Hamia kwenye habari

Nifanye Nini Ikiwa Ninashinikizwa Nifanye Ngono

Nifanye Nini Ikiwa Ninashinikizwa Nifanye Ngono

“Si ni afadhali tu ukubali?” huenda ukauliza. “Kwani, si kila mtu anafanya ngono?”

Hebu tua na ufikiri!

Ukweli wa mambo: Si kila mtu anayefanya ngono.

Ni kweli kwamba huenda ukasoma kuhusu idadi kubwa ya vijana wanaofanya ngono. Kwa mfano, uchunguzi uliofanywa nchini Marekani ulionyesha kwamba kufikia wakati wanapomaliza shule ya sekondari, vijana 2 kati ya 3 nchini humo huwa wamefanya ngono. Lakini, usisahau kwamba hilo linamaanisha kijana 1 kati ya 3 hafanyi ngono—na hiyo ni idadi kubwa sana.

Lakini vipi kuhusu wale ambao wanafanya? Wachunguzi wamegundua kwamba wengi kati ya vijana hao hupatwa na angalau moja kati ya matatizo yafuatayo.

Kushuka moyo. Vijana wengi ambao wamefanya ngono kabla ya ndoa wanasema kwamba walijuta baadaye.

Kufanya ngono kabla ya ndoa ni kama kuchukua mchoro mzuri na kuutumia kama tambara la mlangoni

Kutoaminiana. Baada ya kufanya ngono kila mmoja huanza kujiuliza, ‘Amewahi kufanya ngono na nani mwingine?’

Kukosa kuona mambo kihalisi. Moyoni mwao, wasichana wengi wangependa kuwa na mtu atakayewalinda, si mtu anayetaka tu kuwatumia. Na wavulana wengi hawavutiwi sana na msichana ambaye amekubali wanachotaka.

Jambo kuu: Mwili wako ni wenye thamani sana, usiache utumiwe ovyo. Onyesha kwamba una nguvu za kutii sheria za Mungu za kujiepusha na ngono kabla ya ndoa. Kisha, utakapofunga ndoa, unaweza kufanya ngono. Nawe utaifurahia kabisa—bila wasiwasi, majuto, wala mahangaiko ambayo mara nyingi hutokea mtu anapofanya ngono kabla ya ndoa.—Methali 7:22, 23; 1 Wakorintho 7:3.