Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Uteute wa Konokono Unaonata

Kwa muda mrefu wataalamu wa upasuaji wameona uhitaji wa kupata gundi zinazoweza kuwasaidia katika upasuaji na kutibu majeraha kwenye tishu za mwili. Gundi nyingi zilizopo sasa haziwezi kutumiwa kutibu sehemu za ndani ya mwili. Zina sumu, zinakuwa ngumu zinapokauka, na hazishiki kwenye tishu zenye umajimaji. Kwa kuchunguza uteute wa konokono, * wanasayansi wamepata njia ya kutatua matatizo hayo.

Jambo la kufikiria: Konokono anapohisi kwamba yuko hatarini, yeye hutoa uteute wenye gundi yenye uwezo wa kumfanya anate kwenye jani lililolowa. Mbinu hiyo ya kujikinga humlinda konokono, huku akiwa na uwezo wa kusogea polepole.

Watafiti walichunguza uteute huo na kugundua mambo kadhaa yanayoifanya iwe gundi bora ya kiasili. Kwa mfano, uteute huo hutumia mchanganyiko wa uwezo wa kemikali kujiunganisha na nguvu za uvutano wa kielektroni. Hupenya ndani ya sehemu ambayo konokono amejipandikiza na ina uwezo wa kutanuka kunapokuwa na mkazo. Kwa kubuni gundi yenye sifa kama ya uteute wa konokono, watafiti wametokeza gundi yenye uwezo mkubwa zaidi kuliko gundi za kitiba zinazotumiwa kwa sasa ambayo ina uwezo wa kunata kwenye viungo vya mwili wa mwanadamu. Inasemekana kwamba gundi hiyo hunata “kwenye viungo vya mwili kama vile gegedu inavyonata kwenye mfupa.”

Wataalamu wanaamini kwamba gundi hiyo itakuwa sehemu ya vifaa vya kazi vya kila mtaalamu wa upasuaji, na kuondoa uhitaji wa kushona na kuunganisha kwa kutumia uzi na stepla. Inaweza kutumiwa kurekebisha gegedu au kupandikiza vifaa vya kitiba mahali hususa vinapopaswa kuwa ndani ya mwili. Tayari majaribio yamethibitisha ubora wa gundi hiyo katika kuziba shimo lililokuwa ndani ya moyo wa nguruwe na kuweka kiraka kwenye mashimo yaliyo kwenye maini ya panya.

Mara nyingi wanasayansi hupata suluhisho kwa matatizo ya kawaida kwa kuchunguza uumbaji unaotuzunguka. Donald Ingber, mkurugenzi wa taasisi iliyofanyiza gundi hiyo anasema hivi: “Unahitaji tu kujua mahali pa kutafuta na kutambua ni wazo gani linalofaa zaidi.”

Una maoni gani? Je, gundi ya asili ya uteute wa konokono ilijitokeza yenyewe? Au ilibuniwa?

^ fu. 3 Jina lake la kisayansi ni Arion subfuscus.