NCHI NA WATU
Kutembelea Kyrgyzstan
NCHI ya Kyrgyzstan ipo Asia ya Kati, imezungukwa na milima mirefu yenye vilele vilivyofunikwa na theluji, na inapakana na nchi za Kazakhstan, Uzbekistan, Tajikistan, na China. Karibu asilimia 90 ya nchi hiyo ni milima. Kyrgyzstan inajivunia kuwa na kilele kirefu cha mlima katika safu ya milima ya Tian Shan ambacho kipo meta 7,439 kutoka usawa wa bahari. Karibu asilimia nne ya nchi hiyo ni misitu. Inasemekana kwamba Kyrgyzstan ndiyo nchi pekee duniani ambapo misitu mikubwa ya miti ya mijozi ya asili inapatikana.
Watu wa Kyrgyzstan wanajulikana kwa ukarimu na kuwaheshimu wengine. Nchini Kyrgyzstan inafaa kutumia neno “wewe” kwa upole unapomtambulisha mtu aliyekuzidi umri na pia kumpisha aketi kwenye kiti ndani ya usafiri wa umma au kumruhusu aketi kwenye kiti cha mbele wakati wa matukio ya pekee.
Kwa kawaida familia huwa na watoto watatu au zaidi. Mara nyingi mvulana wa mwisho huishi na wazazi wake hata baada ya kuoa ili awatunze watakapozeeka.
Wasichana wanafundishwa kazi mbalimbali za nyumbani ili waweze kutunza familia zao vizuri. Kufikia umri wa utineja, tayari wasichana hao wanakuwa na ustadi wa kutosha wa kutunza familia zao. Kwa kawaida zawadi hutayarishwa kwa ajili ya bibi arusi. Zawadi hizo zinatia ndani matandiko ya kila aina, mavazi mbalimbali na zulia lililotengenezwa kwa mikono. Bwana arusi hutoa pesa na mifugo kama mahari.
Kondoo au farasi huchinjwa wakati wa sherehe au mazishi. Nyama hizo hugawanywa vipande na kila kipande kinakuwa maalumu kwa ajili ya mtu fulani pekee. Kwa kuwa watu hao wanaheshimu sana utamaduni wao, kila mtu hupewa kipande cha nyama kulingana na umri wake, au wadhifa katika jamii. Baada ya ugawaji huo wanakula chakula kikuu cha nchi hiyo kinachoitwa Beshbarmak. Chakula hicho huliwa kwa mikono.