Hamia kwenye habari

VIJANA HUULIZA

Ninaweza Kupunguzaje Uzito?

Ninaweza Kupunguzaje Uzito?

 Je, kweli ninahitaji kupunguza uzito?

 Baadhi ya matineja husema kwamba wanataka kupunguza uzito. Hata hivyo . . 

 •   Wengi wao huhangaikia zaidi kuhusu muonekano wao kuliko afya yao. Ili kupunguza uzito, baadhi yao wameamua kutumia njia za kufanya hivyo kwa haraka, kama vile kutokula baadhi ya milo kwa siku au kutumia dawa za kupunguza uzito. Mara nyingi njia hizo hazina matokeo mazuri na hata ni hatari.

   “Baadhi ya wasichana hujinyima chakula ili wapate matokeo haraka. Mara nyingi njia hii haifanyi kazi, kisha huchukua muda mrefu kwa mwili wao kupona kutokana na uharibifu uliopata.”—Hailey.

 •   Wengi wanaohangaikia uzito wao hawana sababu ya kufanya hivyo. Uzito wao uko sawa—lakini labda wanajihisi wanene wanapojilinganisha na marafiki wao au watu maarufu walio wembamba katika mitandao.

   “Nilipokuwa na umri wa miaka 13, nilikuwa najilinganisha na marafiki wangu. Nilifikiri wangenipenda zaidi ikiwa ningefanana nao—hilo lilimaanisha nilihitaji kuwa mwembamba kama kijiti.”—Paola.

 Kwa upande mwingine, baadhi ya vijana wanahitaji kupunguza uzito. Kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni . . .

 •   Vijana milioni 340 hivi duniani kote, wenye umri wa kati ya miaka 5 hadi 19 wana uzito mkubwa kupita kiasi.

 •   Mwaka 1975, ni asilimia 4 tu ya watu waliokuwa na umri wa miaka 5-19 waliokuwa na uzito mkubwa mno. Kufikia mwaka 2016, idadi hiyo ilipanda hadi asilimia 18.

 •   Katika nchi nyingi duniani, ni jambo la kawaida kwa watu kuwa na uzito mkubwa sana kuliko uzito mdogo sana.

 •   Katika nchi zenye kipato cha chini, watu huwa na uzito wa kupita kiasi hata katika familia ambazo hazipati chakula cha kutosha.

 Ni njia gani bora ya kupunguza uzito?

 Utachagua njia gani?

 1.   Kutokula baadhi ya milo.

 2.   Kuchanganya mazoezi na lishe bora.

 3.   Kutumia dawa za kupunguza uzito.

 Jibu Sahihi: Njia ya 2: Kuchanganya mazoezi na lishe bora.

 Kutokula baadhi ya milo au kuacha kula aina fulani ya chakula kunaweza kuleta matokeo kwa haraka. Lakini huenda njia hizo zisiwe nzuri kwa afya yako, na labda unaweza kurudia uzito wako wa awali mara tu unapoanza tena njia yako ya kula ya kawaida.

 Kwa upande mwingine, ikiwa utaweka mradi wa kuwa na afya nzuri, utakuwa na mwonekano mzuri na utahisi vizuri. Dakt.  Michael Bradley a anasema, “Matokeo salama, bora kwa afya, na ya muda mrefu zaidi yanatokana na . . . kubadili mtindo wako wa maisha katika njia ambazo unaweza kudumisha kwa maisha yako yote. Somo? Ikiwa unahitaji kupunguza uzito, usifikiri kwamba unahitaji kuepuka vyakula fulani bali, unahitaji kubadili mtindo wa maisha.

 Hatua za kuchukua

 Biblia inatuambia tuwe “wenye kiasi katika mazoea”—na hilo linatia ndani mazoea yetu ya kula. (1 Timotheo 3:11) Hata inataja kihususa kwamba tunapaswa kuepuka kula kupita kiasi. (Methali 23:20; Luka 21:34) Ukiwa na kanuni hizo akilini, jaribu kufanya mambo yafuatayo ili upate njia bora ya maisha na afya nzuri:

 •   Jifunze kuhusu mazoea mazuri ya kula.

   Huhitaji kufuata mazoea hayo kupita kiasi, lakini kuwa na ujuzi wa kiasi kuhusu lishe bora kunaweza kukusaidia kwa muda mrefu ili uwe na mazoea ya kula lishe bora. Lishe bora ni moja kati ya njia bora zaidi za kuhakikisha unadumisha uzito mzuri.

 •   Fanya mazoezi kwa ukawaida.

   Fikiria mambo unayoweza kufanya kila siku ambayo yanaweza kuwa kama mazoezi. Kwa mfano, badala ya kupanda lifti, panda ngazi. Tumia nusu saa kwa ajili ya kutembea nje haraka badala ya kucheza michezo ya video.

 •   Badala ya vyakula visivyo na lishe, kula vyakula vyenye lishe bora.

   Tineja anayeitwa Sofia anasema hivi, “Ninajaribu kuweka karibu vitafunwa vyenye lishe kama vile matunda na mboga. Kwa njia hiyo sishawishiki kula vyakula visivyo na lishe.”

 •   Kula taratibu.

   Baadhi ya watu hula chakula haraka sana hivi kwamba wanakosa “kusikia” miili yao inaposema, inatosha! Kwa hiyo, punguza mwendo. Pumzika kwanza kabla hujaongeza chakula. Unaweza kugundua kwamba huna njaa kama unavyofikiri.

 •   Dhibiti kiasi cha kalori unachokula

   Soma vibandiko vya lishe ili ujue kiasi cha kalori kinachopatikana kwenye chakula. Dokezo: Vinywaji vilivyoongezwa sukari, vyakula visivyo na lishe vinavyopikwa haraka na vyakula vyenye sukari nyingi vinavyoliwa baada ya mlo vinaweza kuwa chanzo kikubwa cha kalori—na kuongeza uzito.

 •   Uwe na usawaziko.

   Sara mwenye umri wa miaka 16 anasema hivi, “Wakati fulani nilikuwa nahangaikia sana kuhesabu kalori hivi kwamba kila nikiangalia sahani ya chakula ninachoona ni namba tu!” Usiwe “mhasibu wa kalori.” Nyakati fulani unaweza kujiruhusu kufurahia vyakula vyenye sukari.

 Pendekezo: Zungumza na daktari wako kuhusu uzito wako. Anaweza kuzingatia hali yako ya kiafya na kukusaidia kubadili mtindo wa maisha kwa njia ambayo itakufaa.

a Kitabu When Things Get Crazy With Your Teen.