Mambo ya Walawi 13:1-59
13 Na Yehova akasema na Musa na Haruni, na kuwaambia:
2 “Ikiwa ngozi ya mwili wa mtu itatokeza upele au kigaga+ au doa na kukua katika ngozi ya mwili wake na kuwa pigo la ukoma,+ basi ataletwa kwa Haruni kuhani au kwa mmoja wa wanawe walio makuhani.+
3 Naye kuhani ataliangalia lile pigo lililo katika ngozi ya mwili.+ Nywele zilizo katika pigo hilo zikigeuka na kuwa nyeupe na pigo lionekane kuwa limepenya chini ya ngozi ya mwili wake, ni pigo la ukoma. Naye kuhani atalitazama, naye atamtangaza kuwa asiye safi.
4 Lakini ikiwa doa ni jeupe katika ngozi ya mwili wake nalo halionekani kuwa limepenya chini ya ngozi yake na nywele zake hazijageuka na kuwa nyeupe, basi kuhani atamtenga+ mwenye pigo hilo siku saba.
5 Naye kuhani atamtazama siku ya saba, na ikiwa pigo hilo linaonekana kuwa limekoma, pigo hilo halijaenea katika ngozi, kuhani atamtenga+ pia siku nyingine saba.
6 “Naye kuhani atamtazama katika siku ya saba mara ya pili, na ikiwa pigo limefifia nalo pigo halijaenea katika ngozi, kuhani atamtangaza pia kuwa safi. Lilikuwa kigaga. Naye atayafua mavazi yake na kuwa safi.
7 Lakini ikiwa pasipo shaka kigaga hicho kimeenea katika ngozi baada ya kuonekana mbele ya kuhani ili kuthibitisha utakaso wake, basi atajionyesha tena mara ya pili mbele ya kuhani,+
8 naye kuhani atatazama; na ikiwa kigaga hicho kimeenea katika ngozi, basi kuhani huyo atamtangaza kuwa asiye safi. Ni ukoma.+
9 “Ikiwa pigo la ukoma litatokea katika mtu, ataletwa kwa kuhani.
10 Naye kuhani atatazama;+ na ikiwa kuna upele mweupe katika ngozi nao umegeuza nywele kuwa nyeupe na ubichi wa nyama iliyo hai+ upo kwenye upele huo,
11 huo ni ukoma wa kudumu+ katika ngozi ya mwili wake; naye kuhani atamtangaza kuwa asiye safi. Hapaswi kumtenga,+ kwa kuwa yeye si safi.
12 Sasa ikiwa pasipo shaka ukoma huo unatokea katika ngozi, nao ukoma ufunike ngozi yote ya mtu mwenye pigo hilo toka kichwani pake mpaka miguuni pake na kuonekana kikamili machoni pa kuhani;
13 naye kuhani ametazama nao ukoma umeufunika mwili wake wote, basi atalitangaza pigo hilo kuwa safi. Lote limegeuka kuwa jeupe. Yeye ni safi.
14 Lakini siku ambayo nyama mbichi itaonekana ndani yake, atakuwa najisi.
15 Naye kuhani+ ataiona nyama hai, naye atamtangaza kuwa asiye safi. Hiyo nyama hai si safi. Ni ukoma.+
16 Au ikiwa nyama hai itarudi na kubadilika kuwa nyeupe, ndipo atakuja kwa kuhani.
17 Naye kuhani atamtazama,+ na ikiwa pigo hilo limebadilika na kuwa jeupe, ndipo kuhani atalitangaza pigo hilo kuwa safi. Yeye ni safi.
18 “Na kuhusu nyama, ikiwa jipu+ litatokea katika ngozi yake nalo lipone,
19 na mahali pa jipu patokee upele mweupe au doa jekundu-jeupe, ndipo atajionyesha kwa kuhani.
20 Naye kuhani atatazama,+ na ikiwa linaonekana kuwa limepenya chini ya ngozi na nywele zake zimegeuka na kuwa nyeupe, ndipo kuhani atamtangaza kuwa asiye safi. Ni pigo la ukoma. Limetokea katika jipu.
21 Lakini kuhani akilitazama, na, tazama sasa, hakuna nywele nyeupe ndani yake wala halijapenya chini ya ngozi na limefifia, kuhani atamtenga+ siku saba.
22 Na ikiwa pasipo shaka limeenea katika ngozi, ndipo kuhani huyo atamtangaza kuwa asiye safi. Ni pigo.
23 Lakini doa likibaki mahali pake, halijaenea, ni jipu lenye kuwasha;+ naye kuhani atamtangaza kuwa safi.+
24 “Au ikiwa ngozi ya mwili itakuwa na kovu kutokana na moto, na ubichi wa nyama wa kovu hilo uwe doa jekundu-jeupe au jeupe,
25 ndipo kuhani atalitazama; na ikiwa nywele zimegeuka na kuwa nyeupe katika doa hilo nalo linaonekana kuwa limepenya chini ya ngozi, ni ukoma. Umetokea katika kovu hilo, naye kuhani atamtangaza kuwa asiye safi. Ni pigo la ukoma.
26 Lakini ikiwa kuhani ataliangalia, na, tazama sasa, hakuna nywele nyeupe katika doa hilo nalo halijapenya chini ya ngozi nalo limefifia, ndipo kuhani atamtenga siku saba.
27 Naye kuhani atamtazama katika siku ya saba. Ikiwa pasipo shaka limeenea katika ngozi, ndipo kuhani atamtangaza kuwa asiye safi. Ni pigo la ukoma.
28 Lakini doa hilo likibaki mahali pake, halijaenea katika ngozi nalo limefifia, ni upele wa kovu; naye kuhani atamtangaza kuwa safi, kwa sababu ni kovu lenye kuwasha.
29 “Na mwanamume au mwanamke, ikiwa atapata pigo kwenye kichwa au kwenye kidevu,
30 ndipo kuhani+ ataliona pigo hilo; na ikiwa linaonekana kuwa limepenya chini ya ngozi, nazo nywele ni za manjano na ni chache ndani yake, ndipo kuhani atamtangaza kuwa asiye safi. Ni kuanguka kwa nywele kusiko kwa kawaida.+ Ni ukoma wa kichwa au wa kidevu.
31 Lakini ikiwa kuhani ataliona pigo la kuanguka kwa nywele kusiko kwa kawaida, na, tazama! linaonekana kuwa halijapenya chini ya ngozi wala hakuna nywele nyeusi hapo, ndipo kuhani atamtenga+ mwenye pigo la kuanguka kwa nywele kusiko kwa kawaida kwa siku saba.+
32 Naye kuhani atalitazama pigo hilo katika siku ya saba; na ikiwa kule kuanguka kwa nywele kusiko kwa kawaida hakujaenea, wala hakuna nywele za manjano ambazo zimekuwa hapo na kule kuanguka kwa nywele kusiko kwa kawaida+ hakujapenya chini ya ngozi,
33 ndipo atanyolewa, lakini hatapanyoa mahali palipoanguka nywele isivyo kawaida;+ naye kuhani atamtenga siku nyingine saba huyo mtu ambaye nywele zimeanguka isivyo kawaida.
34 “Naye kuhani atatazama kule kuanguka kwa nywele kusiko kwa kawaida katika siku ya saba; na ikiwa kule kuanguka kwa nywele kusiko kwa kawaida hakujaenea katika ngozi, wala haionekani kwamba kumepenya chini ya ngozi, ndipo kuhani atamtangaza kuwa safi,+ naye atayafua mavazi yake na kuwa safi.
35 Lakini ikiwa pasipo shaka kule kuanguka kwa nywele kusiko kwa kawaida kunaenea katika ngozi baada ya kuthibitishwa kwa utakaso wake,
36 ndipo kuhani+ atamwona; na ikiwa kule kuanguka kwa nywele kusiko kwa kawaida kumeenea katika ngozi, kuhani hana haja ya kuchunguza nywele za manjano; yeye si safi.
37 Lakini ikiwa kwa kuonekana kwake, kule kuanguka kwa nywele kusiko kwa kawaida kumesimama na nywele nyeusi zimeota hapo, kule kuanguka kwa nywele kusiko kwa kawaida kumepona. Yeye ni safi, naye kuhani atamtangaza kuwa safi.+
38 “Na mwanamume au mwanamke, ikiwa madoa+ yatatokea katika ngozi ya mwili wao, madoa meupe,
39 ndipo kuhani+ atatazama; na ikiwa madoa hayo katika ngozi ya mwili wao ni ya rangi nyeupe iliyofifia, ni upele usio na madhara. Umetokea katika ngozi. Yeye ni safi.
40 “Naye mwanamume, ikiwa kichwa chake kitaanza kuwa na upara,+ ni upara. Yeye ni safi.
41 Na ikiwa kichwa chake kitakuwa na upara upande wa mbele, ni upara wa paji la uso. Yeye ni safi.
42 Lakini ikiwa pigo jekundu-jeupe litatokea katika upara wa utosi au wa paji la uso, ni ukoma unaotokea katika upara wa utosi wake au paji lake la uso.
43 Naye kuhani+ atamtazama; na ikiwa kuna upele wa pigo jekundu-jeupe katika upara wa utosi wake au wa paji lake la uso unaoonekana kama ukoma katika ngozi ya mwili,
44 yeye ni mwenye ukoma. Yeye si safi. Kuhani atamtangaza kuwa asiye safi. Pigo lake lipo kichwani pake.
45 Naye mwenye ukoma ambaye ana pigo ndani yake, mavazi yake yatararuliwa,+ na kichwa chake kisitunzwe,+ naye anapaswa kufunika masharubu+ yake na kupaaza sauti, ‘Si safi, si safi!’+
46 Siku zote ambazo pigo hilo litakuwa ndani yake atakuwa si safi. Yeye si safi. Atakaa akiwa ametengwa. Makao yake yatakuwa nje ya kambi.+
47 “Kwa habari ya vazi, ikiwa pigo la ukoma litatokea ndani yake, iwe ni ndani ya vazi la sufu au ni ndani ya vazi la kitani,
48 au ndani ya mtande+ au ndani ya mshindio wa kitani na wa sufu, au ndani ya ngozi au ndani ya chochote kilichotengenezwa kwa ngozi,+
49 nalo pigo la rangi ya kijani-manjano au la rangi nyekundu-nyekundu litokee ndani ya vazi hilo au ndani ya ngozi au ndani ya mtande au ndani ya mshindio au ndani ya chombo chochote cha ngozi, ni pigo la ukoma, nalo lazima lionyeshwe kwa kuhani.
50 Naye kuhani+ ataona pigo hilo, naye atalitenga+ pigo hilo siku saba.
51 Atakapokuwa ameliona pigo hilo katika siku ya saba, ya kwamba pigo hilo limeenea katika vazi au katika mtande au katika mshindio+ au katika ngozi ambayo inaweza kutumiwa kwa ajili ya matumizi yoyote, pigo hilo ni ukoma hatari.+ Si safi.
52 Naye atateketeza vazi hilo au mtande huo au mshindio huo katika sufu hiyo au katika kitani+ hicho, au chombo chochote cha ngozi ambamo pigo hilo linaweza kutokea, kwa sababu ni ukoma hatari.+ Utateketezwa katika moto.
53 “Lakini ikiwa kuhani anatazama, na, tazama sasa, pigo hilo halijaenea katika vazi au katika mtande au katika mshindio au katika chombo chochote cha ngozi,+
54 kuhani pia ataamuru waoshe kile ambacho ndani yake mna pigo hilo, naye atalitenga mara ya pili kwa siku saba.
55 Naye kuhani atatazama pigo hilo baada ya kuoshwa, na ikiwa kuonekana kwa pigo hilo hakujabadilika na bado pigo hilo halijaenea, si safi. Utaliteketeza katika moto. Ni tundu lililo chini katika kiraka kilichochanika upande wa ndani au wa nje.
56 “Lakini ikiwa kuhani ametazama, na, tazama sasa, pigo limefifia baada ya kuoshwa, ndipo atalirarua kutoka katika vazi au ngozi au mtande au mshindio.
57 Hata hivyo, ikiwa bado linaonekana katika vazi au katika mtande au katika mshindio+ au katika chombo chochote cha ngozi, linatokea. Utakiteketeza+ motoni chochote kile ambacho ndani yake mna pigo hilo.
58 Nalo vazi au mtande au mshindio au chombo chochote cha ngozi ambacho utaosha, pigo litakapokuwa limetoweka kutoka kwake, kitaoshwa tena mara ya pili; nacho kitakuwa safi.
59 “Hiyo ndiyo sheria ya pigo la ukoma katika vazi la sufu au kitani,+ au katika mtande au katika mshindio, au katika chombo chochote cha ngozi, ili kukitangaza kuwa safi au kukitangaza kuwa si safi.”