Hamia kwenye habari

VIJANA HUULIZA

Nifanye Nini Nikinyanyaswa Mtandaoni?

Nifanye Nini Nikinyanyaswa Mtandaoni?

 Unachopaswa kujua

 Intaneti inafanya iwe rahisi kunyanyaswa. Kitabu CyberSafe kinasema: Intaneti “inawafanya hata watoto wenye tabia nzuri wawe wanyanyasaji kwa sababu hawawezi kuonekana na wale wanaonyanyaswa.”

 Ni rahisi kuwalenga watu fulani. Watu wanaojitenga, wanaonekana tofauti na wengine, au wasiojiamini.

 Kunyanyaswa mtandaoni kuna madhara makubwa. Kunaweza kuongeza upweke na kushuka moyo, na kunaweza hata kusababisha baadhi ya wale wanaonyanyaswa wajiue.

 Unachoweza kufanya

 Kwanza, jiulize hivi: ‘Je, kweli ninanyanyaswa?’ Wakati mwingine watu wanasema mambo ya kuumiza lakini kihalisi hawamaanishi wanachosema. Ukipatwa na hali kama hiyo unaweza kufuata ushauri wenye hekima wa Biblia unaosema hivi:

 “Usikasirike haraka, kwa maana hasira ni dalili ya mjinga.”​—Mhubiri 7:9, maelezo ya chini.

 Kwa upande mwingine ikiwa mtu anamsumbua, anamfedhehesha au kumtisha mtu mwingine kimakusudi mtandaoni. Huo ni unyanyasaji.

 Ikiwa unanyanyaswa, kumbuka jambo hili: Jinsi unavyokabili mnyanyaso huo kunaweza kuwa na matokeo mazuri au mabaya. Jaribu kutumia pendekezo moja au mawili kati ya mapendekezo yafuatayo.

 Mpuuze mnyanyasaji. Biblia inasema hivi: “Mtu mwenye ujuzi huyazuia maneno yake, na mtu mwenye utambuzi atabaki mtulivu.”​—Methali 17:27.

 Sababu moja inayofanya ushauri huu uwe na mafanikio: Nancy Willard aliandika hivi katika kitabu chake Cyberbullying and Cyberthreats: “Kusudi kuu la mnyanyasaji ni kumfanya mtu anayelengwa awe na wasiwasi. Ikiwa anayenyanyaswa atakuwa na wasiwasi, basi mnyanyasaji atakuwa ameshinda.”

 Jambo kuu: Wakati mwingine ni bora kutochukua hatua yoyote.

 Epuka mtazamo wa kulipiza kisasi. Biblia inasema hivi: “Msilipe ubaya kwa ubaya au matukano kwa matukano.”​—1 Petro 3:9.

 Sababu moja inayofanya ushauri huu uwe na mafanikio: Kitabu Cyber-Safe Kids, Cyber-Savvy Teens kinasema hivi: “Kuwa na hasira ni kuonyesha udhaifu ambao utafanya unyanyaswe zaidi.” Kulipiza kisasi kunaweza kufanya ionekane kwamba wewe umechangia tatizo hilo kwa kiwango kilekile kama yule anayekunyanyasa.

 Jambo kuu: Usiongeze mafuta kwenye moto.

 Jilinde. Biblia inasema hivi: “Usiache ushindwe na uovu.” (Waroma 12:21) Kuna mambo unayoweza kufanya ili kukomesha unyanyasaji​—bila kusababisha madhara makubwa zaidi.

 Kwa mfano:

  •    Zuia namba ya mtu anayekutumia ujumbe wa kukunyanyasa. Kitabu Mean Behind the Screen kinasema hivi: “Huwezi kuumizwa na kitu usichosoma.

  •   Hifadhi ushahidi wote, hata kama hutausoma. Ushahidi huo unatia ndani ujumbe wa jeuri kupitia ujumbe mfupi wa simu, Intaneti, barua pepe, vitu vilivyotumwa katika mtandao wa kijamii, ujumbe wa sauti, au aina yoyote ya mawasiliano.

  •   Mweleze mnyanyasaji aache. Tuma ujumbe thabiti lakini usioonyesha hisia zozote, kama vile:

    •  “Usitume ujumbe mwingine.”

    •  “Ondoa kitu ulichotuma kwenye mtandao wa kijamii.”

    •  “Ikiwa hutaacha, nitachukua hatua nyingine ili kuhakikisha unaacha.”

  •   Jiamini. Kazia uangalifu uwezo wako badala ya udhaifu wako. (2 Wakorintho 11:6) Kama wanyanyasaji wengine, wale wanaotumia mtandao pia huangalia watu wanaoonekana kuwa rahisi kunyanyaswa.

  •   Mweleze mtu mzima. Anza na wazazi wako. Unaweza kutoa taarifa kwenye tovuti au shirika linalotoa huduma ya Intaneti ambayo mtu anayekunyanyasa anatumia. Kama hali ni mbaya sana, wewe na wazazi wako mnapaswa kutoa taarifa kuhusu hali hiyo shuleni, polisi, au kutafuta msaada wa kisheria.

 Jambo kuu: Sasa una hatua kadhaa unazoweza kuchukua ili kuzuia usisumbuliwe au kupunguza kwa kiasi fulani madhara ya kunyanyaswa mtandaoni.