Kitabu cha Pili cha Wafalme 1:1-18

  • Eliya atabiri kifo cha Ahazia (1-18)

1  Baada ya kifo cha Ahabu, Wamoabu+ waliwaasi Waisraeli.  Huo ndio wakati ambapo Ahazia alianguka chini kupitia kiunzi kilichokuwa katika chumba chake cha darini kule Samaria, akajeruhiwa. Kwa hiyo akawatuma wajumbe, akawaambia: “Nendeni mkamuulize Baal-zebubu mungu wa Ekroni+ ikiwa nitapona jeraha hili.”+  Lakini malaika wa Yehova akamwambia Eliya*+ Mtishbi: “Ondoka, nenda ukakutane na wajumbe wa mfalme wa Samaria, uwaulize, ‘Je, mnaenda kutafuta ushauri kutoka kwa Baal-zebubu mungu wa Ekroni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli?+  Kwa hiyo Yehova anasema hivi: “Hutatoka katika kitanda unacholalia, kwa maana hakika utakufa.”’” Kisha Eliya akaenda zake.  Wajumbe hao waliporudi kwake, mara moja akawauliza: “Kwa nini mmerudi?”  Wakamjibu: “Kuna mtu aliyekuja kukutana nasi, akatuambia, ‘Nendeni, rudini kwa mfalme aliyewatuma mkamwambie, “Yehova anauliza hivi: ‘Je, unawatuma wajumbe waende kutafuta ushauri kutoka kwa Baal-zebubu mungu wa Ekroni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli? Kwa hiyo, hutatoka katika kitanda unacholalia, kwa maana hakika utakufa.’”’”+  Ndipo mfalme akawauliza: “Mtu aliyekuja kukutana nanyi na kusema maneno hayo alikuwaje?”  Wakamwambia: “Alikuwa mwanamume aliyevaa vazi la manyoya+ na mshipi wa ngozi kiunoni.”+ Mara moja akasema: “Ni Eliya Mtishbi.”  Kisha mfalme akamtuma mkuu wa 50 na wanaume wake 50 kwa Eliya. Mkuu huyo alipanda kwenda kumwona, akamkuta ameketi kwenye kilele cha mlima. Akamwambia: “Mtu wa Mungu wa kweli,+ mfalme anasema, ‘Shuka chini.’” 10  Lakini Eliya akamjibu mkuu huyo wa 50: “Ikiwa kwa kweli mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni,+ ukuteketeze wewe na wanaume wako 50.” Basi moto ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza pamoja na wanaume wake 50. 11  Kwa hiyo mfalme akamtuma tena mkuu mwingine wa 50 na wanaume wake 50 kwenda kwa Eliya. Akaenda na kumwambia: “Mtu wa Mungu wa kweli, mfalme anasema, ‘Shuka chini haraka.’” 12  Lakini Eliya akawajibu, “Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu wa kweli, moto na ushuke kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na wanaume wako 50.” Basi moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza pamoja na wanaume wake 50. 13  Kisha mfalme akamtuma tena mkuu wa tatu wa 50 na wanaume wake 50. Lakini yule mkuu wa tatu wa 50 akapanda, akainama na kupiga magoti mbele ya Eliya, akaanza kumsihi apate kibali mbele yake na kumwambia, “Mtu wa Mungu wa kweli, tafadhali, acha uhai wangu na uhai wa watumishi hawa wako 50 uwe* na thamani machoni pako. 14  Tayari moto umeshuka kutoka mbinguni ukawateketeza wale wakuu wawili wa kwanza wa 50 na makundi yao ya 50, lakini sasa acha uhai wangu uwe* na thamani machoni pako.” 15  Ndipo malaika wa Yehova akamwambia Eliya: “Shuka pamoja naye. Usimwogope.” Basi akainuka, akashuka na kwenda pamoja naye kwa mfalme. 16  Kisha Eliya akamwambia mfalme: “Yehova anasema hivi: ‘Uliwatuma wajumbe kutafuta ushauri kutoka kwa Baal-zebubu mungu wa Ekroni.+ Je, ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli?+ Kwa nini hukutafuta neno lake? Basi hutatoka katika kitanda unacholalia, kwa maana hakika utakufa.’” 17  Kwa hiyo akafa, kulingana na neno la Yehova ambalo Eliya alikuwa amesema; na kwa kuwa Ahazia hakuwa na mwana, Yehoramu*+ akawa mfalme baada yake katika mwaka wa pili wa Yehoramu+ mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda. 18  Na mambo mengine katika historia ya Ahazia,+ mambo aliyofanya, je, hayajaandikwa katika kitabu cha historia ya nyakati za wafalme wa Israeli?

Maelezo ya Chini

Maana yake “Mungu Wangu Ni Yehova.”
Au “nafsi yangu na nafsi ya watumishi hawa wako 50 iwe.”
Au “nafsi yangu iwe.”
Yaani, ndugu ya Ahazia.