata mafundisho yake. Mimi mwenyewe nimejionea hilo maishani. Tangu nilipobatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova mwaka wa 1973, Biblia imekuwa mwongozo wangu. Matokeo ni kwamba, nina maisha yenye kuridhisha na yaliyo na kusudi.