Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Uteute wa Hagfish

 Kwa miaka mingi, wanasayansi wamevutiwa sana na uteute unaonata, unaotengenezwa na samaki anayeitwa Hagfish. Kwa nini wanasayansi wanavutiwa nao? Ute wa samaki huyo unasemekana kuwa mojawapo ya “vitu laini zaidi vinavyoweza kuvutika.”

 Fikiria hili: Hagfish anafanana na samaki anayeitwa mkunga anayeishi kwenye sakafu ya bahari. Samaki mwingine akijaribu kumla, tezi fulani za pekee za hagfish hutoa ute huo. Ute huo una protini za aina mbalimbali na zilizo na nyuzinyuzi ndefu. Protini hizi hufanya kazi kwa pamoja na kubadilisha maji yanayomzunguka hagfish kuwa uteute unaonata. Ute huo huziba mfumo wa kupumua wa samaki mwindaji, na kumlazimisha amwache hagfish mara moja.

 Ute huo ni wa pekee sana. Kila nyuzi ya protini ina upana mdogo kiasi kwamba inaweza kuingia mara mia moja katika unywele mmoja wa mwanadamu na una nguvu mara kumi zaidi ya nailoni. Samaki huyo anapotoa ute huo, unachanganyika na maji ya bahari kisha yale makamasi na nyuzinyuzi zinafanyiza muundo unaofanana na chujio lenye pembe tatu. Muundo huo unaweza kuhifadhi maji mara 26,000 zaidi ya uzito wake. Tena, jambo lenye kustaajabisha ni kwamba uteute huo unafanyizwa na maji tu karibu asilimia 100 hivi!

 Wanasayansi hawajafanikiwa kutengeneza ute wenye uwezo kama ule wa hagfish. Mtafiti mmoja anasema hivi: “Mfumo huu wa asili ni tata sana.” Wanasayansi wameazimia kutengeneza nyuzinyuzi za protini kwa kutegemea jenetiki, wakitumia bakteria. Lengo ni kutengeneza kitu chepesi, kisichokatika, kinachovutika na kinachoweza kuoza. Nyuzinyuzi za protini zilizobuniwa kiwandani zinaweza kutumika kutokeza vifaa vinavyotumiwa na madaktari na pia kutengeneza nguo. Zinaweza kutumiwa kwa njia nyingine nyingi pia.

 Una maoni gani? Je, muundo wa pekee wa ute wa Hagfish ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?