Kitabu cha Pili cha Mambo ya Nyakati 17:1-19

  • Yehoshafati, mfalme wa Yuda (1-6)

  • Kampeni ya kufundisha (7-9)

  • Nguvu za kijeshi za Yehoshafati (10-19)

17  Na Yehoshafati+ mwanawe akawa mfalme baada yake, akaimarisha mamlaka yake juu ya Israeli.⁠  Aliweka majeshi katika majiji yote ya Yuda yenye ngome na kuweka kambi za kijeshi katika nchi ya Yuda na katika majiji ya Efraimu ambayo Asa baba yake alikuwa ameyateka.+  Yehova aliendelea kuwa pamoja na Yehoshafati kwa sababu alitembea katika njia za awali za Daudi babu yake+ naye hakutafuta Mabaali.  Kwa maana alimtafuta Mungu wa baba yake+ na kufuata* amri yake wala si mazoea ya Waisraeli.+  Yehova aliendelea kuuimarisha kabisa ufalme mikononi mwake;+ na watu wote wa Yuda wakaendelea kumpa Yehoshafati zawadi, akawa na utajiri na utukufu mwingi.+  Moyo wake ukawa jasiri katika njia za Yehova, na hata aliondoa mahali pa juu+ na miti mitakatifu*+ huko Yuda.  Katika mwaka wa tatu wa utawala wake aliwaita wakuu wake, yaani, Ben-haili, Obadia, Zekaria, Nethaneli, na Mikaya, ili wafundishe katika majiji ya Yuda.  Walikuwa pamoja na Walawi wafuatao: Shemaya, Nethania, Zebadia, Asaheli, Shemiramothi, Yehonathani, Adoniya, Tobaya, na Tob-adoniya, pamoja na kuhani Elishama na kuhani Yehoramu.+  Walianza kufundisha nchini Yuda, wakiwa na kitabu cha Sheria ya Yehova,+ nao walizunguka katika majiji yote ya Yuda wakiwafundisha watu. 10  Na falme zote katika nchi zilizozunguka Yuda zikashikwa na hofu ya Yehova, nazo hazikumshambulia Yehoshafati. 11  Wafilisti wakamletea Yehoshafati zawadi na pesa kama ushuru. Waarabu wakamletea kondoo dume 7,700 na mbuzi dume 7,700 kutoka katika makundi yao. 12  Yehoshafati akaendelea kuwa mkuu zaidi na zaidi,+ akaendelea kujenga ngome+ na majiji yenye maghala+ huko Yuda. 13  Alitekeleza miradi mikubwa katika majiji ya Yuda, naye alikuwa na wanajeshi, mashujaa hodari, Yerusalemu. 14  Walipangwa kulingana na koo zao:* mkuu wa maelfu katika ukoo wa Yuda alikuwa mkuu Adna, naye alikuwa na mashujaa hodari 300,000.+ 15  Na mkuu Yehohanani alikuwa chini ya amri yake, naye alikuwa na mashujaa hodari 280,000. 16  Na pia Amasia mwana wa Zikri aliyejitolea kwa ajili ya utumishi wa Yehova alikuwa chini ya amri yake, naye alikuwa na mashujaa hodari 200,000. 17  Na kutoka katika ukoo wa Benjamini,+ kulikuwa na Eliada, shujaa hodari, naye alikuwa na wanaume 200,000 waliokuwa na pinde na ngao.+ 18  Na Yehozabadi alikuwa chini ya amri yake, naye alikuwa na wanaume 180,000 waliokuwa tayari kwa ajili ya vita. 19  Wanaume hao walikuwa wakimhudumia mfalme pamoja na wale ambao mfalme aliwaweka katika majiji yenye ngome kotekote nchini Yuda.+

Maelezo ya Chini

Tnn., “kutembea katika.”
Angalia Kamusi.
Yaani, ukoo wa upande wa baba.