Waamuzi 16:1-31

  • Samsoni akiwa Gaza (1-3)

  • Samsoni na Delila (4-22)

  • Samsoni alipiza kisasi na kufa (23-31)

16  Siku moja Samsoni alienda Gaza, akamwona kahaba fulani na kuingia nyumbani mwake.  Watu wa Gaza wakaambiwa, “Samsoni ameingia humu.” Basi wakamzingira na kumvizia usiku kucha kwenye lango la jiji. Wakakaa kimya usiku kucha, wakisema miongoni mwao, “Kesho asubuhi tutamuua.”  Lakini Samsoni akaendelea kulala mpaka usiku wa manane. Kisha akaamka na kung’oa malango ya jiji pamoja na miimo yake miwili na komeo. Akajitwika mabegani na kuipeleka kwenye kilele cha mlima ulio karibu na Hebroni.  Baada ya hayo akampenda mwanamke fulani katika Bonde* la Soreki, aliyeitwa Delila.+  Basi watawala wa Wafilisti wakaenda kwa mwanamke huyo na kumwambia, “Mdanganye*+ ili ujue chanzo cha nguvu zake nyingi na jinsi tunavyoweza kumshinda, kumfunga, na kumdhibiti. Na kila mmoja wetu atakupa vipande 1,100 vya fedha.”  Baadaye Delila akamwambia Samsoni, “Naomba uniambie chanzo cha nguvu zako nyingi na kitu kinachoweza kutumiwa kukufunga na kukudhibiti.”  Samsoni akamwambia, “Wakinifunga kwa kamba saba mbichi za upinde, nitakuwa dhaifu kama mwanadamu mwingine yeyote.”  Basi watawala wa Wafilisti wakamletea mwanamke huyo kamba saba mbichi za upinde, akamfunga nazo.  Nao wakawaficha watu fulani katika chumba cha ndani ili wamvizie, basi Delila akamwambia, “Wafilisti wamekuja kukushambulia, Samsoni!” Ndipo akazikata hizo kamba kwa urahisi kama uzi wa kitani unavyokatika unapoguswa na moto.+ Nao hawakujua siri ya nguvu zake. 10  Basi Delila akamwambia Samsoni: “Umenihadaa* na kunidanganya. Sasa tafadhali, niambie unaweza kufungwa kwa kitu gani?” 11  Kwa hiyo akamwambia, “Wakinifunga kwa kamba mpya ambazo hazijatumiwa, nitakuwa dhaifu kama mwanadamu mwingine yeyote.” 12  Basi Delila akachukua kamba mpya akamfunga nazo, kisha akamwambia hivi Samsoni kwa sauti kubwa: “Wafilisti wamekuja kukushambulia, Samsoni!” (Wakati huo watu waliokuwa wakimvizia walikuwa wamejificha katika chumba cha ndani.) Ndipo akazikata kamba hizo kutoka mikononi mwake kama nyuzi.+ 13  Kisha Delila akamwambia Samsoni, “Mpaka sasa umenihadaa na kunidanganya.+ Niambie unaweza kufungwa kwa kitu gani?” Akamjibu, “Kwa kufuma vishungi saba vya nywele zangu kwa uzi wa mtande.” 14  Basi akavifunga kwa kigingi na kumwambia hivi kwa sauti kubwa: “Wafilisti wamekuja kukushambulia, Samsoni!” Basi akaamka kutoka usingizini na kung’oa kigingi hicho cha wafumaji na uzi wa mtande. 15  Sasa Delila akamwambia, “Unawezaje kusema ‘Nakupenda’+ wakati moyo wako haupo pamoja nami? Umenihadaa mara tatu na hujaniambia chanzo cha nguvu zako nyingi.”+ 16  Delila alimsumbua Samsoni siku baada ya siku na kumshinikiza, akamchosha* hivi kwamba akatamani kufa.+ 17  Mwishowe akamfunulia moyo wake na kumwambia, “Kichwa changu hakijawahi kamwe kuguswa na wembe, kwa kuwa mimi ni Mnadhiri wa Mungu tangu kuzaliwa.*+ Nikinyolewa, nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu kama wanadamu wengine wote.” 18  Delila alipoona kwamba Samsoni amemfunulia moyo wake, akawaita mara moja watawala wa Wafilisti+ na kuwaambia, “Njooni, kwa maana sasa amenifunulia moyo wake.” Basi watawala wa Wafilisti wakaja kwa Delila wakiwa na zile pesa. 19  Delila akamlaza Samsoni mapajani; akamwita mtu ili amnyoe vile vishungi saba vya nywele zake. Ndipo Delila akaanza kumdhibiti, kwa maana alikuwa akiishiwa na nguvu. 20  Kisha Delila akamwambia hivi kwa sauti kubwa: “Wafilisti wamekuja kukushambulia, Samsoni!” Ndipo akaamka kutoka usingizini na kusema, “Nitatoka nje kama awali+ na kujinasua.” Lakini hakujua kwamba Yehova alikuwa amemwacha. 21  Basi Wafilisti wakamkamata na kumng’oa macho. Wakampeleka Gaza na kumfunga kwa pingu mbili za shaba, akawa akisaga nafaka gerezani. 22  Lakini nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa.+ 23  Watawala wa Wafilisti wakakusanyika ili kusherehekea na kumtolea dhabihu nyingi mungu wao Dagoni,+ kwa kuwa walisema, “Mungu wetu amemtia mikononi mwetu adui yetu Samsoni!” 24  Watu walipomwona, wakamsifu mungu wao wakisema, “Mungu wetu amemtia mikononi mwetu adui yetu aliyeharibu nchi yetu+ na kuua watu wengi kati yetu.”+ 25  Mioyo yao ilipojaa furaha wakasema, “Mwiteni Samsoni atutumbuize.” Basi wakamwita Samsoni kutoka gerezani ili awatumbuize; wakamsimamisha katikati ya nguzo. 26  Samsoni akamwambia hivi mvulana aliyekuwa amemshika mkono: “Niache niguse nguzo zinazotegemeza nyumba hii, ili niziegemee.” 27  (Basi nyumba hiyo ilikuwa imejaa wanaume na wanawake. Na watawala wote wa Wafilisti walikuwemo, na darini kulikuwa na watu wapatao 3,000, wanaume na wanawake, waliokuwa wakimtazama Samsoni akiwatumbuiza.) 28  Ndipo Samsoni+ akamlilia Yehova akisema, “Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova, nikumbuke, tafadhali, na kunitia nguvu,+ tafadhali, mara hii moja tu, Ee Mungu, acha niwalipize kisasi Wafilisti kwa ajili ya jicho moja tu, kati ya macho yangu mawili.”+ 29  Kisha Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati zilizotegemeza nyumba hiyo, nguzo moja kwa mkono wa kulia na ile nyingine kwa mkono wa kushoto. 30  Kisha Samsoni akasema hivi kwa sauti kubwa: “Acha nife* pamoja na Wafilisti!” Ndipo akasukuma nguzo hizo kwa nguvu zake zote, na nyumba hiyo ikawaangukia watawala na watu wote waliokuwemo.+ Kwa hiyo watu aliowaua wakati wa kifo chake walikuwa wengi kuliko aliowaua maishani mwake.+ 31  Baadaye ndugu zake na watu wote wa familia ya baba yake wakaja kumchukua. Wakamzika kati ya Sora+ na Eshtaoli katika kaburi la Manoa+ baba yake. Samsoni alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka 20.+

Maelezo ya Chini

Au “Korongo.”
Au “Mshawishi.”
Au “Umenichezea.”
Au “nafsi yake ikachoka.”
Tnn., “kutoka tumboni mwa mama yangu.”
Au “nafsi yangu ife.”