Waamuzi 14:1-20

  • Mwamuzi Samsoni atafuta mke Mfilisti (1-4)

  • Roho ya Yehova yamwezesha Samsoni kumuua simba (5-9)

  • Samsoni atega kitendawili kwenye harusi (10-19)

  • Mwanamume mwingine apewa mke wa Samsoni (20)

14  Ndipo Samsoni akaenda Timna, na akiwa huko akamwona mwanamke Mfilisti.*  Basi akarudi na kuwaambia hivi wazazi wake: “Nimevutiwa na mwanamke fulani Mfilisti huko Timna, ninaomba mniletee awe mke wangu.”  Lakini baba yake na mama yake wakamwambia, “Je, huwezi kupata mke kati ya watu wetu wa ukoo na kati ya ndugu zetu wote?+ Je, ni lazima uoe mke kutoka kati ya Wafilisti wasiotahiriwa?” Lakini Samsoni akamwambia baba yake, “Niletee mwanamke huyo, kwa sababu ndiye anayenifaa.”*  Lakini wazazi wake hawakujua kwamba Yehova aliongoza jambo hilo, kwa sababu Alikuwa akitafuta nafasi ya kuwapiga Wafilisti, kwa kuwa Wafilisti walikuwa wakiwatawala Waisraeli wakati huo.+  Basi Samsoni akaenda na baba yake na mama yake hadi Timna. Alipofika katika mashamba ya mizabibu ya Timna, simba* akamjia akinguruma.  Ndipo roho ya Yehova ikamtia nguvu,+ naye akampasua simba huyo vipande viwili, kama mtu anavyompasua mwanambuzi kwa mikono yake. Lakini hakumwambia baba yake au mama yake jambo alilofanya.  Kisha akaenda kuzungumza na yule mwanamke, na bado Samsoni aliona kwamba anamfaa.+  Baadaye alipokuwa akirudi kumchukua mwanamke huyo aende naye nyumbani,+ alienda kuangalia ule mzoga wa simba, nao ulikuwa na nyuki wengi na asali.  Basi akakwangua asali hiyo na kuitia mikononi mwake, akaila huku akitembea. Alipomfikia baba yake na mama yake, akawagawia ili wale. Lakini hakuwaambia kwamba aliikwangua kutoka katika mzoga wa simba. 10  Na baba yake akaenda kumwona yule mwanamke, naye Samsoni akafanya karamu huko, kwa maana hivyo ndivyo vijana wa kiume walivyokuwa wakifanya. 11  Na watu walipomwona, wakamletea vijana 30 wa kuandamana naye. 12  Kisha Samsoni akawaambia, “Nina kitendawili. Mkikitegua katika siku saba za karamu, nitawapa mavazi 30 ya kitani na mavazi mengine 30. 13  Lakini mkishindwa kukitegua, mtanipa mavazi 30 ya kitani na mavazi mengine 30.” Wakamwambia, “Tega kitendawili chako, tusikie.” 14  Basi akawaambia, “Mlo ulitoka katika mlaji,Na kitu kitamu kilitoka kwa mwenye nguvu.”+ Nao hawakuweza kutegua kitendawili hicho kwa siku tatu. 15  Siku ya nne wakamwambia hivi mke wa Samsoni: “Mshawishi mume+ wako ili atutegulie kitendawili hicho. Kama sivyo, tutakuteketeza kwa moto pamoja na watu wa nyumba ya baba yako. Je, mlitualika hapa ili mchukue mali zetu?” 16  Basi mke wa Samsoni akamlilia na kusema, “Hakika unanichukia; hunipendi.+ Uliwategea watu wangu kitendawili, lakini hujaniambia maana yake.” Samsoni akamwambia, “Hata sijamwambia baba yangu wala mama yangu! Nikwambie wewe?” 17  Lakini akaendelea kumlilia siku zilizobaki za karamu hiyo ya siku saba. Hatimaye Samsoni akamtegulia kitendawili hicho katika siku ya saba, kwa sababu alimsumbua sana. Ndipo mwanamke huyo akawaambia watu wake maana ya kitendawili hicho.+ 18  Basi siku ya saba kabla ya jua kutua,* wanaume wa jiji hilo wakamwambia hivi Samsoni: “Ni nini kitamu kuliko asali,Na ni nani mwenye nguvu kuliko simba?”+ Akawaambia: “Kama hamngelima na ng’ombe wangu mchanga,+Hamngekitegua kitendawili changu.” 19  Kisha roho ya Yehova ikamtia nguvu,+ akaenda Ashkeloni,+ akawaua watu 30, akachukua mavazi yao na kuwapa watu waliotegua kitendawili.+ Akarudi nyumbani kwa baba yake akiwa amekasirika sana. 20  Kisha wakamchukua mke wa Samsoni+ na kumpa mmoja wa wale vijana walioandamana naye.+

Maelezo ya Chini

Tnn., “mwanamke wa binti za Wafilisti.”
Tnn., “anafaa machoni pangu.”
Au “mwanasimba mwenye manyoya marefu shingoni.”
Au labda, “kabla hajaingia katika chumba cha ndani.”