Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jiji la Toledo lina historia na utamaduni mwingi wa nchi ya Hispania. Katika mwaka wa 1986, jiji hilo lilichaguliwa kuwa Eneo Linalopaswa Kuhifadhiwa Duniani na ni kivutio kikuu cha watalii

 NCHI NA WATU

Kutembelea Hispania

Kutembelea Hispania

HISPANIA ni nchi yenye watu wa jamii mbalimbali na mandhari tofauti-tofauti. Maeneo mengi nchini humo hulimwa ngano, mizabibu, na mizeituni. Upande wa kusini, Hispania imetenganishwa na bara la Afrika na sehemu ya bahari yenye upana wa kilometa 14.

Watu wengi kutia ndani Wafoinike, Wagiriki, na Wakarthage walihamia nchi hiyo iliyo kaskazini magharibi mwa bara la Ulaya. Waroma walipoiteka nchi hiyo katika karne ya tatu K.W.K., waliita Hispania. Kisha, Wakigothi na Waarabu-waislamu walihamia nchini humo, nao waliacha kumbukumbu za tamaduni zao.

Hivi karibuni katika kipindi cha mwaka mmoja, zaidi ya watalii milioni 68 walitembelea Hispania. Wengi hutembelea Hispania ili wafurahie kuota jua, fukwe maridadi, sanaa, historia, na majengo ambayo ni hazina  kubwa ya nchi hiyo. Vyakula vya Kihispania huwavutia watu wengi wanaotembelea huko. Vyakula vya asili hutia ndani viumbe wengi wa baharini, vipande vyembamba vya nyama ya nguruwe, mchuzi uliotayarishwa vizuri, kachumbari na mboga zilizotiwa au kupikwa kwa mafuta ya zeituni. Spanish omelets, paella, na tapas ni vyakula vinavyojulikana duniani kote.

Mariscada ni chakula cha asili kinachoandaliwa kutokana na viumbe wa baharini

Watu wakicheza dansi ya flamenko

Wahispania ni watu wachangamfu na wenye urafiki. Wengi hudai kuwa wao ni waumini wa Kanisa Katoliki, lakini ni wachache tu ambao wanahudhuria Misa. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na wahamiaji wengi kutoka barani Afrika, Asia, na Amerika ya Latini. Wengi wao hupenda kuzungumzia imani yao ya kidini na tamaduni zao. Mashahidi wa Yehova wamefurahia kuwa na mazungumzo yenye matokeo mazuri pamoja nao na kuwafundisha maoni ya Biblia kuhusiana na habari mbalimbali.

Mwaka wa 2015, zaidi ya Mashahidi 10,500 walijitolea kujenga au kurekebisha majengo yao 70 ya ibada yanayoitwa Majumba ya Ufalme. Baadhi ya Majumba hayo yamejengwa katika maeneo ambayo yalitolewa na manispaa za nchi. Ili kuwasaidia kiroho wahamiaji, Mashahidi wa Yehova hufanya mikutano kwa lugha zaidi ya 30 kutia ndani Kihispania. Mwaka wa 2016, zaidi ya watu 186,000 walihudhuria tukio muhimu lililofanywa na Mashahidi wa Yehova la kukumbuka kifo cha Yesu Kristo.