Waamuzi 11:1-40

  • Mwamuzi Yeftha afukuzwa, baadaye afanywa kuwa kiongozi (1-11)

  • Yeftha azungumza na Waamoni (12-28)

  • Nadhiri ya Yeftha na binti yake (29-40)

    • Maisha ya useja ya binti yake (38-40)

11  Yeftha+ Mgileadi alikuwa shujaa hodari; mama yake alikuwa kahaba na baba yake aliitwa Gileadi.  Lakini mke wa Gileadi pia akazaa wana. Wana hao walipokua, walimfukuza Yeftha na kumwambia, “Hutarithi chochote katika nyumba ya baba yetu kwa sababu wewe ni mwana wa mwanamke mwingine.”  Basi Yeftha akawakimbia ndugu zake akaenda kuishi katika nchi ya Tobu. Na watu wazembe wakajiunga naye na kumfuata.  Baada ya muda, Waamoni wakapigana na Waisraeli.+  Waamoni walipokuwa wakipigana na Waisraeli, wazee wa Gileadi wakaenda mara moja kumchukua Yeftha kutoka katika nchi ya Tobu.  Wakamwambia hivi Yeftha: “Njoo uwe kamanda wetu ili tupigane na Waamoni.”  Lakini Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, “Je, si ninyi mlionichukia sana na kunifukuza kutoka nyumbani mwa baba yangu?+ Kwa nini mnanijia sasa mkiwa na matatizo?”  Ndipo wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, “Ni kweli, lakini sasa tumerudi kwako. Ukienda pamoja nasi kupigana na Waamoni, utakuwa kiongozi wetu na wa wakaaji wote wa Gileadi.”+  Ndipo Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, “Mkinirudisha ili nipigane na Waamoni na Yehova anisaidie kuwashinda, bila shaka nitakuwa kiongozi wenu!” 10  Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, “Yehova na awe shahidi* kati yetu na kutuhukumu tusipofanya unayosema.” 11  Basi Yeftha akaenda pamoja na wazee wa Gileadi, na watu wakamweka kuwa kiongozi na kamanda wao. Na Yeftha akasema tena masharti yake yote mbele za Yehova huko Mispa.+ 12  Kisha Yeftha akatuma wajumbe kwa mfalme wa Waamoni,+ akisema, “Nimekukosea nini hivi kwamba umekuja kuishambulia nchi yangu?” 13  Mfalme wa Waamoni akawaambia wajumbe wa Yeftha, “Nimekuja kupigana nanyi kwa sababu Waisraeli walipotoka Misri+ walichukua nchi yangu, kuanzia Arnoni+ mpaka Yaboki hadi Yordani.+ Basi sasa irudishe kwa amani.” 14  Lakini Yeftha akawatuma tena wajumbe kwa mfalme wa Waamoni 15  ili wamwambie: “Yeftha anasema hivi: ‘Waisraeli hawakuchukua nchi ya Wamoabu+ wala nchi ya Waamoni,+ 16  kwa sababu Waisraeli walipotoka Misri, walipitia nyikani hadi Bahari Nyekundu+ na mpaka Kadeshi.+ 17  Kisha Waisraeli wakatuma wajumbe kwa mfalme wa Edomu,+ wakisema, “Tafadhali turuhusu tupitie katika nchi yako,” lakini mfalme wa Edomu akakataa. Kisha wakatuma wajumbe kwa mfalme wa Moabu,+ naye pia akakataa. Basi Waisraeli wakaendelea kukaa Kadeshi.+ 18  Walipopitia nyikani, waliizunguka nchi ya Edomu+ na nchi ya Moabu. Wakapitia upande wa mashariki wa nchi ya Moabu+ na kupiga kambi katika eneo la Arnoni; hawakufika kwenye mpaka wa Moabu kwa sababu Mto Arnoni ulikuwa mpaka wa Moabu.+ 19  “‘Kisha Waisraeli wakatuma wajumbe kwa Sihoni mfalme wa Waamori, mfalme wa Heshboni, wakamwambia hivi: “Tafadhali, turuhusu tupitie katika nchi yako twende katika nchi yetu.”+ 20  Lakini Sihoni hakuwaruhusu Waisraeli wapitie katika eneo lake kwa sababu hakuwaamini, basi Sihoni akawakusanya watu wake na kupiga kambi huko Yahazi na kupigana na Waisraeli.+ 21  Kwa hiyo Yehova Mungu wa Israeli akamtia Sihoni na watu wake wote mikononi mwao, Waisraeli wakawashinda na kumiliki nchi yote ya Waamori, wakaaji wa nchi hiyo.+ 22  Basi wakamiliki eneo lote la Waamori kutoka Arnoni mpaka Yaboki na kuanzia nyikani mpaka Yordani.+ 23  “‘Yehova Mungu wa Israeli ndiye aliyewafukuza Waamori kutoka mbele ya watu wake Israeli,+ na sasa je, unataka kuwafukuza Waisraeli? 24  Je, humiliki nchi yoyote unayopewa na mungu wako Kemoshi?+ Basi kila mtu ambaye Yehova Mungu wetu amemfukuza kutoka mbele yetu, ndiye tutakayemfukuza.+ 25  Je, una nguvu kuliko Balaki+ mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu? Yeye hakushindana na Waisraeli wala kupigana nao. 26  Waisraeli walipokuwa wakikaa katika jiji la Heshboni na miji yake,*+ Aroeri na miji yake, na katika majiji yote yaliyo ukingoni mwa Mto Arnoni kwa miaka 300, kwa nini hamkuyakomboa wakati huo?+ 27  Sijakukosea, lakini umenikosea kwa kunishambulia. Yehova ambaye ni Mwamuzi+ na aamue leo kati ya Waisraeli na Waamoni.’” 28  Lakini mfalme wa Waamoni hakusikiliza ujumbe wa Yeftha. 29  Roho ya Yehova ikamjia Yeftha,+ naye akapitia Gileadi na Manase na kufika Mispe kule Gileadi,+ na kutoka Mispe akaenda kupigana na Waamoni. 30  Ndipo Yeftha akaweka nadhiri+ kwa Yehova akisema, “Ukiwatia Waamoni mikononi mwangu, 31  yeyote atakayetoka nje ya mlango wa nyumba yangu ili kunipokea nitakaporudi baada ya kuwashinda Waamoni atakuwa wa Yehova,+ nami nitamtoa kama dhabihu ya kuteketezwa.”+ 32  Basi Yeftha akaenda kupigana na Waamoni, na Yehova akawatia mikononi mwake. 33  Akawaua watu wengi kutoka Aroeri mpaka Minithi, majiji 20, mpaka Abel-keramimu. Kwa hiyo Waamoni wakashindwa na Waisraeli. 34  Mwishowe Yeftha akafika nyumbani kwake Mispa,+ na tazama! binti yake akatoka ili kumpokea, huku akipiga tari na kucheza dansi! Naye alikuwa ndiye mtoto pekee. Yeftha hakuwa na mwana wala binti mwingine ila yeye. 35  Yeftha alipomwona, akararua mavazi yake na kusema, “Ole wangu, binti yangu! Umenivunja moyo,* kwa kuwa nimesababisha uende mbali. Nimetoa ahadi kwa Yehova, na siwezi kuivunja.”+ 36  Lakini akamwambia, “Baba yangu, ikiwa umetoa ahadi kwa Yehova, nitendee kama ulivyoahidi,+ kwa kuwa Yehova amelipiza kisasi dhidi ya maadui wako, Waamoni.” 37  Kisha akamwambia baba yake, “Naomba jambo hili: Niruhusu niwe peke yangu kwa miezi miwili, acha niende milimani nikaulilie ubikira wangu pamoja na wasichana wenzangu.”* 38  Ndipo akamwambia, “Nenda!” Basi akamruhusu aende kwa miezi miwili, akaenda milimani pamoja na wasichana wenzake kuulilia ubikira wake. 39  Baada ya miezi miwili, akarudi kwa baba yake, kisha baba yake akatimiza nadhiri aliyoweka kumhusu.+ Hakufanya ngono na mwanamume yeyote. Basi kukawa na desturi* hii katika Israeli: 40  Kila mwaka, wasichana Waisraeli walienda kumpongeza binti ya Yeftha Mgileadi siku nne kwa mwaka.

Maelezo ya Chini

Tnn., “msikilizaji.”
Au “miji jirani.”
Tnn., “Umenishusha chini sana.”
Au “nikalie pamoja na rafiki zangu kwa sababu sitaolewa kamwe.”
Au “sheria.”