Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Ngozi ya Tunda la Balungi Inayoweza Kuhimili Mshtuko

Ngozi ya Tunda la Balungi Inayoweza Kuhimili Mshtuko

 Balungi ni tunda kubwa tamu la jamii ya chungwa linalokua kwenye mti. Tunda hilo halibondeki hata baada ya kuanguka mita 10 kutoka juu kwenye mti! Ni nini kinachofanya tunda hilo liwe na uwezo wa kuhimili mshtuko wa namna hiyo?

 Jambo la Kufikiria: Watafiti wamegundua kwamba sehemu nyeupe iliyo ndani ya ganda la Balungi ina chembe zenye nafasi kama za sponji. Nafasi hizo huzidi kuwa pana kuelekea ndani ya tunda, nazo zimejaa hewa au umajimaji. Kwa hiyo, tunda hilo linapoanguka chini, umajimaji huo unakuwa kama mto. Ngozi ya tunda la Balungi inasinyaa na kuwa ngumu, na kuwa imara badala ya kupasuka.

 Wanasayansi wanajaribu kubuni aina fulani ya chuma ambayo itaweza kuhimili mshtuko kama ngozi ya tunda la Balungi. Wanaamini kwamba kitu kama hicho kinaweza kutumika pia katika kubuni kofia za wanaoendesha pikipiki, vifaa vya kulinda magari wakati wa aksidenti, na vifaa vya kulinda vituo vya angani dhidi ya vimondo.

 Una maoni gani? Je, ngozi ya tunda la Balungi ilijitokeza yenyewe? Au ilibuniwa?