Hamia kwenye habari

Sheria za Mungu Kuhusu Usafi Zilikuwa za Hali ya Juu

Muda mfupi kabla ya taifa la Israeli kuingia kwenye Nchi ya Ahadi karne 35 hivi zilizopita, Mungu alisema kwamba angewalinda dhidi ya “ugonjwa wowote unaotisha” walioujua nchini Misri. (Kumbukumbu la Torati 7:15) Njia moja aliyofanya hivyo ni kwa kuwapa maagizo yaliyohusisha mambo mengi kuhusu kudhibiti magonjwa na kudumisha usafi. Kwa mfano:

  • Sheria ilionyesha kwamba kuoga na kufua nguo ni lazima.—Mambo ya Walawi 15:4-27.

  • Mungu alisema hivi kuhusu kinyesi cha wanadamu: “Mahali pa faragha panapaswa kutengwa nje ya kambi, na mnapaswa kwenda kujisaidia huko. Kati ya vifaa vyenu mtakuwa na kijiti. Mnapochuchumaa nje, mnapaswa kukitumia kuchimba shimo na kisha kufunika kinyesi chenu.”—Kumbukumbu la Torati 23:12, 13.

  • Watu waliofikiriwa kuwa na magonjwa ambayo yangeweza kuambukiza walitengwa na watu wengine kwa kipindi fulani. Kabla ya kurudi kambini, wagonjwa hao waliopona walipaswa kufua nguo na kuoga ili waonwe kuwa “safi.”—Mambo ya Walawi 14:8, 9.

  • Mtu yeyote aliyegusa maiti alitengwa kwa muda.—Mambo ya Walawi 5:2, 3; Hesabu 19:16.

Sheria za Israeli zilionyesha mawazo na maoni ya kitiba kuhusu usafi yaliyovumbuliwa mapema kabla ya wakati wake.

Watu katika maeneo mengine walikuwa na viwango vya chini sana vya usafi. Kwa mfano:

  • Uchafu ulitupwa mitaani. Maji yaliyochafuliwa, chakula, na takataka nyingine zilichangia hali mbaya ambazo zilitokeza magonjwa mengi na kusababisha vifo vya watoto.

  • Madaktari zamani hawakuwa na ujuzi mwingi kuhusu viini na vitu vinavyosababisha magonjwa. Wamisri walitumia vitu kama damu ya mjusi, mavi ya ndege, panya waliokufa, mkojo, na mkate uliojaa kuvu kuwatibu wagonjwa. Pia, mara nyingi kinyesi cha wanadamu na wanyama kilitumiwa katika matibabu.

  • Wamisri wa kale walipata vijidudu kadhaa kutoka kwenye maji machafu ya Mto Nile na vijito vilivyotumiwa kunyunyizia mashamba. Vivyo hivyo, watoto wengi wachanga nchini Misri walikufa kwa sababu ya kuharisha na magonjwa mengine yaliyotokana na chakula kichafu.

Kwa upande mwingine, Waisraeli walinufaika na walikuwa na afya nzuri kuliko watu wa mataifa mengine kwa sababu ya kufuata viwango vilivyowekwa katika sheria ya Mungu.